lol..hii makala ni ndefu ila hutajututia muda wako kuisoma..tunajifunza kila leo.
KATIKA ulimwengu wa
mapenzi, baadhi ya wanaume hujikuta katika wakati mgumu, kutokana na kushindwa
kuwashawishi wanawake hata wakawapata kimapenzi, iwe katika mapenzi ya kawaida,
au hata uchumba ambao hatima yake ni ndoa.
Ukweli kuhusiana na suala hili ni kwamba
vijana wengi wa siku hizi hawafahamu jinsi ya kukabiliana na wanawake, ama kwa
kuwa hawapati mafunzo ya kutosha kutoka kwa wazazi wao, au pengine kutokana na
wanawake wa sasa kuwa wajanja, kiasi kwamba wanawatisha na kuwakatisha tamaa
mapema.
Ni dhahiri kuwa vijana wengi wa zama hizi huwachukulia wanawake kwa
mtazamo fulani ambao hauwasaidii kuwafahamu vema, hali ambayo matokeo yake ni
kukosekana kwa mafanikio na tija katika suala la mapenzi. Katika zama hizi
ambapo ungangari wa wanaume umepungua kutokana na kampeni za usawa wa jinsia,
vijana wa kiume ama huwaona wasichana kama vituo vya polisi, au wengine
huwaogopa kutokana na kujidhania kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kuwatosheleza,
hasa mwanamke anayehusika anapokuwa ni mrembo wa kusemwa na wengi. Unaweza kuwa
umezimika au umekufa na kuoza kwa mwanamke, lakini pia ulimi wako ukawa mzito,
hata ukashindwa kumweleza haja yako na kumfanya avunjikevunjike na kukupenda,
hata kama hakuwa na wazo la kukutana na wewe maishani mwako.
Jambo la muhimu la
kwanza ambalo kijana wa kiume hupaswa kulizingatia ni kwamba, unapoanza
kutafuta wasichana kwa minajili ya mapenzi, unapaswa kwanza kuwa mtu wa
kujiheshimu na kuonesha heshima kwao pia. Baadhi ya watu husema, mheshimu
msichana unayemfuatilia, kama ambavyo ungependa kuona mama yako au dada yako
akiheshimiwa na mume/bwana wake.
Lakini pia, unapotaka kujiongezea nafasi za
kupata mwanamke, hususan kama unataka mmoja tu kwa ajili ya mapenzi ya daima au
ndoa, jitahidi kuwa mtafutaji. Simba asiyewinda mwishowe ama hufa njaa, au
huishia kula wanyama dhaifu kama binadamu. Usipojihangaisha katika kipindi
muafaka cha kutafuta mwanamke unaweza kujikuta ukiwanajisi watoto wasioweza
kujitetea na ukaishia jela.
Unapokutana na msichana kwa mara ya kwanza na
kuzungumza naye kuhusiana na mapenzi, mwoneshe tabia ambayo atahisi kuwa
inakutofautisha na vijana wengine wote wa kiume aliopata kukutana nao kwa
mazungumzo, au anaofanya nao kazi ofisini, au anaosoma nao. MTENDEE UUNGWANA,
UKARIMU Ili kuhakikisha unaiteka roho ya msichana kwa jinsi hii, jitahidi kuwa
mtu wa mahaba, badala ya kuonekana kuwa na tamaa ya kumwingilia kimwili. Pia
mshike mkono wake kwa jinsi isiyoonesha tamaa bali upendo, mfungulie mlango wa
nyumba na gari, mwandalie kiti mfikapo mahali na mkataka kukaa na kwa ujumla
mfanyie ukarimu na uungwana.
MCHUKULIE WA THAMANI Pia katika vitendo vyako,
mfanye msichana adhani unamchukulia kuwa wa thamani na wa maana sana .
Unapompeleka nyumbani kwako, mathalani, mbusu mkononi au shavuni (akiwa tayari)
wakati wa kuagana naye, huku ukimwahidi kuwa utampigia simu. Msichana
atashangaa na kujiona wa thamani kubwa kwako, kwani umemtendea kama mtu muhimu
kwako. MTENDEE KAMA MALKIA Ikitokea ukatoka na msichana huyo mara nyingine, au
akakutembelea nyumbani kwako, endelea kumchukulia kama binti mfalme au binti
malkia.
Katika zama hizi za kupungua kwa upendo katika jamii, wanawake wana kiu
ya mahaba na mwanaume anayefahamu jinsi ya kutoa mahaba ni mtu adimu kwa watu
wa jinsia ya kike. USIHARAKIE NGONO Katika siku za kwanza, hakikisha kuwa huwi
na haraka ya kutaka ngono, kwani ukivuta subira, msichana mwenyewe atakuonesha
kwa ishara kuwa yuko tayari kwa ngono. Vuta subira, kwani kabla hujakata tamaa
na kujiona unachelewa kuonja asali, tayari msichana huyo ataanza kuanguka
penzini na wewe kwani wewe ni mwanaume unayemheshimu na kumtendea kwa ukarimu,
mahaba na heshima.
Hakika hata yule mwanamke anayedhaniwa kuwa malaya au
changudoa hupenda kutendewa hivi na mwanaume. Kwa hiyo kwa ujumla, kabla ya
kufikia mahali ukajidhania kufanikiwa katika medani ya utongozaji na ukampata
mwanamke wa kukufaa, unapaswa kufahamu ni nini hasa wanawake hutaka kutoka kwa
wanaume na jinsi ya kujipatia nafasi katika moyo wake na baadaye kuuteka.
SIFIA
UZURI WAKE Mwambie msichana huyo kuwa ni mzuri, na kwamba ni mtu wa kufaa kuwa
naye maishani – mtu anayefaa kuwa mama wa watoto wako. Wanawake hupenda sifa
kama hizo hasa kama watahisi kuwa mwanaume amezitoa kwa dhati na si kwa kutania
au kudhihaki, au kumvalisha kilemba cha ukoka. Hapa inambidi mwanaume kuwa
makini, asije akatia chumvi sana , akashtukiwa.
ACHANA NA WANAWAKE WENGINE
Jambo lingine la muhimu ni kuhakikisha kuwa unapokuwa unamfuatilia mwanamke
mmoja huwi na tamaa ya kuwafuatilia wengine wengi. Hakikisha kuwa msichana
unayemfukuzia anahisi kuwa umeweka akili yako yote kwake. Hata hivyo, hakikisha
kuwa hufikii mahali ukawa kama mjinga kwa ajili ya kutaka kumfurahisha, kwani
hakika hutamfurahisha kwa kufanya hivyo bali unaweza kumkosa.
Na kama baada ya
kumtendea ukarimu na kumheshimu bado ataonekana akiendelea kuambatana na
wanaume wengine au kuzungumzia wapenzi wake wa zamani, achana naye kwanza,
kwani huyo hajakuheshimu. Hakikisha kuwa mwanamke unayemheshimu yeye pia
anakuheshimu, la sivyo achana naye na muda si muda watakujia wanawake
wakionesha nia ya kukutaka. Usikubali kupoteza nguvu zako na muda wako kwa
msichana anayeonesha kila dalili kuwa hakupendi na anakuyeyusha.
MFANYE KUWA
RAFIKI Lakini kuna ushauri mkubwa zaidi anaoweza kupewa mwanaume, hasa kijana,
kuhusiana na wanawake. Ukiutekeleza ushauri huu basi karibu kila mwanamke
utakayekutana naye atakupenda na inaweza hata ikadhaniwa kuwa unatumia dawa.
Ushauri wenyewe ni kwamba jitahidi kumfanyia urafiki mwanamke unayetoka naye.
Mpe nafasi ya kujisikia huru na salama awapo na wewe na utabaini muda si mrefu
kuwa umekuwa mmoja wa wanaume wanaopendwa zaidi katika sayari hii kwani
wanawake wengi ( kama si wote) watakupenda. Hii itatokana na ukweli kuwa kila
msichana utakayetoka naye, hata katika hali isiyokuwa ya kimapenzi, atawaeleza
marafiki zake kuhusiana na tabia yako na kila mmoja atatamani kutoka na wewe
kwani unafahamu jinsi ya kumkuna mwanamke pale panapomwasha, kwa matendo yako.
Inaaminika kuwa kitu ambacho humfanya mwanamke ampende sana mumewe au bwana
wake, au mwanaume mwingine yeyote, ni ule ukweli kuwa mwanaume huyo amemwonesha
urafiki mkubwa. Rafiki ni mtu ambaye mnajuana, kupendana na kuaminiana na mara
nyingine huweza kuitwa maswahiba au wandani. Ni mwanamke mjinga tu asiyeweza
kumpenda mtu aliyemwonesha sifa hizi. USIJILAZIMISHE KUMPENDA Jambo la msingi
kabla ya kutekeleza yote yaliyobainishwa hapo juu ni kujihakikisha wewe
mwenyewe kwanza kuwa mwanamke mwenyewe unampenda kwa dhati na si kwamba
amekulazimisha mwenyewe kwa kukuganda.
Hakikisha kuwa hujilazimishi kuambatana
na mwanamke ambaye rohoni mwako huhisi kumpenda. Kama msichana atakujia na
kukwambia kuwa anakupenda lakini wewe ukawa huhisi mapenzi kwake, kuwa mkweli
na kumwambia kuwa hauko tayari kuambatana naye. Wanawake pia humpenda mwanaume
aliye muwazi na mkweli. HAKIKISHA ANAKUPENDA KWELI Sasa baada ya jitihada zote
za kumwingiza 'line' mwanamke ambaye una uhakika kuwa unampenda, unaweza
ukajikuta katika mtihani mwingine: hujui kama mwanamke unayemfukuzia amekupenda
kwa dhati au la. Hupaswi kuwa na wasiwasi kuhusiana na hili pia.
Hebu tuangalie
dalili kadhaa za mwanamke ambaye hakupendi. Kwanza, kama mwanamke hakupendi,
hata baada ya kumwonesha kila dalili kuwa unamjali na umemfanya swahiba wako,
utabaini kuwa kila unapotaka kumkaribia yeye anasogea, au anakukwepa. Mwanamke
huyu pia utamwona akionekana kama mtu aliyekerwa na jambo kila unapokutana
naye, ataepusha macho yake kukutana na yako, atakunja mikono yake kifuani mwake
kuepuka kukushika mkononi mnapokutana na atajitahidi kufunga miguu yake
unapozungumza naye. Pia mwanamke huyu ukiwa naye anaonekana kutojali na kama
ana simu atakuwa anatuma au kupokea ujumbe wakati wewe ukimweleza jambo.
Tena
wakati ukizungumza naye utabaini kuwa macho yake yameelekezwa kwa wanaume
wengine kama wapo – ishara kwamba katika wewe bado hajampata mwanamume anayemfaa.
Mwanamke huyu pia hatafanya jitihada za makusudi za kutaka kuzungumza na wewe,
utamsifia lakini hatajibu, wala hatajibu maswali yako na hatauliza maswali
yoyote kuhusiana na wewe au mambo yako. Kama msichana huyu haumwi, basi dalili
hizi zinatosha kukufahamisha kuwa hakutaki na ukiendelea kumfuatafuata unaweza
kujikuta unapoteza muda wako bure.
Mwanaume mwenye hekima hufahamu maana ya
dalili hizi na hasubiri mwanamke amtamkie kuwa 'sikutaki' au kumtukana na
kumdhalilisha hadharani. Kama Waswahili wasemavyo, mara nyingi akufukuzaye
hakwambii toka. Pamoja na kwamba zipo sababu nyingi binafsi za mwanamke
kutojisikia kumpenda mwanaume, yawezekana sana kuwa katika uchunguzi wake
amebaini kuwa wewe si mtu wa mahaba na kwamba huwezi kuwa mwandani wake wa
maisha, au pengine amekushtukia kuwa unamfuatilia mwanamke mwingine. Ili
kuepuka adha ya kunyanyaswa na mwanamke kwa kukataliwa, unapaswa kuzifahamu
sifa kadhaa anazopaswa kuwa nazo mwanaume ili kuishinda roho ya kigumu ya
mwanamke.
Kwanza, mwanaume mwenye uwezo wa kuiteka roho ya mwanamke ni yule
ambaye anapoingia katika mbio za kutafuta mpenzi au mchumba hufahamu
anachokifanya, huku akijua kuwa hakuna muda wa kupoteza.
Huyu huchukua hatua
kuhakikisha anavuta hisia za mwanamke. Pili, mwanaume mshindi katika fani hii
ni yule anayejifunza kutokana na mafanikio yake ya zamani na kusahau kushindwa
kwake kwa zamani. Mwanaume huyu huzingatia kuboresha upande wake, akiboresha
mwonekano wake na tabia zake, ili kumvutia mwanamke. Vilevile, mwanaume mshindi
katika medani ya mapenzi huwa mtu wa kujiamini. Hujisikia yuko huru na salama
mbele ya wanawake, jambo ambalo wanawake hulichukulia kama sifa mojawapo ya
mwanaume wa kufaa. Pia mwanaume mshindi huifahamu siri ya kufurahi na kila
apatapo muda mzuri huonesha furaha na tabasamu. Mwanaume huyu hufahamu jinsi
tabasamu, kicheko na bashasha vinavyoweza kumvutia mwanamke na kuuvunjavunja
moyo wake.
Mwanaume aliyeifahamu siri ya ushindi katika mapenzi pia si mtu wa
kusitasita, bali kila anapoona upenyo wa kumfikia mwanamke amtakaye huutumia,
bila kuanza kufikiria jinsi ya kuanza, wala matokeo. Mwanaume huyu hufahamu
kuwa wajibu wake ni kuomba na kwamba suala la kunyimwa au kupewa ni la
mwanamke. Kuna usemi wa kabila moja hapa nchini usemao 'mwombaji haaibiki, bali
huaibika anayemnyima'. Nadhani wanaume hawa huuzingatia usemi huu pia. Pia
mwanaume mwenye uwezo wa kuiteka roho ya mwanamke ni yule ambaye hujiwajibisha
kwa asilimia 100 katika jambo lolote linaloweza kutokea katika maisha ya
kimapenzi. Mwanaume huyu hujiona anahusika, bila kujali kuwa jambo lililotokea
ni zuri au baya. Mwanaume huyu hajengi msimamo wake kutokana na kushindwa kwake
kumpata mwanamke fulani, bali hujifunza kutokana na kila kosa. Pia huwa na
mawazo chanya, mathalani aendapo kwenye mtoko huzingatia tu kuwa anakwenda
kuburudika, bila kujali kuwa linaweza kutokea jambo baya huko.
Hizo ni baadhi
tu ya sifa za 'mabingwa' katika suala zima la mapenzi. Kama utazifanya kuwa
sehemu ya hulka yako, ni wazi kuwa utafanikiwa sana katika mbio zako za
kumtafuta mpenzi na hutakuwa na maswali mengi kuhusu iwapo mwanamke amekupenda
au la, kwani kila kitu kitakuwa dhahiri. Ushauri: 0654 043953
No comments:
Post a Comment