Monday, June 13, 2016

Dondoo 4 za uoteshaji maua ndani ya nyumba



Kuna kitu cha kipekee kuhusu bustani, maua  - mchakato wa kuotesha vitu hai kwa ajili ya kufurahisha nafsi na vilevile kuongeza mvuto wa ndani ya nyumba kwa ujumla wake.  Kama wewe ni mmojawapo ambaye bustani inakuhuisha nafsi kiasi kwamba ungetamani kuwa nayo hata ndani kama ilivyo nje basi makala hii ni kwa ajili yako. Ili
kufanikisha hilo zingatia dondoo zifuatazo:

·        Kuwa makini na unapotaka kuweka ua au mmea wako
Linapokuja swala la mvuto, maua au mmea fulani unapendeza zaidi ukiwa eneo fulani la ndani ya nyumba.  Kwahivyo fikiria eneo unalolipenda na litakalokidhi mahitaji yako huku ukikumbuka kuwa mimea inapaswa kuwa jirani na mwanga wa jua. Kama unachukua muda mwingi kukaa sebuleni inawezekana ndipo unapenda kuongeza uhai kwa kupaongezea uzuri asili wa nje.

·        Jua mahitaji ya mmea wa ndani
Unapokuwa unafahamu vizuri mahitaji ya ua au mmea unaotaka kuotesha ndani itakusaidia kuuweka mahali sahihi na vilevile kuchagua ile inayokidhi vigezo hivyo. Unaweza ukadhani kuwa chumba kina giza sana haifai kuweka mmea lakini kumbe ukweli ni kuwa kuna mimea na maua ambayo yanahitaji mwanga hafifu sana. Bila shaka umeshaona maua ambayo yanahitaji kivuli kikubwa na yale ambayo ukiyaweka kivulini tu yanakufa. Mgawanyo mzuri wa maua haya upo kwenye wale wauzaji wa bustani walizootesha kando ya barabara. Utagundua kuwa yapo maua ambayo wameyaotesha juani kabisa na yapo ambayo wameyaweka kule chini ya miti ambako hamna jua kabisa na mwanga ni kidogo sana. Kwahivyo kwa namna hii hii unapaswa kufahamu juu ya hayo maua unayotaka kuotesha ndani.

·        Mwagilia kutokea chini
Huenda kwenye umwagiliaji wako wote wa siku zote kwenye bustani za nje umezoea kumwagilia juu kwenye majani. Kwa maua ya ndani unapaswa kumwagilia pale kwenye udongo ndani ya chungu. Zipo pia kontena za kuoteshea maua haya ambazo zina visahani. Unaweza kumwagilia kwenye kisahani na mizizi ya mmea huo ikajiloweka yenyewe humo kufyonza hayo maji. Vilevile kuwa na ratiba na kipimo maalum cha kumwagilia. Mimea mingi ya ndani inatosha kumwagiliwa maji glasi moja na mara 2 kwa juma ndani ya chungu kimoja.

·        Epuka sehemu yenye joto sana au baridi sana
Mimea ni vitu hai ambavyo ninadhurika na mabadiliko ya halijoto. Kama halijoto itabadilika kuwa joto sana kwa mfano karibia na jiko au baridi sana labda kuna kiyoyozi kikali muda wote ua likioteshwa kwenye mazingira kama hayo litakufa. Epuka kuweka vyungu vyako vya maua karibia na maeneo hayo mawili.

Makala haya yameandaliwa na Vivi Obed.  0755 200023

No comments:

Post a Comment