Kama
umeshagundua ni kwamba watu wengi wanajitetea kuwa hawana mpangilio ndani ya
nyumba zao kwa ajili hawana muda wa kufanya hivyo. Na pengine hata wewe
unayesoma hapa sasa hivi una sababu hiyohiyo. “Ooh napenda sana kuweka mpangilio
na kuondoa mrundikano wa vitu lakini muda sina”.
Ni
kweli watu wana pilika na
shughuli nyingi pengine ni kazini, au kwenye jamii,
muda na familia au pia labda ni matukio ya kujifurahisha binafsi. Ndio maisha!
Kwahivyo tunafanyaje sasa wakati tunapotaka kupangilia nyumba zetu lakini hakuonekani
muwa na muda wa kutosha kufanya hivyo?
Kwanza
kabisa tenga dakika 15 tu kila siku.
Haijalishi
tuko na shughuli kiasi gani, karibia kila mmoja wetu anaweza kupata dakika 15
kwenye ratiba yake ya siku. Ndio inaweza kuwa ni kupunguza muda unaokuwa kwenye
mitandao ya kijamii, au inaweza kumaanisha ni kuamka mapema dakika kadhaa kabla
au kwenda kulala ukiwa umechelewa dakika kadhaa . Ila nikuambie ukweli kuwa
kama unaweza kujitolea dakika 15 kila siku kwa ajili ya kuweka mpangilio, utapata
matokeo makubwa baada ya kipindi fulani.
Hatua
ya pili ni tengeneza orodha.
Chukua
kalamu na karatasi na andika maeneo ambayo unatakiwa kuweka mpangilio. Na kama
eneo unaona litahitaji zaidi ya dakika 15 basi ligawe katika maeneo madogodogo.
Kwa mfano kama ni eneo la jikoni unaweza kuligawa katika maeneo madogo kama
vile mpangilio kwenye jokofu, kwenye droo ya vijiko, kwenye kabati la vikontena
na kadhalika.
Inawezekana
maeneo mengine yakahitaji kupangiliwa zaidi ya mara moja.
Hatua
ya tatu ni tegesha muda.
Kila
siku kwenye zile dakika zako 15 chagua eneo moja kwenye orodha yako la kuweka mpangilio.
Endapo dakika 15 zitaisha kabla hujamaliza na ukajikuta kwamba huwezi kuongeza
dakika hata moja basi acha utamalizia kesho yake.
Hatua
ya nne ni chambua ipasavyo.
Unapotumia
dakika zako 15 kuweka mpangilio hakikisha unaangalia kila kitu kwa kina. Kwa
mfano kama kuna vitu ambavyo vimevunjika, vina madoa au vimechakaa vitupe. Kama
kuna kitu ambacho hutumii tena lakini kiko kwenye hali nzuri bado, kigawe.
Tenga boksi kwa ajili ya hivi vitu vya kugawa na mara linapojaa peleka kwenye
vituo vya watoto yatima au safirishia ndugu na majirani wa kijijini ambao kwa uchumi
wao wanahitaji msaada huo.
Ni
kweli kuwa saa nyingine moyo unakuwa mgumu kugawa vitu ambavyo vinafanya kazi
vizuri lakini kumbuka kuwa kama hivitumii tena ukiendelea kuvihifadhi
vitakusababishia mrundikano tu.
Hatua
ya tano ni tenga eneo kwa kila kitu.
Utagundua
kuwa ikiwa kila kitu kina eneo lake, ni rahisi sana kuweka vitu kwenye mpangilio. Kwa ajili kinapokuwa kimetoka pale
kilipotakiwa kuwa unachotakiwa ni kukichukua na kukirudisha hapo tu.
Haya
sasa baada ya kupata elimu hii ya kutumia dakika 15 kila siku kuweka mpangilio
ndani ya nyumba yako, je msomaji wangu uko tayari kufanya zoezi hili? Kama
kweli mwaka huu unataka nyumba yako ianze kuwa na mpangilio nakushauri utumie
elimu ya makala hii. Najua huenda unafikiri kuwa dakika 15 ni chache sana
kuweza kufanya chochote lakini nakuambia jaribu na utaona matunda yake.
Usisahau kurudi kunishukuru!
No comments:
Post a Comment