Jinsi ya kupamba
ukuta wa nje ya nyumba yako
Kupamba ukuta wa nje ya nyumba kunahitaji mpango
ulioandaliwa. Unatakiwa uangalie vitu kama hali ya hewa, sanaa za mapambo na
rangi ya ukuta. Muunganiko wowote wa rangi, mimea na sanaa za ukutani vinaweza kutumika kama
nyenzo za kutengeneza ladha yako binafsi kwenye ukuta wa nje wa nyumba. Kumbuka
kama nyumba ni ya kupanga hakikisha unapata baraka za mwenye nyumba!
Moja ya njia rahisi zaidi za kuhuisha au kubadili muonekano
wa kuta za nje ni kupaka rangi. Kabla
fundi rangi hajaanza kazi yake hakikisha marekebisho yote yanayohitajika kwenye
ukuta yamefanyika kwanza, kwa mfano kuziba nyufa na kadhalika. Kwa ujumla
maandalizi ya ukuta kabla ya kupaka rangi sio kitu rahisi sana kwa hivyo
hakikisha unapangilia vyema ili kupata matokeo unayohitaji. Kama kuta hizo
hazijawahi kupakwa rangi hakikisha unafikiria kwa makini juu ya nini unachotaka
kama umeamua kuzipaka rangi.
Paka rangi ambayo ni maalumu kwa kuta za nje na shirikisha
wataalamu wa mambo ya rangi, uchanganyaji
na upakaji wake. Hii ni muhimu kwani rangi za kuta za nje ya nyumba ni
tofauti na zile za kuta za ndani kwani hizi za kuta za nje zina uwezo wa
kupambana na hali ya hewa ya nje, wadudu kama fangasi na pia zinasafishika
kirahisi kwa maji. Mara kuta zako zinapokuwa zimepakwa rangi zingatia kuzitunza
kwa kuwa mradi wa kupaka rangi ni mkubwa kwahivyo sio kazi ungependa kufanya
kila baada ya miezi kadhaa.
Mifereji ya maji ya mvua ijulikanayo kama gata nayo
isisahaulike kupakwa rangi. Iwe gata ni za chuma au plastiki kuna rangi zake
mahsusi kwa nje na ndani hasa ukizingatia kuwa ndani inakuwa inaloa maji kila
mvua zinaponyesha. Maeneo ambayo yana chuma kwenye mifereji hii nayo
yanaandaliwa kitaalamu kuzuia kutu kama nilivyosema awali kuwa hakikisha
unafanya kazi ya kupaka rangi na wataalamu.
Kuta zilizopo karibia na majani, otesha vichaka vya maua na
miti katika uwiano utakaoleta rangi
nzuri ya muonekano wa maua ya asili. Kama ni muhimu unaweza pia kuotesha maua
kwenye vyungu vidogo vya maua vya kuninginiza ukutani.
Kuna nyenzo nyingi zilizopo za kuweza kuweka urembo ukuta wa
nje ambazo ni pamoja na mbao, tofali, marumaru au mawe kama yale ya Tanga. Tumia
nyenzo hizi kwa ukuta mzima au kwa maeneo ya chini tu. Kona ambazo hazina kitu
zinaweza kupendezeshwa kwa urembo wa mawe au chuma.
Mapambo mengi ya sanaa kwenye nyumba mara nyingi yanawekwa
sebuleni au zile sehemu ambazo burudani inafanyika. Lakini wakati kuta za ndani zinaweza kuwa za kupendeza kwa
sanaa za aina mbalimbali, watu wengi wanaweka juhudi kidogo kupamba kuta za nje ya nyumba wakati kiukweli ndizo wageni wanazoona
kwanza.
Kupamba kuta za nje kutafanya hata zile za ndani yavutie zaidi. Kupamba ukuta wa
varanda kwa mfano, kwa sanaa nzuri za kuta za nje itasaidia kusisitiza uzuri wa
mazingira ya eneo hilo. Kuna aina nyingi
za kuchagua ambazo zitaendana na jengo na pia ladha ya mwenye nyumba. Vinyago vya ukutani pia vinaweza kuongeza
staili kwenye ukuta wa nje uliokaa bila pambo. Na mapambo haya hayatakiwi kuwa
ghali, kwa mpango mzuri na umakini hata ile sanaa ya bei rahisi kabisa inaweza
kuleta mvuto wa ajabu. Kinachotakiwa tu ni kuchagua mandhari fulani na chagua
sanaa sahihi za kuendana na mandhari uliyochagua.
Fremu kubwa kwa mfano inasaidia kuleta mvuto maalumu kwenye
ukuta mtupu. Chagua fremu kubwa za picha za kanvasi zenye mandhari uliyochagua
kupamba ukuta wako wa nje ya nyumba. Sanaa
chache tu zilizowekwa kimkakati kwenye ukuta wa nje zitaleta tofauti kubwa.
Mapambo ya ukuta wa nje yanapendezesha nyumba yako kama vile
ya ukuta wa ndani. Njia mojawapo ya kupata sanaa za kupamba ukuta wa nje ya
nyumba ni kupiga picha makazi yako na kujitengenezea picha kubwa za fremu.
Fremu hizo pambia kwenye kuta za maeneo ya varanda, bwawa la kuogelea na hata
zile za bustani. Zingatia ubora wa sanaa
ambao utaweza kupambana na kupauka kutokana na jua na pia unyevu na kubanduka
rangi.
Makala kama hii, katalogi na mtandao vinakuwezesha kupata
mawazo ya mapambo ya ukuta wa nje. Mara nyingine mapambo haya kama picha za fremu
za kanvasi zinaweza kuwa ghali lakini hutajutia hela yako kama ni tamanio la
moyo wako kwani mapambo haya yatakufanya kujisikia raha na kuridhika na jinsi
ambayo mahali unapoishi panavyoonekana.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment