Thursday, May 23, 2013

My article for newspaper: meza ya kahawa


Jinsi ya kupamba meza ya kahawa


Meza ya kahawa inaweka sebule pamoja na ikiwa imepambwa vyema inahuisha muonekano mzima wa chumba. Meza ya kahawa ni meza  isiyo refu ambayo imebuniwa kuwekwa mbele ya sofa, kuegemesha vinywaji ( na ndipo jina lilipotokea) majarida, vitabu na vitu vingine vidogodogo vya kutumia wakati mtu amekaa sebuleni kama vile kosta za kuwekea vinywaji na hata wakati mwingine hutumika kuwekea miguu. Meza ya kahawa ni kitovu cha sebule nyingi na zipo za maumbo mbalimbali kama vile duara, yai au pembe nne na nyingi ni za mbao na chache za kioo pia zipo chache sana  za chuma. Meza hizi pia zinaweza kuwa na sehemu ya kuhifadhia kwa chini.  Cha msingi ni kutumia hii sehemu tambarare ya meza kuonyesha mapambo ya chumba chako bila kutupia kila kiwezekanacho juu yake.
Kwa kuwa meza ya kahawa ina matumizi mengi, mara nyingi ni ngumu kujua ni kwa vipi uipambe. Je umeshajiuliza, ufanye nini na hii sehemu  tupu ya meza ya kahawa? Wakati mwingine ni vyema kuipamba isivyo rasmi sana ili kuleta hisia za burudani na starehe ili hata kuweza kunyanyua mguu wako na kuutuliza hapo na kusoma gazeti wakati ukifurahia kinywaji chako. Au labda ni wakati wa kula chakula hivyo kutakiwa kukaa meza ya chakula lakini kuna kipindi cha luninga ukipendacho kwa wakati huohuo, basi unageuza meza ya kahawa kuwa ya chakula. Ukifikiria kwa uhalisia, kwa muonekano usio rasmi mapambo ya meza ya kahawa yanawezesha wanafamilia kuitumia kwenye kukutana kupumzika, kucheza michezo, kusoma vitabu na kuangalia luninga wakati huohuo wakiburudika na vinywaji. Meza hii inakusanya pamoja faraja na furaha ya familia. Bila hii meza ya inchi 60 kwa 30, ni wapi ungeweka vivywaji vyako, karatasi, vitabu, majarida na kadhalika…je ni sakafuni?

Hata hivyo kwa sebule zilizo rasmi meza ya kahawa iliyo juu ya zulia jeupe na yenye mapambo ya thamani yanayong’aa ni ya kushangaa tu kwa jicho, haiguswi hadi pale tu anapotembelea mgeni wa heshima! Lakini ijulikane kuwa kwa sebule zisizo rasmi meza ya kahawa iliyowekwa kwa jinsi ambayo kati ya sofa na meza kuna nafasi ya kutosha kwa miguu kuwa huru shughuli zinapoisha meza husafishwa, hupangwa vizuri na kuachwa maridadi ikisubiri shughuli nyingine kwa mgeni mwingine au kwa makutano mengine ya familia.

Wakati wa kupamba meza yako ya kahawa zingatia nafasi iliyopo, jinsi watu wanavyopita kukalia sofa. Hutapenda kuvunja mapambo yako ya thamani kutokana na msongamano. Hakikisha kuna uwiano kati ya pambo na meza, kwa mfano usiweke vesi kubwa ya maua  yenye matawi kama zile za kuweka sakafuni kwenye kona ya chumba kwenye meza ya kahawa. Kwa ajili sebuleni ni sehemu ambayo mazungumzo yanaendelea hutapenda kuona mgeni wako aliyekaa sofa ya upande mmoja akivunjika shingo kujaribu kumuangalia mgeni aliyekaa sofa ya upande wa pili kutokana na kuzuiwa na ukubwa wa maua yaliyoko mezani.

Jua eneo sahihi la kuweka meza yako ya kahawa na mpangilio wa mapambo yake kutokana na matumizi ya meza yenyewe. Kama nilivyoandika kwenye makala iliyopita ya muonekano wa sebule ya kuwa kuna sebule ambazo zinatumiwa na wanafamilia na wageni kwa pamoja (sebule zisizo rasmi) na kuna zile ambazo ni chumba rasmi kinachotumika kukiwa na mgeni tu; hivyo basi kama meza ya kahawa ipo kwenye sebule isiyo rasmi wakati wa kuipamba zingatia kuwa itakuwa inavurugwa na kuwagikiwa vinywaji mara kwa mara. Ni wengi wenu mmesikia waume zenu na watoto wakilalamika  “hivi hiki kimeza kinatakiwa kuwa hapa kweli?” Usiweke mapambo ya kuvunjika kirahisi hapa, yahifadhi kwa eneo lingine.   Tumia mapambo ambayo hayawezi kuharibiwa kirahisi kwa mfano kwenye meza ya sebule isiyo rasmi usiweke vesi za maua zenye maji pamoja na vitabu pamoja.
Kwenye kupamba meza ya kahawa ni muhimu kuzingatia mapambo mengine yaliyoko hapo sebuleni. Iwapo utaamua kupamba meza yako ya kahawa kwa vimapambo vidogo vidogo vingi basi ni vyema ukaviweka kwenye sinia la mapambo au kuvitandaza kwenye kitambaa cha kati cha meza ya kahawa ili meza isionekane kama bahari ya vikorokoro. Kwa mfano kama ukiweka kwenye sinia la mapambo basi wakati kuna shughuli wahusika wanaweza kusogeza sinia pembeni na meza kutumika kwa shughuli.

Wakati wa kutafuta mapambo ya meza yako ya kahawa, hakikisha unatafuta pambo la kati ambalo ni alama yako ama kitu unachopendelea, au labda ulilinunua ulipotembelea mahali fulani kwa hivyo litakuwa linakupa ukumbusho fulani. Utahitaji pambo kubwa la kumiliki meza ambalo la
linaweza kuwa vesi ya maua, mshumaa au kinyago au kitu chochote tu ambacho kitavuta jicho.
Furahia kupamba meza yako ya kahawa kwani ni njia mojawapo nzuri ya kubadili muonekano wa sebule bila ya kutumia gharama kubwa au wataalamu. Iwe ni kwa kuweka pambo moja kubwa au mengi madogodogo mkakati wako ni kupata mlingano na uwiano ndani ya chumba.

Mwisho ila muhimu zaidi, kabla hujapamba meza yako ya kahawa, ni muhimu kuchagua staili ya meza ambayo itaendana na mahitaji na maisha unayoishi. Fikiria kuhusu kazi zake na itatumikaje. Je ni ya kwenye sebule iliyo rasmi au ni sebule ya familia nzima pamoja  ambapo watoto wanakaa na kufanya kazi zao za shule au mume wako atawekea miguu wakati akitazama ITV?  Kufahamu matumizi na mahitaji ya meza yako ya kahawa itakupa mwelekeo sahihi wa ni mapambo gani ya kununua na jinsi ya kuyapambia!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment