Jinsi ya kupanga vyombo kwenye makabati ya
jikoni
Je vyombo vyako
vinataka kuporomoka wakati ukifungua makabati ya jikoni? Kama ndivyo basi ni
wakati wa kupanga na kuhifadhi upya na makala hii ni sahihi kwako. Njia bora zaidi ya kupangilia vyombo na vifaa
kwenye makabati yako ya jikoni ni kufikiria ni kwa vipi unavitumia vyombo
vyenyewe. Ni vyombo na vifaa vipi unajikuta ukivitumia kila siku, na ni vipi
vinakaa tu kabatini. Tosa vile ambavyo unaweza kuendesha shughuli zako za hapo
jikoni bila kuwa navyo na elekeza nguvu kwenye kufanya makabati yako yaonekane
yanafanya kazi, masafi na yana mvuto. Mara utakapopanga ndani ya makabati yako
basi utajisikia furaha tena kuingia jikoni.
Ili kuweza
kufanikisha zoezi la kuhifadhi vyombo kwa unadhifu kwenye makabati yako ya jikoni
kwanza kabisa ondoa kila kitu kwenye makabati. Ni rahisi kuanza mradi wowote wa
kupanga upya kwa kuanza na eneo safi, na kwa makabati ya jikoni ni hivyo hivyo.
Songa mbele na toa kila kitu kwenye makabati kuanzia sahani, glasi, vikombe,
sufuria, vikaangio na kila kitu kingine chochote ulichohifadhi kwenye makabati
yako hayo. Panga kila kitu juu ya kaunta zako za jiko au hata kama una meza ya
jikoni ili kuweza kutathmini ni nini unacho na ni kipi unahitaji. Kuondoa vile usivyohitaji kutasaidia kuondoa mrundikano hivyo kukuwezesha
kuhifadhi vyema vile unavyohitaji. Na kama utajigungua kuwa kuna chombo ama
kifaa unakihitaji lakini huna basi hakikisha unakinunua kwanza kabla ya kuweka
mpangilio wako. Kama ukisubiri itakuwa ngumu kupata eneo la kukihifadhi
baadaye.
Fikiria kugawa vyombo vya zamani na vile usivyohitaji kwa wanaohitaji
zaidi, au hata kupeleka kwenye mnada wa vyombo vilivyotumika endapo viko katika
hali nzuri. Kufahamu kuwa vifaa vyako vya zamani vinaenda kwenye jiko lingine
itakupa amani zaidi ya kuvitupa tu bila mpangilio.
Futa makabati yako ambayo hayana chombo chochote kuanzia juu hadi chini.
Tumia sabuni nzuri za kusafishia pamoja na kitambaa cha kufutia na safisha kila
mahali hadi kwenye milango yote ile ya mbao na hata kama ya kioo ipo. “Kama utataka
kutumia kemikali za kusafishia,tumiavinega iliyochanganywa na maji kidogo,” anasema
Bi Mwajuma Issa ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kufanya usafi majumbani. Kemikali hii ya asili ya kusafishia
imefanikiwa sana kwenye makabati ya jikoni ila kama makabati yako yametengenezwa
kwa mbao ambayo haijapakwa rangi basi hakikisha unatumia sabuni za kusafishia
ambazo hazitaharibu mbao. Kwa namna hii unaweka makabati yako tayari kwa ajili
ya mpangilio mpya wa vyomba na vifaa vingine vya hapo jikoni. Kusafisha
makabati yako kwa mtindo huu kutaangamiza makazi ya wadudu na kufanya nyombo,
vifaa na vyakula utakavyohifadhi humo kuwa freshi.
Nunua vihifadhio vya kukusaidia katika mpangilio wa jikoni kama vile
vitrey vinavyotumika kuweka baadhi ya vyakula vikavu kama vitunguu na viungo ,
kitufe cha visu kwa ajili ya kuhifadhia visu vingi kwa wakati mmoja na pia
kurahisiha matumizi na vitu vingine vidogodogo kama vya kuwekea vijiko kadhaa
na uma ambazo zinatumika kila siku. Kwa kawaida vihifadhio hivi husimamishwa
kwenye kaunta za jiko. Pia makontena
kwa ajili ya kuhifadhia vyakula kama mchele, unga na sukari vitakusaidia kuweka
mpangilio jikoni
Baada ya kabati kukauka unyevu wote sasa ni wakati wa kutandika karatasi za
kwenye makabati ya vyombo kabla ya kupanga vyombo vyako. Sasa una makabati yako yakiwa
masafi na yameshatandikwa, ni wakati wa kufikiri ni kwa namna gani unataka
kuweka mpangilio wa vyombo unavyotaka kuhifadhi ndani. Tathmini hivyo vyombo na
vifaa unavyotaka kuhifadhi. Weka kila chombo kwenye kundi lake kutokana na aina
ya chombo. Wakati wa kupanga makabati ya jikoni inaleta mantiki kupanga vyombo
vinavyoendana pamoja.
Hifadhi
vyombo vya thamani na kuvunjika kwenye kabati za juu ya kaunta ambapo ni ngumu
kwa watoto kufungua na kuvunja.
·
Hifadhi pamoja vyombo
vya kuvunjika kama vile glasi za kunywea maji, glasi za juisi na glasi nyingine
zozote za matumizi ya kila siku.
·
Hifadhi pamoja glasi
za mvinyo na shampeni.
·
Hifadhi pamoja sahani
zako za kuvunjika na mabakuli. Ila hapa ieleweke vizuri kuwa sio sawa kuweka
sahani na mabakuli kwenye mstari mmoja kama njia ya kuhifadhi nafasi kwani
inaweza kusababisha kuvunjikiana.
·
Tofautisha sahani na
bakuli za matumizi ya kila siku na zile za matumizi ya msimu.
·
Kama makabati yako ya
jikoni yana milango ya kioo fikiria ni vyombo vipi ungependa vionekane kwa nje
kwani makabati haya ni kwa matumizi na umaridadi.
Hifadhi sufuria na vikaangio kwenye kabati za chini karibia na jiko. Kila
mmoja ana jiko la tofauti, lakini kwa mara nyingi makabati ya chini (chini ya
kaunta) ndio sahihi kwa sufuria na vikaangio. Vyombo hivi huwa ni vizito na
mara nyingi kuokoa nafasi sufuria moja inaingizwa ndani ya nyingine kuendana na
ukubwa kwa hivyo inaleta mantiki kuvihifadhi eneo ambalo haitakuwa na haja ya
kuvitoa tokea juu. Zile sufuria na vikaangio unavotumia mara kwa mara viweke
karibia na mlango ili kuchukua kirahisi na zile ambazo unatumia kwa nadra
zihifadhi mwishoni mwa makabati. Pia
unaweza kuona ni rahisi kuhifadhi sufuria na vikaangio vya kutumika mara kwa
mara kwenye raki yake inayoning’inizwa ukutani mbele ya makabati yako. Hii
inasaidia kuning’iniza kila moja peke yake badala ya kubebana.
Panga vijiko,
uma na visu vya ziada kwenye droo flati,ukiwa umegawanyisha kila kimoja kwenye
mahali pake. Vile vinavyotumika mara kwa mara hifadhi kwenye kihifadhio cha
vijiko na uma kilichowekwa juu ya kaunta na kitufe cha visu. Pia weka droo moja
la flati kwa ajili ya kuhifadhi vitambaa na vitaulo vya kufutia vyombo.
Tafuta eneo kwa
ajili ya kuhifadhia vifaa kama blenda na tosta ambapo vile ambavyo unatumia
kila siku waweza hifadhi juu ya kaunta. Kama blenda ni ya juisi ambayo
inatumika mara chache kwa juma basi hifadhi kwenye kabati
Hifadhi
sabuni na vifaa vya kusafishia ndani ya kabati lililo chini ya sinki.
Sasa
umemaliza kuhifadhi vyombo kwenye kabati zako za jikoni, zicheki mara kwa mara
kuhakikisha kuwa bado vyombo na vifaa vyako vipo kwenye mpangilio uliochagua.
Unaweza kuwa unaweka vidonge vya kuua wadudu kama mende mara moja kila baada ya
miezi sita.
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye
ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment