Monday, October 31, 2016

Namna ya kupendezesha sebule kwa rangi ya bluu

Kwa lengo la kutengeneza sebule yenye hisia ya utulivu, muonekano wa usafi na kiwango njia mojawapo ni kwa kutumia rangi za familia ya bluu. Mara zote bluu imekuwa ni rangi freshi na inafanya ndani kuwe na uhai. Usishangae ni kwanini sebule za bluu zinaonekana nadhifu na maridadi ziadi.

Rangi mbalimbali zilizo kwenye familia ya bluu zinafanya ndani kupendeze na bila shaka kuvutie. Unaweza kutumia bluu ukutani, kwenye zulia, pazia au
vifaa vingine kama vile taa za vivuli, mito ya mapambo, mapambo ya kwenye shelfu, mezani na ya kwenye kabati la maonyesho na hata bluu kwenye fenicha. Vitu hivi vinavyoweza kuwa na rangi moja ya bluu au miguso ya bluu katika muundo wa maua au michoro yake vinaifanya sebule kuwa na muonekano wa kisasa.                                                                                                                              Mandhari inakuwa ya kuvutia kiasi kwamba unatamani kutumia siku nzima ukiwa umekaa sebuleni.

Bluu ni rangi tulivu ya asili, japo sio siri kuwa wengi wanashindwa kupendezesha sebule kwa kutumia rangi hii. Sababu zinaweza kuwa mbalimbali kama vile kutokufahamu ni kwa namna gani wanaweza kuishirikisha na rangi nyingine na rangi hizo ni zipi. Inachukua nguvu ndogo tu ya kuchagua na kuoanisha rangi nyingine tulivu zinazoendana na bluu kama vile kijivu, zambarau, nyeusi, krimu na nyeupe. Au kama unataka kuonyesha msisitizo wa ndani mwako, oanisha bluu na rangi za metaliki au damu ya mzee.

Pazia zenye michoro au maua ya bluu ni ongezeko lenye kuvutia sebuleni.  Pazia za maua ya bluu sebuleni zinapendeza pale ambapo kuta zina rangi ya krimu au nyeupe kwani inatengeneza muonekano wa utulivu. Bluu hiyo inapotumika madirishani na kwenye vitupio kama vile mito ya makochi, zulia na mapambo mengine inafanya ujirani mzuri wa rangi kati ya maeneo hayo mawili.

Pia kama sofa ni la rangi za jamii ya bluu, pendezesha sebule kwa zulia la rangi ya kijivu.  Au njia nyingine ni ya kuwa na pazia za krimu unazozioanisha na kiti au sofa zilizotenenezwa kwa kitambaa cha maua au michoro yenye rangi ya bluu iliyokolea, yaani bluu nzito kwenye rangi za familia ya bluu.
Bluu na krimu laini ni njia ya ajabu ya kutuliza chumba hasa sebule. Muunganiko huu unaendana na fenicha za rangi nyepesi kama vile zilizopaushwa na jua. Kwenye fenicha hizo weka mapambo madogodogo na vitupio vyenye bluu ya kukolea na ile ya kuwaka.

Kwa ukutani unaweza kutumia bluu pia ila uzingatie kuwa bluu nzito inafaa pale ambapo sebule ni kubwa na inapokea mwanga mwingi wa jua, kinyume cha hapo bluu hii itasababisha giza. Ikiwa unataka kuongeza mwanga sebuleni tumia bluu nyepesi pamoja na njano.


Kuna njia nyingi mno za kuweza kupendezesha sebule kwa bluu. Kikomo ni ubunifu wako!

No comments:

Post a Comment