Uchaguzi na matumizi ya tandiko la mlangoni
Kwa nyumba nyingi wakati mgeni wako akifika mbele ya
nyumba yako, kitu cha kwanza anachokutana nacho ni mlango uliofungwa na tandiko
la mlangoni. Ingawa tandiko za mlangoni zina kazi ya kufutia miguu pia kuna njia
mbalimbali ya kuzifanya ziwe ni kama mapambo ya kwenye nyumba.
Uchafu na unyevu
unaobebwa kwenye nyayo toka nje ya nyumba unaweza kuharibu sakafu na pia
unachafua, na hii inamaanisha kutakuwa na hitaji la kufagia, kusafisha kwa mashine
ya upepo au kudeki mara nyingi zaidi ya ambavyo ingekupasa. Tandiko za mlangoni ambazo ni jamvi kama ni nje ya nyumba ama kizulia kwa
eneo la ndani ya nyumba; ingawaje watu wamekuwa wakizidharau ni njia yako ya
mwanzo kabisa ya kuzuia uchafu, mchanga na udongo visiingie ndani. Tandiko hizi
si za gharama kubwa na mara nyingine wala hazihitaji mvuto kwa hao wanaozitumia.
Weka tandiko za mlangoni kwenye sehemu zote za
kuingilia na hasa zile zinazotumika zaidi. Kuendana na hali yako ya kuishi
unaweza kuwa na milango ya pembeni na ya nyuma zaidi ya ule wa mbele. Hakikisha
kuwa yote ina tandiko za mlangoni. Pia kwenye sehemu ambazo hazijamaliziwa kwa
mfano kwenye banda la gari ambalo lina mlango mdogo wa kuingilia ndani
hakikisha napo unaweka jamvi mlangoni.
Tandiko za kukanyagia kwenye milango ya nje yaani
jamvi chagua ambazo zina matobomatobo au zenye nyuzi zilizo kama brashi. Jamvi
zinaweza zisionekane kuwa na mvuto lakini ni madhubuti kwa kufutia viatu na
zinadumu muda mrefu, zinafanya kazi nzuri sana kama tandiko za milango wa nje.
Zitumie nyumbani kwa eneo lenye matope na kwenye banda la gari au kwa mlango wa
nje wa pembeni na wa nyuma kama huzitaki kwenye mlango wa mbele.
Pia waweza kuweka kile chuma cha kutolea matope pale
ambapo kuna (au unategemea) kuwe na matope mengi na watie watu moyo kukitumia
pale wanapokuwa wamebeba tope kubwa kwenye viatu vyao.
Chagua tandiko hizi za mlangoni kwa kuzingatia
zinawekwa ndani au ni nje. Tandiko za mlango za ndani zinaonekana zaidi kama
vizulia na zinasaidia kufuta majasho ya miguu. Hakikisha mlango unaweza
kufunguka vizuri kizulia kikiwepo.
Kwa hivyo tandiko za mlangoni zinaweza kukaa kwa
ngazi tatu kutokana na mahitaji yake. Zile za nje kabisa zikiwa ni kama brashi
zikifuatiwa na za mseto ambazo ni mchanganyiko wa kubrashi na kunyonya majasho
na za mwisho zikiwa ni laini kama zulia ambapo zote hizi zinasaidia kudaka
uchafu kwa ngazi zote ili kuondoa kabisa uwezekano wa uchafu wa nje kuingia
ndani.
Kama jamvi zitakuwa maeneo ambayo zitaloa mvua
chagua staili ambayo itakauka haraka. Chagua zulia za mlangoni za ndani ambazo
hazitaharibu sakafu ya chini yake na ambazo zitaendana na mapambo ya ndani
yaliyopo. Je kizulia husika ni kwa ajili ya mapambo tu? Chagua rangi ambazo
hazitaonyesha uchafu kwa mfano nyeusi na damu ya mzee na pia rangi zisizochuja.
Safisha jamvi na vizulia vya mlangoni mara kwa mara.
Inawezekana vikajaa uchafu kiasi kwamba havisafishi viatu tena bali ndio
vinavyochafua. Kung’uta, safisha kwa mashine ya upepo au fagia takataka zilizo
juu juu. Kama tandiko ni kavu hatua hii itasaidia kuondoka uchafu mwingi kabla
ya kusafisha kwa kulowesha kwa kuzipiga maji yenye shinikizo.
Vua viatu vyako wakati unaingia ndani mwako, hasa
kama umetokea sehemu yenye matope au udongo mwingi. Jenga njia ya kuingilia kwa
sakafu ngumu ili kufanya mazingira masafi kabla hujaingia ndani.
Kwa kuwa tandiko za mlangoni zipo za aina nyingi
kutokana na matumizi baadhi ya watu wanapata taabu wakati wa kuchagua tandiko
sahihi kwa mahitaji na ladha yao. Kwa sababu hiyo basi jiulize maswali mawili
pale unapohitaji kununua tandiko jipya la mlangoni, ambayo ni “ unaenda
kulifanyia nini hilo tandiko na unaenda kuliweka wapi?” Majibu ya maswali haya
mawili rahisi yatakuongoza wewe mnunuzi na muuzaji kupata tandiko litakalokufaa
kuendana na hitaji lako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment