Wednesday, May 29, 2013

My article for newspaper: pamba kwa mimea ya ndani



Ongeza uasili ndani ya nyumba kwa kupamba na mimea

Kama unataka kupamba nyumba yako kwa njia ya asili na kuleta hewa safi ndani hakuna chaguo zuri zaidi ya mimea ya ndani ya nyumba. Mimea ya ndani ni zana ya mapambo ambayo huongeza uzuri wa rangi ya kijani kwa kiasi cha kutosha na kuboresha hali ya hewa ndani ya chumba. Unaweza ukaiweka kwenye kona tupu, kwenye madirisha, shelfu au kama pambo la kati. Kitu kizuri juu ya mimea ya ndani ni kuwa inaweza kukua vizuri eneo lolote, liwe dogo au kubwa pamoja na hali ya hewa ya ndani na mwanga utakaoweza kupatikana. Kuna aina mbalimbali za mimea ya ndani kwa wauzaji wa maua ya asili ambayo inakidhi kila hitaji.

Hata hivyo ni wachache wanaoweza kukabiliana na changamoto na utunzaji wa mimea ya ndani. Kazi kama kuyamwagilia kila siku,  kuweka mbolea, kuondoa majani makavu na kupruni ni mambo kadhaa yanayoweza kumkatisha mwenye nyumba tamaa. Bado kiukweli mimea ya ndani sio ngumu kivile kuitunza.

Unatakiwa kuchagua chumba ambacho umeamua kupamba kwa mimea ya ndani. Mimea hii inaonekana maridadi kwenye sehemu yoyote ya nyumba. Unaweza ukaipambia jikoni, bafuni, sehemu ya kuingilia au sebuleni. Unatakiwa kuchagua sehemu nzuri ya kuweka huo mmea katika chumba husika. Epuka kuweka mmea karibia na moto au karibia na bomba la kuchemshia maji. Hakikisha kuwa sehemu uliyochagua inapokea mwanga wa jua wa kutosha kwa ajili ya afya ya mchakato wa usanisinuru (hii ni njia ya mimea ya kujitengenezea chakula kwa kutumiamwanga wa jua).

Unatakiwa kuchagua aina ya mimea ya ndani unayotaka kuweka.  Mimea na maua yanayofaa kuwekwa ndani ya nyumba ipo ya aina nyingi kwenye bustani za wauza maua. Mimea maarufu ya ndani ni ya jamii ya aloe vera, bambuu, kaktasi na magimbi. Wakati wakununua uliza mahitaji ya mmea husika kwa mfano kiasi cha jua, joto na maji kinachohitajika ili mmea ustawi vizuri. Nunua tu ile ambayo unaona utaweza kuitunza. Kumbuka walau mara moja kwa wiki zungusha chungu cha mmea kuwezesha mmea kukua kwa uwiano.

Mimea ya ndani inatakiwa kuwekwa kwenye vyungu vya mapambo kuendana na mapambo mengine yaliyopo hapo mahali. Vinaweza kuwa vyungu vya kauri vilivyochorwa kwa mikono au vyungu vya kisasa vya rangi ya silva inayong’aa pia vyungu vya kioo vinaonekana maridadi sana kwa maeneo ya sebuleni na chumba cha kulia chakula.

Kwa ujumla utunzaji wa mimea ya ndani  unahitaji muda na nguvu kidogo ingawa kuna matatizo yanayoweza kutokea na kuleta usumbufu mkubwa. Mojawapo  na kubwa la  matatizo haya ni ukungu ambao unaweza kujijenga kwenye udongo au majani ya mimea yako ya ndani. Ukungu ni jambo linaloweza kuleta uharibifu kwako na kwa mimea yako. Ikiwa basi tatizo la ukungu limejitokeza chukua kitambaa kilicholoa ushike jani kwa chini (ili kuliongezea nguvu  lisivunjike) na lifute, hii itaondoa ukungu wote unaoonekana. Usije ukajaribu kufuta na kitambaa kikavu kwani utaharibu sehemu ya juu  ya jani. Wakati majani yote yakiwa yameshafutwa, ruhusu mmea kukauka kwa kuuweka eneo ambalo linaingiza hewa.

Kama ukungu umeota kwenye udongo wa chungu basi ondoa eneo la juu na uweke udongo mwingine. Hata hivyo kama udongo utakuwa umevamiwa kwa kiasi kikubwa basi inashauriwa kuondoa udongo wote na kujaza chungu upya. Ongezea na dawa ya kuzuia fangasi kwenye udongo wa mimea yako ya ndani.

Hakikisha maji kwenye chungu yanatembea. Njia kuu ya ukungu kujijenga ni udongo kuwa na maji maji kwa kipindi kirefu. Kila chungu cha mimea ya ndani kiwe na ukanda wa kokoto ndogo chini ili kuruhusu mchanganyiko ulioko ndani ya chungu kukauka vyema. Hii inafanya mimea yako iwe na afya na kupunguza uwezekano wa ukungu kujijenga. Pia weka mmea wako wa ndani eneo ambalo linaingiza hewa kwa vile ukungu unashamiri eneo ambalo hewa ni hafifu.

Safisha mimea yako ya ndani mara kwa mara. Vumbi linajijenga kwenye majani ya mimea ya ndani kama linavojijenga kwenye  maeneo mengine ndani ya nyumba. Hili vumbi linafanya uchafu mwingine ujijenge juu ya majani na mmea kushindwa kufanya vyema usanisinuru hivyo kudhoofu. Kufuta majani mara kwa mara na kitambaa kilicholoa inasaidia kuondoa vumbi kujijenga kwa hivyo kuondoa uwezekano wa ukungu. Ondoa majani yaliyokufa mapema iwezekanavyo.

Mimea ya ndani inaweza kuwa na faida kubwa katika nyumba zetu na maisha yetu. Inaweza kuchuja hewa ndani ya nyumba na kufanya mazingira yenye afya. Hata hivyo ni vyema kuwa makini kwakuwa kuna mimea ambayo ni sumu kwa wanyama wa ndani kama vile paka na kadhalika na pia kwa watoto wadogo. Fanya utafiti wako vizuri na uone ni wapi pa kupamba na asili ndani ya nyumba yako. Chunguza mimea mbalimbali ambayo unaweza kupamba maeneo hayo na uone kama utunzaji wake utaendana na maisha unayoishi. Kama ukikwama pata ushauri kwa wataalamu wa mambo ya bustani na mimea. Wataalamu hawa watakusaidia kupata na kukuhakikishia mimea ya ndani  itakayokufaa.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment