Huenda uko kwenye mchakato wa kupendezesha nyumba
mpya au unaboresha ya zamani, kioo ni pambo muhimu unalohitaji angalau kwenye
kila chumba. Ukisema kioo tu inaonekana kama ni kitu rahisi, madukani vipo
vingi vidogo, vikubwa na vya maumbo mbalimbali. Hata hivyo ikifika wakati
unapotaka kununua, kupata kilicho sahihi kwa chumba fulani pasipo changamoto,
zingatia mambo haya matatu.
1. Urefu wa ukuta – Kabla ya
kununua kioo, unatakiwa upime urefu
na upana wa ukuta unapotaka kukiweka. Hii inakusaidia kufahamu kabla ukubwa wa
kioo unachohitaji ungali bado hujafika kwa muuzaji. Kuta ndogo zinapendeza
zikiwekwa kioo kidogo (au kutowekwa kabisa kuendana na udogo wa ukuta) ili
pasionekane kuwa na mrundikano. Kioo kikubwa kwenye ukuta mrefu na mpana
kinatengeneza muonekano wa kuvutia.
Kwa nyongeza, fikiria
ni picha gani unayotaka kuutengenezea huo ukuta unaotaka kuweka kioo. Je ni
ukuta wa bafuni ambao kwa asili ni lazima uwe na kioo kwa ajili ya kutumika na
sio nia hasa ya kupendezesha, au unataka kioo unachotaka kuweka kiwe ni alama
ya pambo na kupendezesha ukuta husika? Kama ni kioo cha kutumika, je kinahitajika
kutumiwa kwa shughuli ipi? Ndio tunajua kuwa kazi namba moja ya kioo ni
kujitizama, ila je unajitizama uso tuu wakati wa kunawa kwenye sinki au ni kwa
ajili ya kujitazama utosini hadi unyayoni ili uweze kujiona muonekano mzima?
2. Eneo – Ni ukuta upi ambao unataka kuweka kioo?
Kama ni kwa ajili ya chumba cha wageni, kioo kinakua kama pambo kuliko
matumizi. Kwa maana hiyo weka chenye mvuto na hasa kikiwa cha umbo la duara au
yai kinapendeza zaidi.
Tofauti na chumba cha
kulala cha wageni, kioo bafuni ni kwa matumizi zaidi. Kwa eneo hili unapaswa
kuweka chenye umbo la pembenne na ukubwa wa kutosha kwa ajili ya mtu kujiona
vizuri wakati wa kufanya shughuli zake za kila asubuhi kujiandaa kuvaa, kuchana
na kubana nywele vizuri. Chanzo cha kutosha cha mwanga kwa kioo kilichowekwa
kwa ajili ya matumizi haya ni muhimu.
3. Staili ya chumba – Dondoo ya mwisho ya kuzingatia kwa
wote mnaotaka kuweka vioo vya kupendezesha ni staili ya chumba unachotaka
kukiweka (au ya nyumba nzima kama mandhari ni ya kufanana kila mahali). Je,
mapambo ya ndani ya nyumba yako ni ya aina gani, kwa mfano pengine fenicha nyingi
ni za chuma, itakua vyema ukiweka kioo chenye fremu ya chuma, vivyo hivyo kwa mbao.
Kioo kioane na muonekano wa finishing za fenicha zilizopo.
Nyumba iliyopambwa kwa
staili ya kiutamaduni ikiwa na sanaa ndogo nyingi, kioo nacho kinapendeza kikiwa
na fremu iliyotengenezwa kwa nuundo wa kiutamaduni.
Ukizingatia mambo haya
matatu, unakuwa na uhakika wa kuwa na kioo sahihi kwenye kila chumba kwenye
nyumba yako!
No comments:
Post a Comment