Monday, February 8, 2016

Kutoka Kwa Mdau: FANYA HAYA ILI PAA LA NYUMBA YAKO LIDUMU


Kati ya vitu vyote unavyozingatia wewe mwenye nyumba wakati unapotazama nyumba yako, kukagua, kusafisha na kupaka rangi paa linaweza kuwa ni kitu cha mwisho. Nimeona watu wakipendezesha nyumba ndani, nje na bustani lakini paa likisahaulika. Ingawa huenda paa si kipaumbele chako kati ya vitu unavyotazama kwenye utunzaji wa nyumba, bado haimaanishi kwamba halitakiwi kutunzwa na kuwa na muonekano wa kuvutia. Nyumba yako bila shaka ni
moja kati ya rasilimali za thamani zaidi ulizonazo, unapaswa kuitunza kwa kuzingatia maeneo yote yanayoihusu. Kuita wataalamu wenye uzoefu wa matunzo ya paa kila baada ya kipindi ni jambo muhimu.

Mtaalam wa mambo ya paa bwana Philemon Nkane anatueleza kwa kina kuhusu utunzaji wa paa. Anasema kwanza kabisa ni vyema ifahamike kuwa utunzaji wa paa unahusisha pande mbili, wa kwanza ni mwenye nyumba na wa pili ni mtaalam.

Umakini mkubwa unatakiwa wakati wowote wa kufanya kazi kwenye paa. Kutembea juu ya paa ni hatari, kwahivyo mwenye nyumba usie mtaalam wa kazi hiyo hutakiwi kupanda juu ya paa. Vinginevyo unaweza kulitazama ukiwa eneo tambarare kama pale juu ya zege la varanda. Laa kama haiwezekani kabisa basi muite mtaalam. 

Zifuatazo ni dondoo za jinsi ya kutunza paa ili lidumu muda mrefu:

Mwenye nyumba unatakiwa kuhakikisha kuwa matawi ya miti yanapunguzwa kiasi kwamba hayafikii mfumo wa paa, kwani majani kudondoka na kuozea juu kunachangia kuliharibu.

Mifereji ya maji ya mvua iliyopo kwenye paa na inayolizunguka inapaswa kusafishwa na kuzibuliwa ili ibaki wazi kwani takataka kusimama ndani zikiunganika na maji itasababisha mafuriko ya paa hivyo uharibifu.

Ukarabati wa paa hasa la vigae ni muhimu sana kwani vipo vinavyopata nyufa bila mwenye nyumba kuwa na habari. Kuviondoa mapema inasaidia paa lisiingize maji na kuharibu dari hatimaye vitu ndani. Kama hujawahi kuita mtaalam wa kukagua paa lako kwa zaidi ya miaka  8-10 ni muhimu kufanya hivyo ambapo huenda kuna marekebisho ya kufanyika haraka.

Endapo paa limeota ukungu lisafishwe kwa dawa ya kuua fangas na maji yenye msukumo mkubwa, na hata ikiwezekana lipake rangi upya. Waite wataalam wanaohusika na kazi hii watakushauri.

Wakati wa kusimika vifaa kwenye paa kama vile vifaa vya umeme jua au dishi la satelaiti hakikisha pamoja na wataalam hao, pia anakuwepo mtaalam wa paa.

Muite mtaalam haraka sana pale unapohisi paa linavuja kwani dalili ya kwanza ni kuona sehemu ya dari ikibadilika rangi na hapo ndipo marekebisho yatahitajika haraka.

Paa linapokuwa salama mwenye nyumba naye anakuwa salama. Litunze lidumu.


Je unahitaji ushauri wowote tuchat kuhusu mapambo ya makazi yako, kuna mahali panakutatiza? Utalipia mara moja tu na tutachat hadi matatizo yako yaishe bila kujali itachukua muda gani. Unatakiwa kuwasiliana na mimi simu 0755 200023.

No comments:

Post a Comment