Monday, February 22, 2016

Namna ya kukabiliana na changamoto ya kusambaa midoli ndani ya nyumba

Je wewe ni mzazi na una lundo la midoli kila mahali kwenye nyumba yako? Kama unahisi swali hili linakugusa basi sio wewe peke yako mwenye changamoto hii. Ni asili kwa mzazi kupenda kumnunulia mwanae midoli na michezo mbalimbali ya kidigitali na elektroniki inayoendana na wakati, na hasa kwenye siku ya kuzaliwa au sikukuu ndipo inakuwa mingi zaidi.

Nimeshuhudia nyumba zenye watoto ambapo midoli na
michezo imesambaa kila mahali, sio tu inaonekana kama janga ndani ya nyumba, bali pia ni hatari kwani unaweza ukaikanyaga kwa bahati mbaya ikakuangusha au hata kukutegua mguu.

Maisha yetu ya mchakamchaka hayatoi muda mwingi sana wa kuweka mpangilio ndani ya nyumba zetu. Na kazi hiyo saa nyingine inachosha manake unakusanya midoli na hapohapo watoto wanairudisha tena walikoitoa, usicheke! Najua wazazi na walezi wengi hii inawachosha.

Kuna suluhisho rahisi la changamoto hii ya kuhifadhi midoli na michezo ya watoto kwa kuwa na vifaa vya kukuwezesha kuweka mpangilio, ambapo wanao watakuwa sehemu ya sebule na kuifurahia  lakini sio kuiteka yote kwa kusambaza midoli na michezo yao kila mahali. Kuleta uwiano huu unahitaji vifaa kadhaa vya fenicha ambavyo huenda baadhi tayari unavyo.

Tenga eneo la kabati linaloweza kuhifadhi mrundikano wa midoli hiyo ambapo likiwa limefungwa haionekani. Linaweza kuwa kabati kubwa au hata fupi tu. Ukishakuwa na eneo hili basi ndani yake weka vikap au vitenga vidogo dogo kwa ajili ya watoto kuwekea ile midoli na michezo wanayotaka kuchezea kwa wakati huo.

Kama umewachunguza watoto kwa karibu ni kwamba hawachezei midoli yote kwa wakati  mmoja, huwa wanachagua kadhaa. Kwahivyo wape maelekezo kuwa wanayotaka kuichezea ndio waweke kwenye vikapu, kama ni mtoto zaidi ya mmoja kila mmoja awe na kikapu chake. Mingine ibaki kabatini. Uwe tu na vikapu vya kutosha kwenye kabati hata kama hawavitumii kwa wakati huo, ila wawekee kanuni kuwa kila mmoja awe na kikapu kimoja kwa wakati mmoja.

Mara wanapomaliza kucheza kila wakati uwe unawasisitiza kurudisha midoli yote kwenye vikapu na kuimimina kabatini, watakaporudi tena kwenye michezo watachukua vikapu vitupu wachambue tena upya wanayotaka.

Nakushauri pia ni muhimu kuwa na kabati la luninga lenye nafasi kwa ajili ya kuhifadhi midoli na michezo midogogogo.
Ukiwa na sehemu hii inakusaidia kuondoa mrundikano wa midoli sebuleni au chumba cha luninga. Kama huna kabati la namna hii na tayari ulishasimika luninga yako ukutani ni rahisi kutengeneza fenicha ndogo ya bei nafuu na ukaiweka chini ya dirisha au kwenye kona kwa ajili ya kuhifadhia midoli hiyo. Na fenicha ya namna hii iwe na muonekano wa kitoto ndipo watapenda zaidi kuitumia.

Angalia ndani ya nyumba yako kwa jicho la ziada. Kama midoli na michezo imesambaa kila mahali kama vile ni darasa la chekechea, inawezekana ni muda unaotakiwa kufanya mabadiliko. Unaweza ukawa na nyumba nadhifu yenye mpangilio na watoto wenye furaha na michezo yao kwa wakati mmoja. Ikiwa hivi bila shaka utafurahia unapoishi.


Vivi ambaye ni mshauri wa mapambo ya nyumba, simu 0755 200023

ni follow instagram @vivimachangehomes

No comments:

Post a Comment