Kila mmoja anapenda usingizi wake, na
tunategemea godoro kutupatia mahali safi na nyororo pa kulala. Ni nini
kinafanyika pale godoro lako linapokuwa chafu? Ni kwa namna gani unazuia mavumbi
na wadudu kuweka makao kwenye godoro lako na kukubughudhi na usingizi wako? Ni
ratiba gani ya matunzo na usafi godoro inahitaji?
Kama inavyofahamika kwamba
binadamu anatumia theluthi moja ya maisha yake akiwa amelaza mwili mlalo na
tena wengi wetu juu ya godoro, basi ungetegemea kwamba kusafisha godoro
ingekuwa ni orodha namba moja kati ya vitu vinavyopewa kipaumbele kwenye orodha
ya kusafisha, lakini utashangaa wala siyo. Ni mara chache tunafikiria juu ya
kusafisha godoro.
Tatizo ni kuwa, unaondoa
shuka zote, unabakiwa na godoro ambalo limeshionewa foronya ambayo huwezi kuivua
sio – kama vile kuna zipu unayoweza tu ukafungua kirahisi ukavua foronya na
kwenda kuifua – hapana, ukweli wa masikitiko ni kuwa – wakati tunatoa shuka
zote, tunakuwa kama tumeziba macho kwa uchafu mwingine wowote uliopo juu ya
godoro lenyewe.
Godoro linaweza kuhifadhi
uchafu wa vimiminika, madoa, vumbi na mbaya zaidi hata wadudu kama chawa na
kunguni – kwahivyo kuwa na godoro safi ni
muhimu kwa sababu kadhaa zaidi ya kufahamu kuwa mwili ambao umevalishwa nusu
unalilalia kukiwa na shuka pekee iliyotenganisha mwili huo na godoro.
Kusafisha godoro kwa mashine
ya kunyonya vumbi ni muhimu kwa ajili ya kuondoa vumbi, seli za ngozi zilizokufa
na uchafu mwingine unaotua kwenye godoro lako na ambao unajilimbikiza kadri
muda unavyokwenda. Fikiria kusafisha godoro kwa namna hii kwa walau mara mbili
kwa mwaka. Sasa kumbuka kuwa kwa vile mashine hii ya kusafishia kwa upepo ina
vichwa kadhaa, utapaswa kutumia kile kichwa cha kusafishia viti na sio kile cha
kawaida cha kusafishia zulia kwa huwa kinazoa kila aina ya uchafu kwa hivyo
usingependa kukipitisha hicho kwenye godoro lako. Wakati wa kusafisha godoro ni
vyema kusafisha pia mvunguni.
Vile vile kila baada ya miezi sita iwe ni
wakati wa kugeuza godoro lako juu kwenda chini na miguuni kwenda kichwani. Fikiria
kwa mfano mwenzi wako na wewe mna zaidi ya kilo mia, kwa hivyo kwa kugeuza na kuzungusha
godoro inamaanisha kuwa mnaongeza uhai wake na kuleta uwiano wa uchakavu . Kulingana na ukubwa wa godoro, hii kwa kirahisi kabisa
inaweza kuwa kazi ya watu wawili.
Madoa kama ya mapatapishi, jasho,
damu, mkojo na vimiminika vingine toka mwilini huwa kuna wakati vinatua kwenye
godoro. Kama ilivyo ada kwa doa lolote, ni vyema kulichangamkia liondoke mapema
kabla halijakomaa zaidi. Madoa ya vimiminika yanatakiwa kwanza yafutwe kwa maji
baridi, na kitambaa chenye unyevu. Na baadaye unyevu wa ziada unakaushwa na
kitambaa kikavu. Kumbuka kufuta kwa kukandamiza badala ya kuzungusha mduara ili
kuondoa uwezekano wa kuchana kitambaa cha godoro. Madoa haya ya viminika toka
mwilini asili yake ni protini kwa hivyo tumia maji ya baridi pekee wakati wa
kuondoa madoa haya.
Funika godoro lako kwa
foronya ya kuvulika ili kulinda maeneo ya godoro. Chagua foronya ambayo
inaosheka kirahisi ambayo ni rahisi kuvalisha na kuvua kwenye godoro lako. Foronya
nyingine zimebuniwa maalum kwa kazi ya kuzuia kushika vumbi kwa hivyo
kukupunguzia kazi ya kunyonya godoro vumbi mara kwa mara.
Kama maeneo ya godoro yamepatwa na
tope au udongo ondoa kwa shampoo ya kusafishia sofa na mazulia. Safisha tu lile
eneo lililochafuka kwa kutumia sponji. Suuza eneo hilo kwa sponji jingine la
maji ya moto na kandamiza eneo hilo kwa kitambaa kikavu ili kunyonya unyevu.
Unaweza kuruhusu eneo hilo kukauka kwa kuwasha feni au hata kutoa godoro nje
kwenye jua kali. Usiruhusu maji kuzama sana ndani kwenye kiini cha godoro kwani
maji na godoro sio marafiki.
Endapo godoro litakuwa makazi ya wadudu kama chawa na kunguni jambo hili
si dogo eti wadudu hawa waondolewe tu na watu hapo nyumbani ambao sio wataalam
wa kazi hii. Changamka mapema na mwite mtaalam. Watakusafishia na kupuliza dawa
godoro lako chumba, na hata maeneo mengine ya makazi yako ambayo yatakuwa
yamedhurika na wadudu hawa. Kama umefikiwa na wadudu hawa unataka waondoke na
wataalam wanajua jinsi ya kufanya kazi yao.
Hongera kwa kuwa na dogoro safi ambalo litadumu muda mrefu!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment