Wednesday, April 27, 2016

Namna ya kusafisha feni

Feni kama vilivyo vifaa vingine vya nyumbani, zinatakiwa kusafishwa mara kwa mara. Endapo utakaa muda mrefu bila kuisafisha, uchafu na vumbi linajilimbikiza kwenye mapanga yake na uchafu huo kusambaa ndani ya chumba pale unapoiwasha, ikiacha fenicha na
chumba kwa ujumla kikiwa kichafu na hivyo kufanya utunzaji uwe mgumu.

Habari njema ni kwamba kusafisha feni sio kazi ngumu, na kutokana na mazingira ya nyumba husika, inaweza kusafishwa mara moja ndani wa wiki mbili au mwezi. Ni haraka na rahisi ukiwa na vifaa sahihi.

Zifuatazo ni njia za kusafisha feni za miundo tofauti:

Njia ya kwanza inahusu feni za mezani na sakafuni. Unaweza kusafisha feni za muundo huu kirahisi kabisa kwa kutumia mashine ya upepo (vacuum cleaner). Usafishaji huu ni kwa feni za mezani zenye muundo mgumu kwa mmiliki kufungua bila kumuita fundi. Nyingi ya mashine za kusafisha kwa upepo zina vichwa vya aina tofauti tofauti ambapo unaweza kutumia kichwa chenye brashi ambazo zinasaidia kupenya na kukwaruza vumbi lililoganda na kufanya makoko hasa pale feni inapokuwa haijasafishwa muda mrefu au labda iko maeneo ya wazi na yenye vumbi jingi kiasi kwamba inadaka vumbi sana. Mashine hii inayakwaruza na hapohapo kuyanyonya.

Kwa feni nyingi za kusimamisha sakafuni ni rahisi mwenye nayo kufungua mwenyewe ule uzio wa kuzuia mapanga kwa ajili ya usalama bila kumuita fundi. Baada ya kufungua osha mapanga na uzio kwa kitambaa, maji na sabuni Wakati wa kufungua hakikisha umeizima kwanza.

Njia ya pili inahusu feni za darini na ukutani. Hizi unatakiwa utumie kitambaa kisafi cha kufutia yaani dasta,  kilichofungiwa kwenye fimbo ndefu. Futa mapanga ya feni kwa kwenda mbele na kurudi nyuma. Ili dusta ifanye kazi vizuri  inapaswa kuwa na unyevu kabla hujaanza kufutia ili kuipa uwezo wa kubeba vumbi zaidi na kuepusha kulisambaza.  Vitambaa vya pamba vinafanya kazi nzuri zaidi ya kuondoa vumbi pale vinapokuwa kwenye unyevu. Njia hii ni ukiwa umesimama sakafuni au juu ya meza. Endapo huwezi kufuta upande wa huu wa mapanga unachotakiwa kufanya ni kwenda kwenye njia ya tatu ambayo ni ya kufuta kwa mikono.

Wakati wa kusafisha feni ya darini au ukutani kwa mikono, unapaswa kuwa katika usawa mmoja karibu kabisa na feni hiyo. Tumia ngazi ndogo ya pembetatu ile ya ndani au kitu cha kusimamia ambacho kitakuweka sawa na feni unayotaka kusafisha. Moja ya faida ya kusafisha feni kwa kuishika na mikono yako  ni kwamba unaweza kushikilia mapanga yake na kuifanya itulia vizuri. Kama kitambaa kimechafuka sana na bado unaendelea kufuta badili uchukue kingine au suuza unachotumia na kurudia kufuta ili usiwe unasambaza uchafu kama tunavyojua kuwa mapanga ya feni nyingi yana rangi nyeupe. Futa taratibu kwani mapanga ya feni ni malaini sana usijesababisha uharibifu.
 Na mara unapomaliza kusafisha panga moja unalizungusha ukiwa umesimama palepale ili kusafisha linalofuata.

Ni vyema kuchukua tahadhari pale unapotumia ngazi kwa usafi wa ndani ya nyumba. Mwombe mtu aishikilie kama inawezekana na usipande hadi kileleni. Mtu huyo pia atakusaidia kukushikilia chombo cha maji ya kusafisha hasa pale unapohitaji kusuuza kitambaa na kukikamua ili kurudia tena zoezi la kufuta.
Pia zipo njia nyingine kama kutumia dawa za kupulizia kabla ya kuanza kufuta vumbi.

Unaweza kumaliza usafi wa feni yako kwa kuacha mapanga yakiwa na kinga ya polishi ya kuzuia vumbi ambapo inafanya vumbi lishindwa kujilimbikiza.

Feni nyingi za kisasa za darini zimeambatana na taa. Hakikisha kama feni unayotaka kusafisha ni ya aina hii taaiwe  imezimwa kabla ya kuanza kusafisha. Pia kuna wasafishaji ambao wanatumia ufagio za kuondoa buibui kusafishia feni zao. Hii sio nzuri kwani inafanya vumbi lisambae kote chumbani badala ya kuondolewa.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment