Furahia bustani yako hata baada ya giza kuingia
Kwa wale wenye bustani zao binafsi, kutumia muda
bustanini ni wasaa wanaoupenda sana. Eneo la nje la bustani ni moja ya vitu
vichache vya thamani unavyopata katika ulimwengu huu ambapo unaweza kukaa, kustarehe,
kufurahia na kushangaa uzuri wa mimea na hewa ya asili. Kuwa na mwanga wa
kutosha bustanini nyakati za usiku mara nyingi inawaruhusu wenye bustani
kurefusha muda wanaoweza kutumia kwenye eneo hili la nje ya nyumba zao.
Ili kuweza kuwa na mwanga kwenye bustani inabidi
kuweka taa za bustanini mbali na zile za ulinzi. Taa hizi zinarahisisha maisha
ya usiku ya kwenye bustani na zipo za aina mbalimbali kama vile za kuonyesha
njia, zenye matawi zinazowekwa kwa ajili ya kusisitiza eneo fulani la bustani, za chini ya
maji kwa mfano kwenye bwawa au maanguko ya maji na zile zinazoweza kutundikwa kwenye
miti.
Taa za bustanini zina malengo mawili: kuangaza na
kupamba. Kama zilivyo nyanja nyingine za ubunifu wa bustani, malengo haya
mawili yanaendana bega kwa bega ili kuleta muonekano wa bustani ya kuvutia.
Ingawa mmoja anaweza kumulika bustani nzima kwa kuweka taa za mwanga mkali na
kuondoa dalili yoyote ya giza, hii italeta muonekano usiovutia. Vilevile
mwingine anaweza kuweka taa chache tu za kusaidia miguu kuona eneo la kukanyaga
kwenye njia ya bustani. Hata hivyo hii itafanya eneo lingine lote la bustani
kubaki karibia sawa na giza, kumzuia mtazamaji kufurahia uzuri wa bustani
usiku.
Mpango wako wa kuweka mwanga kwenye bustani
unatakiwa kuweza kuleta suluhisho kwa hali zote hizi mbili. Nia ya mwanga
kwenye bustani ni rahisi. Chagua ni nini kwenye bustani yako ungependa
kionekane zaidi kwa wageni wako, na ni shughuli gani unayotaka kuifanya kwenye
bustani.
Je huwa unaburudisha kwenye bustani yako? Kama una
varanda au fenicha kwenye bustani yako, fikiria mfumo wa mwanga kwenye bustani
ambao utaruhusu wageni kufurahia bustani usiku nyakati za kiangazi. Kama wewe
ni mmojawapo wa wanaopenda kualika wageni chakula cha usiku kwenye bustani yako
hakikisha mfumo wa mwanga unawezesha mgeni kuona anachokula toka kwenye sahani
yake. Kama una watoto wanaopenda kucheza kwenye bustani usiku hakikisha una taa
moja au mbili za mwanga mkali ambazo unaweza kuwasha wakati wa michezo na
kuzizima michezo ikiisha.
Kila mwenye bustani lazima ana walau ukanda mmoja au
zaidi wa maua, au eneo mojawapo kama vile bwawa au hata mti ambao unaufurahia.
Weka mfumo wa mwanga kwenye bustani ambao utawezesha wageni wako kuona vitu
unavyopenda waone kwenye bustani yako usiku kama vile wangeweza kuviona
machana. Kwa mfano taa zenye matawi zinafaa sana kumulika eneo fulani la
bustani kulifanya lionekane zaidi kuliko maeneo mengine wakati wa usiku.
Taa za chini ya maji ni aina ya taa za bustani
zinazowekwa maeneo ya kwenye bwawa, maanguko ya maji na maeneo mengine
yanayofanana na hayo. Taa hizi huwa zinawekwa chini ya eneo la maji ili kusaidia
kufanya eneo hilo lionekane zaidi nyakati za usiku. Na huwa taa hizi zipo hata
za rangi kwa nia ni ile ile ya kuonekana zaidi na vile vile kuleta staili.
Taa za mwanga mkali za kwenye bustani pia zinaweza
kutumika kama taa za ulinzi. Taa hizi zinaweza kuunganishwa na vihisi mwendo
(motion sensor) ambapo ikiwa mvamizi atatokea anazama kwenye mwanga mkali hivyo
kukwamisha mkakati wake wa kivamizi.
Kimsingi, mpango mzima wa mwanga kwenye bustani
uwekwe kwa jinsi ambayo mgeni halazimiki kujua umbo la taa bali kuona mwanga
tu. Cha muhimu ni aone vile vinavyomulikwa, vile unavyotaka aone kwenye bustani
yako, pengine ni mti, njia, bwawa, maanguko ya maji na kadhalika. Kwa hivyo taa
za bustani zilizowekwa kwenye urefu wa kutosha wa kile unachotaka kionekane zitasaidia
kukionyesha kitu hicho tu huku kukiwa na kivuli maeneo ya jirani hivyo kuleta
mvuto wa aina fulani ukilinganisha na kuona kitu kile kile wakati wa mchana.
Kwenye mfumo wako wa taa za kwenye bustani unaweza
ukachanganya pia taa za rangi. Taa za rangi za kwenye bustani zinatumika zaidi
kama mapambo ya msimu wa sikukuu. Hata hivyo
taa za rangi zilizowekwa kwenye mpangilio wenye ladha unaweza kuongeza
uzuri wa muonekano mzima wa bustani. Aina fulani ya maua inaweza kubadilika
kabisa kutokana na kumulikwa kwa taa za rangi wakati mengine yanaweza kufunikwa
yasionekane. Na unaweza kuwa na balbu moja au mbili za rangi mkononi mahususi
kwa kubadili na zilizopo kuendana na msimu.
Wakati wa kuchagua taa za bustani fikiria mimea na
vitu vingine kwenye bustani yako vinavyoakisi mwanga kwa sana. Mimea na vitu
visivyoakisi mwanga kwa sana vinahitaji mwanga mkubwa zaidi kuvifanya
vionekane.
Hata kama mfumo wa mwanga wa kwenye bustani
haukuhusishwa kwenye mpango wa awali wa bustani unaweza kuweka taa za jua na
paneli za kuchaji wakati wa jua badala ya zile za kutumia umeme ambapo hizi za
umeme zinahitaji kutandika nyaya tokea awali na kadhalika. Kwa hivyo taa hizi
za kutumia mwanga wa jua zinakuwa bei nafuu kwa kuwa bustani yoyote inapokea
mwanga wa jua bure.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment