Wengi
hatupendi kufanya usafi bafuni, ni kawaida. Awali ya yote napenda tukubaliane kwamba
katika makala haya bafu safi la kisasa linamaanisha chumba chenye eneo la
kuogea, kupigia mswaki na kujisaidia.
Ni
wachache wanaopenda kujipinda kusugua kuta zilizojenga utando wa sabuni au hata
kusafisha bakuli la choo. Uzuri ni kwamba kuna tabia unaweza kujizoesha na
zikakuwezesha
kulifanya bafu lako kuwa safi kwa muda mrefu na pia kupunguza kazi ya kusafisha
inapofikia ule wakati maalum wa kufanya hivyo. Tabia hizo ni kama ifuatavyo:
Piga mswaki
ukiwa umeinamisha shingo
Wapo
wanaofanya hivyo ila pia wapo wengi tu wanaopiga mswaki wakiwa wamenyoosha
shingo zao wakijiangalia kwenye kioo cha juu ya sinki. Unajua ubaya wake?
Unasambaza mapovu ya dawa ya meno kwenye kioo na kila mahali kuzunguka sinki.
Ukiinamisha kichwa kidogo na kuwa karibu na sinki, mengi ya mapovu haya
yanaishia kwenye sinki na kusafirishwa na maji. Hili sio la kupuuzia kwani
litakuokolea muda wa kusafisha kioo.
Suuza kuta za
eneo la kuogea kila baada ya kuoga
Unaweza
ukadhani kuwa inakuchukulia muda kakini si kweli. Kujenga tabia ya kusuuza
mapovu ya sabuni na maji machafu kwenye ukuta baada ya kuoga kutafanya bafu
lionekane safi kila wakati na zaidi ni kwamba wakati wa siku maalum ya
kusafisha kutapunguza kazi na muda wa kusugua. Fikiria utando wa sabuni na
uchafu wa mafuta toka mwilini ambavyo havitajiwekea tabaka kwenye kuta za bafu
kwa sababu tu umesafisha wakati uleule wa kuoga.
Acha bakuli la
choo safi kila ulitumiapo
Kusafisha
choo kila baada ya kukitumia kunaondoa uchafu na harufu mbaya bafuni. Kusafisha
haimaniishi tu kuflashi lakini pia kusugua endapo kuna uchafu umeng’ang’ania.
Mara zote hakikisha brashi na dawa za kusafishia bakuli la choo ziko umbali wa
mkono.
Futa mabaki ya
vipodozi
Wengi
wenye bafu za kisasa wana maeneo ya kuwekea vipodozi na kuweza kuvipaka wawapo
bafuni. Badala ya kuacha unga wa poda na vipodozi vingine vikiwa vimewagika
kila mahali unaweka ukaloanisha kipande cha karatasi ya chooni na ukafuta hapo
mahali.
Kuwa na sakafu
kavu
Ukiweza
kuweka sakafu ya bafu lako kuwa kavu kila wakati itakuepusha na mengi. Ukavu
sio wa maji tu bali hata mikojo ya watoto ama kimiminika kingine chochote
sakafuni. Njia nzuri pia ya kuwezesha hili ni kutumia mabafu za kupachika au
pazia za bafuni na pia kuwekeza kwenye vizulia vya bafuni ili nyayo zisisambaze
maji unapotoka kuoga.
Msomaji
wangu bila shaka utaona kuwa mantiki nzima ni kuacha safi kila eneo la bafu
pindi unapolitumia.
No comments:
Post a Comment