Huenda wewe na mwenza wako mnaishi maisha yenye kazi
nyingi (busy) ambayo mara nyingi yanapingana na kuwa na muda mzuri wa kukaa
pamoja. Hakika mnajua hisia zenu zinavyokuwa kwa ajili ya kukosa muda huo
muhimu. Ndio maana ni vyema kuwa na chumba cha kulala ambacho mkiwa pamoja kama
wanandoa itawezekana kufurahia ule muda mchache mnaokuwa pamoja. Kwa lengo la
makala hii chumba cha wakuu wa familia ni kile cha baba na mama wa familia – ni koloni lao hapo
nyumbani kama wengine wanavyoweza kusema. Wazazi mkiwa ndio nguzo ya familia
basi mnahitaji chumba cha kipekee. Mnaokaa kwenye chumba hiki ndio mnaolipa
bili na kufanya kazi kwa bidii ili mfanikiwe katika hilo. Kwa nini chumba chenu
kisiwe maalumu? Wakuu wa familia mnastahili chumba hiki!
Je wewe mkuu wa familia unakipenda chumba chako cha
kulala? Chumba hiki kiwe kama mahali patakatifu kwa wanandoa au yeyote
anayelala mule. Chumba kiheshimiwe kisiwe ni ofisi ya nyumbani. Chumba cha
kulala cha wakuu wa familia ni sehemu ya kupumzika hivyo vitu kama kompyuta
havina nafasi kwenye chumba hiki. Ni nini cha kwanza unachokiona mara baada ya
kufungua mlango wa chumba hiki, na ni nini unachokiona cha kwanza mara baada ya
kufungua macho asubuhi. Chumba hiki kiwe ni sehemu huru pasipo na usumbufu kama
wa kufua, ndoo za maji, kompyuta au midoli ya watoto. Chumba hiki sio stoo!
Midoli imekuwa ni
tatizo kwenye chumba cha kulala hasa kwa wazazi wanaokimbia mchakamchaka wa
maisha ya kila siku. Midoli inaishia chumba cha wazazi na hata kitandani. Kuwa wazi
na kuweka mipaka juu ya chumba hiki na hata midoli ya watoto isijazane
chumbani kwako na kitandani. Kwa ujumla watoto wawe na sehemu ya kucheza na
kuweka midoli yao. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni cha watu wazima
ndani ya familia.
Fenicha kuu kwenye chumba hiki ni kitanda. Kimsingi, kitanda kina lengo moja kuu:
kufagilia usingizi wenye afya. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia
kinahitaji kitanda chenye kukidhi vigezo vya usingizi bora. Kama matangazo
tuseme ya magodoro yanavyoonyesha ni kuwa tunatumia theluthi moja ya maisha
yetu kulala. Sasa kwa nini godoro, malazi na fremu ya kitanda visiwe maalumu.
Kuna njia nyingi ya kupata kitanda bora kwa bajeti yeyote. Kitanda chenye fremu
ya chuma tuu kilichosogezwa karibia na ukuta hakikidhi vigezo. Kila kitanda kinahitaji
bodi la kichwani (makala zijazo tutaongelea umuhimu wa bodi hili) ambayo
yanapatikana kwa saizi na mitindo mbalimbali.
Kwa kuwa msisitizo wa chumba hiki ni kwa
wanandoa, kama kuna sehemu kubwa weka
sofa au viti viwili vya kukalia badala ya kimoja. Mara zote fikiria vitu viwili
viwili. Kama wewe ni mwanaume au mwanamke uliye singo lakini ndio mkuu wa
familia weka picha ya peke yako kusisitiza utambulisho wako kuwa huna mtu. Kama
mnaolala humo mko kwenye mahusiano basi mambo ni kwa seti kama vile taa za vivuli
mbili, vimeza vya kando viwili na hata kama mishumaa basi miwili.
Kumbuka unatengeneza mandhari ya kupumzika na kuondoa msongo wa mawazo
wa siku nzima.
Chagua sanaa inayoelezea uhusiano wenu iwe ni picha
ya ngalawa, ndege au hata maneno ya kimahaba. Sio sawa kuweka picha za
marafiki, mababu na hata wanafamilia wengine kwenye chumba hiki. Tatizo ni kuwa
chumba kinaanza kuonekana kinguvu kimezidiwa na vitu. Watu wote hawa wana haja
gani chumbani kwako. Pambeni chumba cha kulala kwa picha zenu nyie wanandoa
mnaolala humo.
Chumba
hiki kamwe kisiwe na mrundikano, weka kero za maisha ya kila siku mbali na
mahali hapa patakatifu. Kama kabati lako la nguo limefurika, punguza ubakize
zile ambazo haswa unazivaa. Pia fikiria kupunguza kiasi cha fenicha ili kuwe na
nafasi chumba kisionekane kusongamana. Sakafu ionekane peupe isijazane vitu.
Zingatia kile
unachokiona kwanza mara baada ya kuingia chumba chako cha kulala.
Kanuni inasema kuwa mlango usiwe usawa mmoja na kitanda, kwa maana ya kuwa
ukiwa umelala kitandani uuone mkango lakini ukifungua mlango macho yasione
kitanda moja kwa moja. Mlango ukiwa namna hii unawapa walalaji kujiamini zaidi
kuwa wanamiliki chumba na usingizi unakuwa mwororo.
Vifaa vya umeme leo hii ni changamoto kwenye chumba
cha kulala. Kompyuta, luninga na vifaa vingine vya umeme vinatuzunguka na
kutunyonya nguvu kwa kuleta nguvu ya
uvutano mithili ya sumaku ambayo baadaye inaleta msongo wa mawazo. Ili
kupumzisha mwili na kuuweka katika afya njema basi ni vyema kuwa mbali na vifaa
vya umeme katika chumba cha kulala. Kama hamna jinsi kuwa ni lazima vifaa hivi
viwepo chumbani basi sio tu vizime na kuacha vijitaa vinawaka bali chomoa kabisa
kwenye umeme wakati wa kulala.
Kumbuka
kuwa kila kitu kwenye nyumba tunazoishi kinatupa ujumbe. Chumba chako cha
kulala wewe mkuu wa familia kinakupa ujumbe gani? Je kinakukumbusha majukumu
yote unayohitajika kukamilisha au kinakupa hisia za utulivu na kukukaribisha
kupumzika? Je kinakushawishi kuwasha luninga au kinakuleta kwenye faragha? Je
kinaongeza msongo wa mawazo kwenye maisha yako? Au kinakupa pumziko la nafsi
hata kama uko singo? Kama ndio basi umeweka mpangilio wa chumba cha kulala
ambacho ni kama mahali patakatifu.
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye
ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment