Mwongozo wa bustani za maua za kwenye vyungu
Hata kama una eneo dogo kiasi gani lakini unapenda bustani za maua, unaweza
ukatimiza tamanio lako hilo kwa kutengeneza bustani za maua za kwenye vyungu.
Au pengine labda una eneo la kutosha kuwa na bustani ya ardhini lakini
bado kuna yale maeneo kama ukutani, ndani ya nyumba au kwenye varanda ambapo
ungependa kuwa na maua, basi suluhisho ni bustani za kwenye vyungu.
Bustani hizi zinakuwezesha kutengeneza bustani maalum kwa ajili ya eneo
lolote. Unaweza kuotesha humo maua yako ya upendeleo ambayo usingependa
kuotesha kwenye eneo kubwa la bustani ya ardhini kwani labda yatamezwa na mimea
mingine iliyopo kwenye bustani husika. Mtunza bustani wa bustani za kwenye
vyungu kikomo chake ni ubunifu wake pekee, anasema landscaper Aisha Idd.
Kwenye makala hii bi Aisha atatufunza jinsi ya kuchagua vyombo vya
kuoteshea, uwekaji wa mbolea, udongo na umwagiliaji wa bustani zako bila
kusahau maua yanayofaa kuotesha kwenye vyungu na mengine mengi!
Baadhi ya vyombo vinavyoweza kutumika kwenye bustani za kwenye vyungu
ni vyungu vidogo vya kuning’iniza na vile vikubwa vya kuweka chini pamoja na
maboksi ya mbao.
Aisha
anatupa mwongozo wa namna ya kuchagua vyungu kwa ajili ya bustani yako hiyo. Anasema
epuka vyungu vyenye midomo myembamba. Pia vyungu vya plastiki nyembamba sana
vinaweza kuharibiwa na jua na vitafanya ua lililoko ndani kukaukiwa na maji
mara kwa mara. Kama utachagua vyungu vya udongo fahamu kuwa udongo unapitisha
maji hivyo kiasi cha mji kitakuwa kinapotea kupitia kuta za chungu. Vyungu vya seramiki
na saruji ndio vizuri zaidi kwenye kuhifadhi maji ila vinatakiwa kuwa na
matundu kadhaa.
Maboksi ya
mbao huenda yakaoza, mbao nyekundu na za aina ya cedar huwa haziozi na zinaweza kutumika bila tatizo. Maboksi ya
mbao zilizowekwa dawa ya kuzuia kuoza au kuliwa na wadudu si mazuri kwani
kemikali zlizopo kwenye dawa hizo huwa zinaweza kuunguza maua. Uzuri wa
mabokisi ya mbao ya kuoteshea maua ni kuwa yanaweza kutengenezwa kwa umbo na ukubwa
utakaofiti eneo linalohitajika kuwekwa.
Vyungu viwe na ukubwa wa wastani
kwani vikiwa vidogo sana vitazuia mizizi ya mmea kutambaa vizuri na pia huwa
vinakauka maji mapema sana. Ukubwa na idadi ya mimea inayooteshwa itatokana na
ukubwa wa chungu kitakachotumika. Maua yenye mizizi inayoenda chini inahitaji
vyungu virefu. Hakikisha kuwa vyungu vyako vinapitisha maji vizuri na tandika
magazeti chini ili kuzuia udongo usiwe unakimbia chungu wakati wa kukimwagilia.
Sasa utajiuliza hayo magazeti si yataloa? Ni kweli ila hata kama yakiloa
yatatengeneza kizuizi chini kwani hama tujuavyo ni kuwa karatasi haiozi. Kwa upande
wa vyungu vidogo vya kuning’iniza hakikisha ya kuwa hutundiki kwenye ukuta
wenye jua la moja kwa moja kwani vitakuwa vinakaukiwa maji mara kwa mara.
Hakikisha kuwa chombo chako cha
kuoteshea bustani za kwenye vyungu kinapitisha maji mapema lakini kinahifadhi
unyevu wa kutosha kuweka mizizi katika hali ya maji. Mboji inafanya udongo
mzuri sana wa kwenye vyungu. Ila ni muhimu kujua hitaji la mmea kwani usijezidisha
udongo wenye mbolea kali, na pia mbolea nyingine kama ya kuku ina tindikali
sana kwahivyo inahitaji maji kwa wingi pindi unapoiweka. Kadri utakavyokuwa
unamwagilia mmea wako ndivyo utkavyokuwa unaweka mbolea kwani huwa maji
yanaondoa baadhi ya vimeng’enyo. Pia kuna mbolea za dukani za maji maji ambazo
waweza tumia kwa kupata maelezo ya kitaalam toka kwa wauzaji.
Umwagiliaji wa bustani yako ya kwenye vyungu
ufanyike pale mmea unapohitaji maji kwa maana ya ikiwa dalili za hali ya
kunyong’onyea zitaanza kujitokeza. Baadhi ya mimea inaweza kuvumilia na
inahitaji ukame kiasi kwamba ukiimwagilia mara kwa mara unaisababishia kuwa na
unyevu wakati wote kwa maana hiyo itakufa. Ielewe mimea uliyo nayo, anasema
Aisha. Kuna mimea mingine ya kwenye vyungu kwa mfano, kama iko ndani ya nyumba
inaweza kumwagiliwa vikombe viwili tu kwa juma zima. Kumwagilia kuwe ni hitaji
na sio jambo la kila wakati na kanuni kuu ya kujua kuwa mmea unahitaji maji ni
kujaribu udongo wake. Kama inchi moja au zaidi ya udongo ni mkavu basi
mwagilia.
Kwenye mazingira ya uwazi, mimea ya
kwenye vyungu inapoteza maji mapema. Wakati wa kiangazi bustani zilizowekwa
kwenye mazingira haya huenda zikahitaji kumwagiliwa kila siku. Sasa basi, ni muhimu kufahamu kuwa sio kila
maua au mmea unafaa kuoteshwa kwenye vyungu. Mimea inayokubalika zaidi kwa
bustani hizi ni ile yenye mizizi michache na mifupi. Pindi uendapo kwenye
bustani za wauza maua zilizojaa maeneo mengi kando kando ya barabara kuu
watakufahamisha.
Umaarufu wa bustani za
kwenye vyungu umetisha.
Mimea kwenye vyungu inaonekana kila mahali,
kutoka kwenye makazi ya watu hadi maofisini, mahotelini, kwenye ma mall na hata barabarani. Udongo mbaya au hakuna eneo la
kuweka bustani sio kisingizio tena cha kutokuweza kufurahia kijiraha cha kuwa
na bustani!
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye
ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment