Huenda unataka kupendezesha kuta za nyumba yako kwa sanaa za
Kitanzania lakini inakupa changamoto kuwa sanaa hizo ni zipi. Labda umeshajenga
au kurekebisha nyumba vizuri ila hatua iliyobaki umalizie ni kupendezesha kuta
zake kwa sanaa.
Makala hii inakufungua fikra uone ni aina zipi unazoweza
kutumia. Kiukweli zipo mbalimbali na kwa wigo mpana. Nimeongea na dada Suma wa
Tanzania Cultural Heritage waliopo jengo la Quality Center na hapa amenyambua aina mbalimbali za michoro ya
ukutani ya Kitanzania kama ifuatavyo.
1.
Michoro ya tingatinga
Tingatinga ni aina ya michoro ambayo ilianzia maeneo ya
Oysterbay Dar es salaam kwenye karne ya 20 na baadaye ikasambaaa Afrika
Mashariki nzima. Jina Tingatinga limetokana na mwanzilishi wa michoro hii aliyekuwa
anaitwa Edward Saidi Tingatinga.
Michoro ya tingatinga haina uhalisia, kwa mfano mchoro wa
twiga utaonekana ni twiga lakini sio kama alivyo twiga halisi. Michoro hii ina
rangi kali za kuvutia na kwa kawaida ni midogo ambapo pia imekuwa rahisi kwa
watu mbalimbali hasa watalii kuinunua na kusafirisha makwao. Badala ya
kuwaachia wageni pekee kufurahia uzuri wa michoro ya tingatinga inawezekana
uzuri huu ukawa sehemu ya ndani ya mahali unapoishi.
2.
Michoro y kisu
Michoro hii ni ya kupendezesha nyumba ukutani kama ilivyo
kwa ile ya tingatinga. Tofauti yake ni kwamba michoro ya kisu inaonyesha picha
halisi, kwa mfano kama ni mchoro wa mtumbwi ni
kwamba unaonekana kabisa kama mtumbwi ulivyo.
3.
Michoro ya Zanzibar
Kama jina lake lilivyo ni kwamba michro hii inaakisi
muonekano wa mandhari ya Zanzibar kama vile ni milango, ufukwe na majengo mbalimbali ya Zanzibar.
4.
Michoro ya kanvasi
Michoro ya kanvasi ipo ya aina mbili ambapo aina ya kwanza
ni ile iliyoko kwenye kanvasi moja na ikakamilika. Aina ya pili ni ile iliyopo
kwenye kanvasi zaidi ya moja ili kuufanya mchoro mzima ukamilike. Kanvasi hizo
zinaweza kuwa tatu au nne na ukiondoa moja mchoro wote unapoteza maana.
5.
Michoro ya magamba ya ndizi, henna na ngozi
Kundi la mwisho la michoro ya ukutani yenye muonekano wa
Kitanzania ni ile iliyotengenezwa kwa magamba ya ndizi, ngozi au henna. Michoro
ya henna inatengenezwa zaidi Tanzania visiwani.
Kwahivyo kwa wewe msomaji wangu unayehitaji kupendezesha
kuta za nyumba kwa michoro yenye asili ya Tanzania, hayo ndio makundi ya
michoro unayopaswa kuzingatia.
Kama una bidhaa au huduma zihusianazo na nyumba nijulishe tufanye mahojiano 0755 200023
No comments:
Post a Comment