Ongeza uasili ndani ya nyumba kwa kupamba na mimea
Kama unataka kupamba nyumba yako kwa njia ya asili
na kuleta hewa safi ndani hakuna chaguo zuri zaidi ya mimea ya ndani ya nyumba.
Mimea ya ndani ni zana ya mapambo ambayo huongeza uzuri wa rangi ya kijani kwa
kiasi cha kutosha na kuboresha hali ya hewa ndani ya chumba. Unaweza ukaiweka
kwenye kona tupu, kwenye madirisha, shelfu au kama pambo la kati. Kitu
kizuri juu ya mimea ya ndani ni kuwa inaweza kukua vizuri eneo lolote, liwe
dogo au kubwa pamoja na hali ya hewa ya ndani na mwanga utakaoweza kupatikana. Kuna
aina mbalimbali za mimea ya ndani kwa wauzaji wa maua ya asili ambayo inakidhi
kila hitaji.
Hata hivyo ni wachache wanaoweza kukabiliana na
changamoto na utunzaji wa mimea ya ndani. Kazi kama kuyamwagilia kila
siku, kuweka mbolea, kuondoa majani
makavu na kupruni ni mambo kadhaa yanayoweza kumkatisha mwenye nyumba tamaa.
Bado kiukweli mimea ya ndani sio ngumu kivile kuitunza.
Unatakiwa kuchagua chumba ambacho umeamua kupamba kwa
mimea ya ndani. Mimea hii inaonekana maridadi kwenye sehemu yoyote ya nyumba.
Unaweza ukaipambia jikoni, bafuni, sehemu ya kuingilia au sebuleni. Unatakiwa
kuchagua sehemu nzuri ya kuweka huo mmea katika chumba husika. Epuka kuweka
mmea karibia na moto au karibia na bomba la kuchemshia maji. Hakikisha kuwa
sehemu uliyochagua inapokea mwanga wa jua wa kutosha kwa ajili ya afya ya
mchakato wa usanisinuru (hii ni njia ya mimea ya kujitengenezea chakula kwa
kutumiamwanga wa jua).
Unatakiwa kuchagua aina ya mimea ya ndani unayotaka kuweka. Mimea na maua yanayofaa kuwekwa ndani ya
nyumba ipo ya aina nyingi kwenye bustani za wauza maua. Mimea maarufu ya ndani
ni ya jamii ya aloe vera, bambuu, kaktasi na magimbi. Wakati wakununua uliza
mahitaji ya mmea husika kwa mfano kiasi cha jua, joto na maji kinachohitajika
ili mmea ustawi vizuri. Nunua tu ile ambayo unaona utaweza kuitunza. Kumbuka
walau mara moja kwa wiki zungusha chungu cha mmea kuwezesha mmea kukua kwa
uwiano.
Mimea ya ndani inatakiwa kuwekwa kwenye vyungu vya
mapambo kuendana na mapambo mengine yaliyopo hapo mahali. Vinaweza kuwa vyungu
vya kauri vilivyochorwa kwa mikono au vyungu vya kisasa vya rangi ya silva
inayong’aa pia vyungu vya kioo vinaonekana maridadi sana kwa maeneo ya sebuleni
na chumba cha kulia chakula.
Kwa ujumla utunzaji wa mimea ya ndani unahitaji muda na nguvu kidogo ingawa kuna
matatizo yanayoweza kutokea na kuleta usumbufu mkubwa. Mojawapo na kubwa la
matatizo haya ni ukungu ambao unaweza kujijenga kwenye udongo au majani
ya mimea yako ya ndani. Ukungu ni jambo linaloweza kuleta uharibifu kwako na
kwa mimea yako. Ikiwa basi tatizo la ukungu limejitokeza chukua kitambaa kilicholoa
ushike jani kwa chini (ili kuliongezea nguvu
lisivunjike) na lifute, hii itaondoa ukungu wote unaoonekana. Usije ukajaribu
kufuta na kitambaa kikavu kwani utaharibu sehemu ya juu ya jani. Wakati majani yote yakiwa
yameshafutwa, ruhusu mmea kukauka kwa kuuweka eneo ambalo linaingiza hewa.
Kama ukungu umeota kwenye udongo wa chungu basi
ondoa eneo la juu na uweke udongo mwingine. Hata hivyo kama udongo utakuwa
umevamiwa kwa kiasi kikubwa basi inashauriwa kuondoa udongo wote na kujaza
chungu upya. Ongezea na dawa ya kuzuia fangasi kwenye udongo wa mimea yako ya
ndani.
Hakikisha maji kwenye chungu yanatembea. Njia kuu ya
ukungu kujijenga ni udongo kuwa na maji maji kwa kipindi kirefu. Kila chungu
cha mimea ya ndani kiwe na ukanda wa kokoto ndogo chini ili kuruhusu
mchanganyiko ulioko ndani ya chungu kukauka vyema. Hii inafanya mimea yako iwe
na afya na kupunguza uwezekano wa ukungu kujijenga. Pia weka mmea wako wa ndani
eneo ambalo linaingiza hewa kwa vile ukungu unashamiri eneo ambalo hewa ni
hafifu.
Safisha mimea yako ya ndani mara kwa mara. Vumbi
linajijenga kwenye majani ya mimea ya ndani kama linavojijenga kwenye maeneo mengine ndani ya nyumba. Hili vumbi
linafanya uchafu mwingine ujijenge juu ya majani na mmea kushindwa kufanya
vyema usanisinuru hivyo kudhoofu. Kufuta majani mara kwa mara na kitambaa
kilicholoa inasaidia kuondoa vumbi kujijenga kwa hivyo kuondoa uwezekano wa
ukungu. Ondoa majani yaliyokufa mapema iwezekanavyo.
Mimea ya ndani inaweza kuwa na faida kubwa katika
nyumba zetu na maisha yetu. Inaweza kuchuja hewa ndani ya nyumba na kufanya
mazingira yenye afya. Hata hivyo ni vyema kuwa makini kwakuwa kuna mimea ambayo
ni sumu kwa wanyama wa ndani kama vile paka na kadhalika na pia kwa watoto
wadogo. Fanya utafiti wako vizuri na uone ni wapi pa kupamba na asili ndani ya
nyumba yako. Chunguza mimea mbalimbali ambayo unaweza kupamba maeneo hayo na
uone kama utunzaji wake utaendana na maisha unayoishi. Kama ukikwama pata
ushauri kwa wataalamu wa mambo ya bustani na mimea. Wataalamu hawa watakusaidia
kupata na kukuhakikishia mimea ya ndani
itakayokufaa.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023