Unavyoweza kuhifadhi taulo zako za bafuni
Ni bafu chache zenye sehemu ya kutosha kwa ajili ya
kuhifadhi taulo. Lakini usijali kwani hata kama bafu lako ni dogo namna gani
njia mojawapo kati ya hizi itakufaa kutundika ama kuhifadhi taulo zako.
Kuweka fimbo za kutundika taulo kwenye ukuta wa bafu
ama nyuma ya mlango (uwe wa mbao kwa uimara) ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi
taulo zako. Fimbo za kutundikia taulo hazichukui nafasi kubwa na wala hazina
marembo kwa hivyo ni suluhisho tosha kuhifadhi taulo zako kavu na hata zile zenye
unyevu. Fimbo za taulo zinaruhusu taulo kukauka kwa usafi zikiwa zimetundikwa
kwa kukunjwa nusu. Fimbo za bafuni za kuwekea taulo zinasaidia mambo makubwa
mawili: kwanza, zinaweka taulo kavu na safi kwa jinsi ambayo ni rahisi kuchukua
na kutumia; pili, zinatandazwa taulo zenye unyevu na kuzifanya kukauka rahisi,
kwa hivyo kuzuia kuota kwa ukungu. Licha ya kufungwa bafuni fimbo za taulo zinaweza
kufungwa pia jikoni kwa ajili ya kuwekea taulo za mkononi.
Muonekano wa fimbo za taulo ni kawaida sana. Ni
fimbo iliyowekwa ukutani ama nyuma ya mlango kwa kutumia mashine ya kutobolea
ukuta na taulo huwekwa hapo, hutolewa kutumika na hurudishwa tena hapo baada ya
kutumika kwa ajili ya kukauka. Ni muhimu fimbo hizi ziwe zimeweka imara kwa kuwa kama tujuavyo taulo zikiwa mbichi
zinakuwa nzito na pia mara nyingine fimbo hizi hutumika na watoto (wakati
mwingine ni kwa utundu wao wa kupenda kubembea kila waonapo panafaa) ama wazee
kujishikilia wakiwa bafuni. Kwa hivyo siwezi kuacha kusisitiza kuwa fimbo za
taulo ni lazima zifungwe kwenye ukuta wa tofali ama mlango wa mbao kwa ajili ya
uimara.
Fimbo za kuwekea taulo zinapatikana kwenye maduka ya
fenicha za nyumbani na zimetengenezwa kwa chuma. Saizi ambazo ziko kwa wingi ni
inchi 18 kwa ajili ya taulo za mkononi na inchi 24 kwa ajili ya taulo za
kuogea. Hakikisha umeshatathmini bafu lako na kuamua ni wapi pa kuchimbia fimbo
ya taulo na uone pana nafasi ya kutosha urefu wa fimbo zilizopo sokoni.
Fimbo za taulo sizo tu zinazoweza kuhifadhi taulo kwa
usafi na kuruhusu zile zenye unyevu kukauka. Kulabu (hook) za taulo, susu
(rack) za kusimama wima, bangili na ngazi za taulo nazo ni njia nyingine za
kuhifadhi taulo za bafuni. Bangili iliyotobolewa ukutani ambapo taulo kadhaa
zinatundikwa ni maarufu sana siku hizi na kwenye maduka ya fenicha wanaziita bangili
za taulo. Chuma kingine kinachoonekana kama ngazi ndogo ambacho hutumika
kuwekea taulo nacho ni njia mojawapo ya kuhifadhi taulo za bafuni. Je una
nafasi kwenye ukuta wa chumba chako cha kulala ambapo unaweza kuweka ngazi hii?
Ni kiasi cha kuishikilia na braketi juu ili isianguke na unaweza kuhifadhi kwa
kutandaza taulo zako za kuogea. Uzuri wa ngazi ya taulo ukilinganisha na fimbo
ni kuwa wakati kwenye fimbo unaweza kuweka taulo zisizozidi 2 kwenye ngazi ya
taulo unaweza kuweka hadi taulo 6.
Lakini kuna njia nyingine ambazo hazitakufanya
uusumbue ukuta wako ambazo zinaonekana za kimapambo zaidi kwa mfano kuweka susu
ya kusimama inayojitegemea kama ile ya kutundika makoti ofsini. Kama chumba
chako cha kulala kina nafasi kidogo ya ziada basi simamaisha susu ya koti kwa
ajili ya kutundikia taulo za bafuni. Susu inaweza kutundikwa taulo kadhaa kwa
wakati mmoja. Fikiria kuiweka sehemu ambayo inaingiza hewa au vinginevyo uwe
unazigeuza mara kadhaa kuwezesha kukauka. Kama susu hii inatundika taulo za
wanafamilia tofauti basi wawe na taulo za rangi tofauti kwa kila mmoja. Hakuna
anayependa kushirikiana taulo.
Badala ya ile susu ya kusimama kuna hii nyingine inayofanana
na ya kuhifadhia chupa za mvinyo. Baadhi ya watu hawafikirii kutumia taulo za
bafuni zaidi ya mara moja kabla hawajaziweka kwenye kapu la nguo chafu ili
kufuliwa. Nenda kistaili zaidi kwa kuhifadhi taulo zako safi zilizobiringishwa
vizuri kwenye susu ya taulo. Susu za taulo zina muonekano wa kuvutia kwa hivyo
kwa upande mwingine ni kama pambo. Taulo safi zinabakia zimebiringishwa vizuri
ndani ya susu hadi wakati wa kutumiwa, na hii inachukua nafasi kidogo kuliko
ile susu ya kusimama. Kuhifadhi taulo kwa kutumia susu ya taulo inakubidi uwe
ni mtu wa kutumia taulo mara moja tu na kulifua.
Kwa hivyo kama ulijisikia kwamba bafu lako ni dogo
kiasi kwamba huna mahali pa kuhifadhi taulo zako hatimaye leo umefahamu njia
kadhaa za kuweza kuhifadhi na kutunza taulo zako wakati huohuo ukiwa
unazitumia. Wekeza katika njia mojawapo kati ya hizi ili kurahisisha maisha
bafuni.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment