Thursday, July 7, 2016

Mitindo mitano ya kutandika kitanda kipendeze


Hata kama hupendi kutandika kitanda lakini hakuna ubishi kuwa unapenda muonekano wake kikiwa kimetandikwa, na kwa namna yoyote ile utapenda kitanda kiwe kimetandikwa pale mtu mwingine anapoingia chumbani.

Kitanda kilichotandikwa vizuri ni kile chenye muonekano wa kuvutia, kikiwa hakina makorokoro mengi na pia ni
rahisi kutandua wakati unapohitaji kulala.  Ifuatayo ni mitindo mitano niliyokuandalia ya kutandika kitanda. Nina imani baada ya kusoma makala hii utahamasika kuanza kutandika kitanda chako kwa kutumia mtindo mmjowapo kati ya hii.

Kunjia tandiko la juu kuanzia pale mito inapoishia
Tandiko la juu ya kitanda ni lile la mwisho wakati wa kutandika. Tandiko hili linaweza kuwa ni blanketi au duveti. Kutandika kwa kukunjia tandiko la juu pale mito inapoishia ni kwamba huenda  una mito mizuri ambayo ungependa ionekane.  Kama ndivyo, unachotakiwa kufanya ni kuipanga kuanzia kichwani kushuka chini hadi itakapoishia kwa idadi uliyo nayo. Eneo lote hilo la mito liache wazi na anza kukunjia tandiko lako la juu  pale mito hiyo inapoishia. Kumbuka kuwa usitandaze mito kwa jinsi ambayo itafunika ubao wa kichwani kwani ubao huu ndio fahari ya kitanda na pia unautumia kuegemea pale unapokaa kitandani ukiwa unasoma kitabu.

Kunjia tandiko la juu eneo la miguuni
Huenda unaona kama vile tandiko la juu linakaba au kuzuia mito isonekane vizuri au labda umetandika shuka nzuri ambazo nazo ungependa zionekane. Kama ndivyo basi, kunjia tandiko lako la juu eneo la chini kabisa karibu na miguuni na ndipo utaziwezesha shuka kuonekana pia. Muonekano huu ni rahisi na unavutia kwani kipande cha tandiko la juu ambacho huwa ni rangi tofauti na ile ya shuka ndicho kinachoonekana kwa sehemu ndogo tu mwishoni mwa kitanda huku kwingine kukiachia mito na shuka kupata wasaa wa kuonekana.

Utepe wa kitandani
Muonekano wa utandikaji kitanda kwa kushirikisha utepe wa kitandani unakaribia kufanana na wa kukunjia tandiko la juu miguuni ila tofauti yake ni kwamba kunakuwa na ongezeko la huo utepe. Huenda umesafiri maeneo mbalimbali na ukakutana na vitambaa ambavyo vina rangi na michoro ya kipekee na ukavipenda. Badala ya kuvinunua na kuvifungia kabatini, vitumie kwenye kuremba kitanda chako baada ya kukitandika. Kwa namna hii utakifurahia kila siku na kitadumu muda mrefu sana kwani hakitumiki/hakilaliwi zaidi ya kutandikwa mwishoni baada ya kumaliza kutandika kitanda na kuondolewa wakati wa kulala.

Tandiko la juu kufunika kote na kuchomekewa
Kwa ujumla huu ndio mtindo rahisi zaidi wa kutandika kitanda kwa kusambaza tandiko la juu kuzunguka kitanda kizima huku ukilichomekea kila upande. Unahakikisha limeonyooka kila mahali halafu unatupia mito juu unaondoka zako. Huu ni utandikaji mwepesi sana, huhitaji kukunja popote kwahivyo hupotezi muda wa kujua kama mkunjo umenyooka ama laa.

Tandiko la juu kufunika kote bila kuchomekewa
Huenda michoro ya duveti lako ni mizuri sana na ungependa yote ionekane kwa ukamilifu wake au labda fremu ya kitanda chako si nzuri kivile, pengine imeshakwaruzika sana unasubiria ukikaa vizuri uipake rangi upya. Ikiwa ndivyo basi  hutataka ionekane sana badala yake utapendelea ukishatandika uache duveti au blanketi likining’inia ili lisaidie kuificha. Huu pia ni utandikaji mzuri, unachotakiwa kufanya ni kusambaza tandiko la juu kwa uwiano huku ukihakikisha kuwa kipande kinachoning’inia kina urefu sawa kila upande,  halafu unatupia mito ya kulalia pamoja na  ya mapambo juu yake umemaliza.

Kwa maoni yangu ni kwamba kila mtindo wa utandikaji unapendwa zaidi na mtu fulani, chagua unaokufaa.


Karibu kwa ushauri simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment