Jinsi ya kuwa na mpangilio ndani ya kabati za jikoni
Iwe ni jiko la kwenye nyumba unayohamia au la siku
zote ikiwa mambo jikoni hayaendi kirahisi kama inavyotakiwa, kuweka mpangilio
kwenye jiko lako kutarahisisha mambo na vilevile kulifanya lionekane safi.
Kuweka vitu katika mpangilo ndani ya kabati za
jikoni kutaleta hisia mpya kwa chumba hiki ambacho kinatumika zaidi nyumbani.
Kabati za jikoni zenye mpangilio zitakusaidia kupata vifaa kirahisi na pia kukuzuia
usinunue vitu mara mbili mbili ambavyo tayari unavyo.
Kutokana na jikoni kuwa na vifaa vya aina mbalimbali
ambavyo vinatakiwa kuwa kwenye kabati basi inamuwia ngumu mhusika kuweka
mpangilio mzuri na ndio maana ni vyema kuwa na mkakati rahisi wa kupanga ambao
ni kuweka vifaa vinavyoendana pamoja.
Tosa kifaa chochote ambacho hukitumii. Mpe rafiki,
ndugu au gawa kwenye vituo vya kutoa misaada kwa jamii. Kuwa mkweli kwa nafsi
yako! Je ni lini mara ya mwisho kutumia hicho kimashine cha kusaga nyama au
hiyo chupa kubwa ya chai ya kutumika labda kwenye chumba cha mkutano wa watu 20
uliyopewa zawadi wakati fulani. Kama ni nyumba yenye familia changa labda chupa
hii ulipewa zawadi kwenye harusi yako. Vifaa vya kutengenezea juisi kama vile
blenda je ni kweli unahitaji kuwa na mbili? Je kuna jinsi rahisi ya kufanya
kazi fulani ama kupata hitaji fulani bila ya wewe kulitengeneza mwenyewe. Kwa
mfano ni jitihada kubwa utatumia kusaga nyama mwenyewe badala yake kwa nini
usinunue nyama iliyosagwa tayari? Kama utapunguza vifaa kama hivi kwenye kabati
zako ya jikoni basi utajipatia nafasi kubwa zaidi ya kuweka vitu vingine
ambavyo unavihitaji zaidi.
Kwa hivyo kabla hujaanza kupanga upya kwenye kabati
zako ya jikoni au kununua vifaa mbalimbali vya kuhifadhia, unatakiwa kuwa
makini sana kwa kuondoa mrundikano wote kwanza. Unavyoweza kutupa au kugawa
vitu vingi zaidi ndivyo utakavyokuwa na vitu vichache ambavyo kweli unavihitaji
na ukaweza kuvipanga na kuvihifadhi.
Baada ya kuondoa mrundikano ni wakati sasa wa
kupangilia vinavyotakikana kuwepo kwenye kabati za jikoni kwa jinsi ambayo
italeta maana unavyopika na muonekano wa jiko lako kwa ujumla. Kimsingi kuweka
mpangilio kwenye kabati za jikoni inamaanisha kupanga vyakula vyako, vifaa,
sufuria na vikaangio na zana nyingine za jikoni kwa njia ambayo inakurahisishia
maisha wewe na familia yako. Usidanganyike na mionekano; hakuna wewe bila wewe.
Jambo la muhimu la kuzingatia ni kuwa panga kwa jinsi ambayo kila kitu
unachokitumia mara kwa mara unaweza kukifikia kirahisi zaidi iwezekanavyo. Jagi
la vijiko na miiko karibia na stovu linasaidia kuweka vifaa vya kupikia karibu.
Rekebisha vitu ambavyo havifanyi kazi. Kama mkono wa
sufuria umevunjika; vitu vya aina hii vinaleta mrundikano kwa hivyo rekebisha
au ondoa ununue nyingine. Kama huwezi kununua nyingine kwa wakati husika basi
weka kwenye orodha ya mahitaji yako kwa siku za mbeleni.
Hifadhi vifaa vinavyotumika mara kwa mara maeneo
ambayo yanafikika kirahisi. Angalia ni kifaa gani unatumia zaidi. Vifaa ambavyo
hutumii mara kwa mara kama vile tuseme kikaangio ambacho unatumia mwishoni mwa
wiki tu au wakati wa likizo vinaweza kuwekwa juu kabisa ya mashelfu au mwisho
kabisa ndani ya kabati. Vinaweza hata kuhifadhiwa stoo badala ya kwenye kabati
za jikoni.
Hakikisha kila kifaa kwenye kabati zako ya jikoni
yana haki ya kuchukua nafasi yako hiyo ya thamani! Vifaa vyote usivyotumia mara
kwa mara viwekwe mbali bila kujali thamani ya kifaa, kama unatengeneza keki
mara moja ndani ya miezi sita basi bakuli la kuchanganyia na vifaa vyote vya
kutengeneza keki vihifadhi stoo.
Tazama kwa umakini vifaa ambavyo ni vya kudumu juu
ya kaunta. Kaunta inatakiwa kusafishwa mara kwa mara kwa vile ni eneo lako la
msingi la kufanyia kazi. Weka kwenye kabati vifaa vingine ambavyo kwa kweli
havina ulazima wa kukaa kaunta.
Kupangilia vifaa kwenye kabati kuendane na kusafisha.
Ukishasafisha droo moja au shelfu, tandika zile karatasi za kwenye kabati la
vyombo kabla hujaanza kupanga vitu. Kusafisha na kupanga kwa wakati mmoja kunarahisisha
kazi. Tumia kabati za chini kwa vifaa vizito na zile za juu kwa vifaa vyepesi
kama glasi za mvinyo na vitu ambavyo unatumia mara kwa mara na unataka
ukinyoosha mkono tu unabeba. Mfano ni chumvi na viungo vya kusaga vya vyakula.
Chagua kontena zitakazoendana na mahitaji ya chakula
kinachohifadhiwa humo. Kontena zenye mifuniko ni sahihi kuzuia chakula kisimwagike wakati zile
zinazozuia hewa isipite ni sahihi zaidi kwani zinafavya chakula kikae muda
mrefu bila kuharibika. Chagua kontena za ukubwa wa kutosha za kuweka vyakula
ndani ya kabati. Vyakula hivi ni kama sukari, unga, mchele na kadhalika.
Kontena ndogo ndogo zinafaa kwa ajili ya viungo vya kusaga vya vyakula. Kontena
za kuhifadhia vyakula kwenye kabati ya jikoni zikiwekwa majina ni bora zaidi
kwani mpishi ataweza kutofautisha kirahisi kati ya kontena la unga wa ngano na
la unga wa mahindi.
Mara kwa mara kagua uwezekano wa kuwepo kwa mende na
wadudu wengine kwenye kabati za jikoni kwani wadudu hawa wanaweza kuharibu
vyakula vyako. Unaweza kuweka vidonge vya kuua mende kabatini au unga wa kuua
wadudu au hata ukaamua kupuliza dawa mara moja kila baada ya miezi sita.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
INAPENDEZA ..................
ReplyDelete