Wednesday, September 26, 2012

My Article for Newspaper: Nguo ya mama mzaa chema



Mchakato wa kupata gauni la mama wa bibi harusi.

Kama wewe ni mama, kati ya matukio yenye furaha zaidi ambayo utapenda Mungu akuonyeshe ukiwa hai ni siku ya harusi ya bintiyo. Mara binti anakuambia mama nataka kuolewa. Hongera! Kuna harusi mbele yako. Siku ambayo binti anaolewa na mwanaume wa ndoto zake inaleta machozi ya furaha kwa mama yeyote mzaa chema. Kwa furaha yote unayokuwa nayo na mipango yote unayoanza kupanga kumbuka tu kuwa ni harusi ya bintiyo na sio yako. Ana mipango na mawazo yake mwenyewe ambavyo angetaka harusi yake iwe.
Sio siri kuwa siku ya harusi ni siku kubwa kwa bintiyo. Lakini usisahau kuwa ni siku yako pia. Utakaa na marafiki zako na familia yako mpya. Utapigwa picha na hata utapata nafasi ya kucheza mziki na mtoto wako wa kiume mpya (bwana harusi). Na  cha muhimu katika yote unashuhudia binti yako akienda kwa mume kuanza maisha mapya.

Kabla hujasema ndio kwa gauni fulani hakikisha linashinda vigezo vyako mwenyewe. Nguo yako mama mzaa chema inatakiwa kuwa kama iliyoshonwa maalumu kwa ajili yako kwa maana ya urefu, ikukae vyema na zaidi ya yote ipitishwe na bibi harusi. Pia nguo hii ikufanye uonekane mrembo. Ni siku yako ya kung’ara pia. Makala hii inakupa mawazo ya kukusaidia mama mzaa chema kupata nguo ya kuvaa siku hiyo maalum maishani.

Kwanza, vaa nguo inayokukaa vizuri, isipwaye--bila hata kujali rangi hili ndio muhimu zaidi. Tengeneza muonekano mzuri kwa kuvaa nguo yenye kiuno au hata iliyounganishwa chini ya kifua na ikamwagika vyema. Huna haja ya kuvaa mburuzo kwa kuwa unaweza kuwa kero kwenye kucheza na kutembea.

Linapokuja swala la viatu vya siku hiyo chagua vya rangi kama ya silva na epuka ile sare sare gauni na viatu. Viatu vya kamba vinafaa zaidi wenye umri mdogo. Chagua kiatu chenye kisigino cha urefu wa wastani. Pia usisahau vitupio kama hereni, bangili na mkufu mnene wa kuvuta jicho. Hakikisha uvaaji haukusumbui wakati wa kusalimiana na kukumbatiana na marafiki wanaokupongeza.

Vaa kuendana na umri. Vazi lenye mikono ya urefu wowote linakubalika zaidi kulinganisha na ambalo halina mikono. Vinginevyo ukichagua kuvaa lisilo na mikono basi tupia na kimtandio au kikoti kidogo kwa juu.  Ungaro ungaro ukizidi unaweza usikupendeze kwa umri wako, kumbuka unakuwa mwanamitindo wa hilo vazi kwa ajli ya binti yako. Atataka kweli kukuona mama yake ukiwa umependeza. Kama binti anakubaliana na mama kuwa mabega wazi sawa, ila kama anaogopa vichwa kukugeukia kutokana na uvaaji usiozingatia umri na pengine kumfunika acha awe mchoyo. Ni siku yake sio yako. Inawezekana kabisa kupendeza bila kuacha sehemu kubwa ya mwili wazi.

Rangi zilizokolea zinaendana na umri mkubwa. Kiukweli bintiyo akiwa anaweka sahihi kwenye cheti cha ndoa mama unakuwa na hisia mbalimbali. Unaanza kuwaza tokea akiwa mchanga na kihuzuni kinapenya kwenye mifupa yako lakini mara rangi ya nguo yako inakupa tumaini/ mng’ao moyoni. Gauni lako lisifanane na la wasimamizi wa harusi. Ni vizuri kupata ushauri wa rangi toka kwa bibi harusi ili usijevaa rangi ambayo imekuwa tofauti sana na rangi za harusi. Pamoja na kuwa rangi ya gauni lako haifanani na ya wasimamizi ila ni vyema ziwe rangi za familia moja. Inashauriwa kuwa mama mzaa chema aepuke gauni la rangi nyeupe (ni bibi harusi tu anatakiwa kuvaa rangi hii). Vile vile, nyeusi inakataliwa; laa kama maharusi wamependa hivyo kwa kuwa inachukuliwa ni rangi ya maombolezo. Wasiliana na bibi harusi kama kuna rangi maalum za harusi.

Kwa kawaida mama wa bibi harusi ananunua gauni kwanza na ndipo anapomwendea mama wa bwana harusi mtarajiwa kiupole na  kumwambia juu ya chaguo lake la nguo. Maelezo utakayompa yatamsaidia kujua avae nguo ya namna gani. Hata hivyo mawasiliano haya yanatofautiana kutokana na familia. Unaweza pia ukaenda manunuzi na mama wa bwana harusi mkachagua pamoja kwa ladha yenu. Kujenga uhusiano huu wa mwazoni itasaidia sana familia zenu mbili huko mbeleni hasa watoto watakapopatikana.

Nyie wamama wawili mvae kila mmoja apendeze kwa ladha yake kwa kuwa sio mashindano. Wala mmoja asionekane kuwa kiongozi au bosi juu ya mwingine kwa suala la mavazi ya siku hiyo. Hata hivyo mama wa bwana harusi huenda akakushukuru wewe mama wa bibi harusi kwa kumpa dondoo za nguo utakayovaa. 

Kwa familia zenye talaka mama wa binti usijali kuhusu mama wa kambo wa bwana harusi. Bwana harusi mwenyewe ataongea na huyo mama yake mlezi kumtaarifu juu ya mavazi. Usimkwaze mama mzazi wa bwana harusi kwa kuonekana unaungana na mke wa mtalaka wake.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

No comments:

Post a Comment