Jinsi
ya kuchagua, kuhifadhi na kutunza visu vyako vya jikoni
Visu ni vifaa muhimu zaidi jikoni. Kwanza tuangalie
muonekano wa jumla wa kisu kinachofaa jikoni ambacho tunaweza kukiita ni kisu
cha mpishi. Kisu hiki ni kile ambacho walau unakitumia kwa kila shughuli
unayofanya hapo jikoni. Ni muhimu sana kufahamu urefu na upana endapo utakuwa
unataka kununa kisu hiki. Kisu cha mpishi kina urefu wa kati ya inchi 8 hadi 12
na upana wa kati ya inchi 1 ½ hadi 2.
Kisu cha mpishi kikiwa na urefu huu wa inchi 8 ni
mwake kwa matumizi mengi tofauti tofauti kwani kikiwa kirefu sana huenda
usiweze kutumia ncha yake vizuri. Mkono wa kisu cha mpishi unaweza kuwa
umetengenezwa kwa vifaa na miundo mbalimbali. Vifaa na miundo ya aina fulani ni
rahisi kushikika mkononi kuliko aina nyingine. Mikono mingine ya visu hivi
inaweza kuwa inateleza wakati wa kukata chakula na hivyo kuleta usumbufu kwako.
Sasa haya yote yakiwa yameshasemwa, basi ni juu yako kuchagua kisu cha mpishi
ambacho utajisikia huru, burudani na rahisi kwako wewe mpishi kukitumia. Unajua
jinsi panavyokuwa na visu kadhaa jikoni lakini unakuwa na kimoja ambacho
unakipenda zaidi kwa maana ya kwamba unaona kinakufaa zaidi kwa matumizi.
Unapaswa kuwa na kati ya visu 3-5 jikoni kwako. Aina
hizi tofauti tofauti zinapatikana kwenye seti ya visu. Hakikisha unachunguza
kwa makini aina ya visu iliyopo kwenye seti endapo utakuwa unanunua kwa seti. Mara
nyingi utakuta kule kwenye seti kuna aina ya kisu ambacho utakitumia mara
chache sana ua hata labda hutakitumia kabisa. Kama ni hivyo basi ni bora kunua
kimoja kimoja badala ya seti. Hata hivyo, faida mojawapo ya kununua visu kwa
seti ni kuwa unapata na kihifadhio chake ambacho unaweza kutunzia visu vyako.
Kama unafanya kazi nyingi na nyama yenye mifupa au
samaki wazima wazima basi fikiria kuwa na kisu kile ambacho sehemu ya kukatia
ni kama msumeno kwa ajili ya kupenya kwenye mifupa na kingine kilicho laini kwa
ajili ya kukatia minofu iliyotenganishwa toka kwenye mifupa.
Usalama na usahihi wa kuhifadhi visu vyako ni jambo
la muhimu mno unalopaswa kuzingatia. Visu vikali kamwe visihifadhiwe vimesambaa
kwenye droo la kabati la jikoni vikiwa
vinagongana na vyombo vingine kwa sababu kuu mbili:
Kwanza ni hatari kuingiza mkono wako kwenye droo
kuchukua kisu kwani kinaweza kukukata, na pili msuguano wa visu na vyombo
vingine kwenye droo vinaweza kusababisha visu kuwa butu.
Kitufe cha kuhifadhia visu au kipande cha sumaku
kilichowekwa ukutani ni njia sahihi zaidi za kuhifadhi visu vyako vya jikoni.
Kama hauna eneo la kaunta kwa ajili ya kuwekea kitufe cha visu au labda hauna
ukuta kwa ajili ya kuwekea hiki kipande cha sumaku basi kwenye droo pekee ndio
mahali unapoweza kuhifadhi visu vyako. Yaani droo liwe ni chaguo la mwisho
baada ya kitufe na sumaku kushindikana. Kwa hali hii inabidi uwe na zuio la
visu ukiwa umevalisha kwenye kila kisu au droo la mbao liliogawanywa visehemu
vidogo dogo ndani kwa ajili ya kila kisu
kuhifadhiwa kwenye kisehemu chake.
Kwa hivyo tumeona kwamba utunzaji wa visu unaenda
sambamba na uhifadhi sahihi. Visu vinatakiwa kusafishwa kwa mikono na kufutwa
kabla ya kuhifadhiwa. Kwa vyovyote vile kisu chochote kitahitajika kunolewa
baada ya kipindi fulani. Unaweza kufanya shughuli hii kwa kumshirikisha mtaalam.
Baadhi ya wataalam huwa wanapita mitaani na baiskeli wakiwa wamebeba mashine zao
za kunolea huku wakitangaza wananoa visu.Vinginevyo unaweza kuamua kufanya kazi
ya kunoa visu vyako mwenyewe nyumbani. Kama utaamua kufanya mwenyewe basi kifaa
kingine cha kufikiria ni hicho cha kunoa visu vyako. Wengine huwa hata na jiwe
la kunokea visu ambalo linatumia ama mafuta au maji kama kilainishi wakati wa kunoa.
Lakini aina nyingine za vinoleo vinavyouzwa madukani havihitaji vilainishi na
vinoleo hivi ni rahisi zaidi kutumia kuliko jiwe.
Natumai umejifunza jambo kuhusu ununuzi, matumizi na
uhifadhi wa visu vyako vya jikoni. Tukutane tena wiki ijayo.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au
christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment