Karibu
msomaji kwenye makala ya leo ambayo
nitaongelea jinsi ya kupamba chumba cha kulala cha binti yako miezi michache
kabla hajazaliwa hadi akiwa na umri wa miaka 18. Fuatana nami kwenye makala hii.
Sasa basi ni miezi michache
imebaki kabla binti yako hajazaliwa. Kutokana na teknolojia kuwa juu mama
mjamzito amepewa uwezo wa kujua jinsia ya mtoto wake aliye tumboni kama
atapenda kufanya hivyo. Endapo basi wazazi watakuwa wanatarajia kuna binti yao
anakuja duniani basi moja kwa moja wanaanza kufikiria kitanda cha mtoto na nguo
na mapambo ya rangi za pinki, njano na kijani ambazo zitatawala chumba cha
kijacho. Wakati ukiwa kwenye maandalizi hayo ni vyema ukaandaa kwa kufikiria
miaka mitano hadi kumi mbeleni.
Kutokana na ukali wa maisha
jaribu kuweka vitu ambavyo ni vya kudumu kwa kukumbuka kuwa kila kitu
unachoweka kwenye chumba hiki ni chake na atakitumia kwa miaka 18 inayofuata na hata kama ni mabadiliko yawe madogo yasiyo
na gharama kubwa. Sasa utaniuliza je, kitanda cha mtoto kitatumika kwa miaka
18? Endelea kujisomea ili upate jibu la
hili swali. Rangi za pinki, njano na kijani nazo pia ni sawa kwa chumba cha mtoto
wako wa kike mchanga lakini jaribu kutumia rangi ambazo zinakaa kati. Kwa mfano
ukitumia pinki iliyokolea na njano ya mwanga wa jua kama rangi za ukuta wa
chumba cha binti yako vitadumu hata atakapokuwa mkubwa na ataipenda pinki hii
kuliko ile nyepesi ya kitoto!
Kununua fenicha ambazo zina
matumizi zaidi ya moja na ambazo zinaweza kukaa kwenye chumba hicho kwa muda
mrefu inaweza kuwa changamoto kuliko swala la rangi. Unahitaji kutembelea
maduka mbalimbali ya fenicha na pia karakana za waseremala. Wote tunajua kile
kitanda cha kichanga binti yako hawezi kukitumia kwa miaka 18 ijayo. Ni sawa
kuwa na kitanda cha mtoto kwa ajili kina vizuizi pembeni ili asianguke. Ila ili
kuweza kuwa na matumizi ya kitanda hiki kwa umri wote wa utoto wa binti yako
tafuta kitanda cha bebi ambacho kinaweza kugeuzwa na kuwa cha binti hapo baadaye.
Kuna baadhi ya maduka ya fenicha ambayo unaweza kupata kitanda kama hiki.
Vinginevyo unaweza kwenda kwenye karakana za waseremala na kuagiza utengenezewe
kitanda cha kikubwa ila kiwekwe vizuizi ambavyo vitafanya kazi kama ile ya
kitanda cha bebi.
Hapo baadae kadri binti yako
anavyokua unapamba chumba chake upya ambapo utaondoa vizuizi na kitabakia kuwa
kitanda cha binti na sio bebi tena. Mzazi siku hizi usitafute kitanda cha bebi
kinachosimama peke yake.
Tafuta ambacho bebi yako pia atakitumia akiwa binti,
kwa njia hii utakuwa umetumia pesa yako kwa busara. Usitumie hela nyingi na
uchumi huu kununua vitu ambavyo utaviondoa tena miaka michache itakayokuja. Kama
unataka kuongeza kitu kwenye chumba cha mtoto wako ambacho anafurahia sasa
lakini sio hapo baadaye hakikisha sio cha gharama kubwa na ni rahisi kukiondoa.
Chumba
cha kulala cha binti yako ni sehemu ambayo atatumia muda mwingi zaidi wakati
akiwa msichana mdogo, atakuwa analala hapo pia wakati mwingine atacheza na madoli
yake hapo. Kuwa mbunifu kwenye kupamba chumba hiki na utumie gharama za
kawaida. Weka zulia la rangi moja ambalo
utaweza kutupia kizulia kingine kidogo cha rangirangi juu yake pale pembeni ya
kitanda. Kizulia hili kidogo rangi kuu ziwe zinaendana na rangi nyingine za
hapo chumbani hata kama ni pazia ama shuka ama ukuta. Zulia litasaidia kuweka
miguu ya bintiyo kwenye joto na hata akiwa amekaa chini na pia linaongeza uzuri
wa muonekano wa chumba. Mwekee shuka, mito na pazia zinazooana na rangi ya mandhari
uliyochagua. Chagua pazia na shuka za kike na pia zenye rangirangi kama maua au
nyota au hata rangi za upinde wa mvua.
Hatimaye binti yako mdogo
anaanza chekechea; muda unakimbia. Weka mpangilio wa chumba kivingine ili kutengeneza
nafasi kubwa ya kucheza na matoi na kusuka madoli yake. Kadri binti anavyokua,
ladha yake inabadilika kwa kasi siku hadi siku achilia mbali mwaka hadi mwaka.
Unaweza ukatetea kutumia hela kwa umakini kwa ajili ya chumba chake kwa kujua
ni nini cha kununua na jinsi ya kukitumia.
Unapamba chumba chake tena
kwa awamu nyingine ya kikubwa. Chagua mandhari itakayotokana na vitu na rangi
anazopendelea binti yako kabla ya kumshtukiza na kuanza kupanga na kuweka vitu
upya chumbani kwake. Pia unaweza kupamba nae pamoja. Anza kwa kupaka tena rangi
na baada ya hapo ongeza fenicha ambazo bintiyo atahitaji ambazo ni kimeza na
kiti chake , meza ya kuvalia, kisofa kidogo na kishelfu cha vitabu.
Rangi ya
vitu hivi iendane na mandhari uliyochagua. Kwa mfano kama mandhari ni rangi ya
pinki, usiweke sofa ambalo halioani na pinki. Pia sasa ni wakati wa kuondoa
zile mbao za kuzuia asianguke na kitanda kubakia cha binti mdogo sio kile cha
kichanga tena.
Kwenye droo za hiyo meza ya
kuvalia hifadhi vitu vyake vya michezo na vitu vidogovidogo viwekwe humo
visitupwetupwe. Kwenye droo hizo weka kwa mpangilio ili asipate shida kuona
vitu. Kama kutakuwa na nafasi ya ziada pia weka kiti cha kubembea. Mabinti
wanaokua wanakipenda kukalia wakati wa kusoma kitabu cha hadithi, gazeti au
jarida. Kwa ajili miaka imeenda kile kizulia cha rangirangi ulichotupia juu ya
lile zulia la rangi moja unaweza ukakibadilisha kwa kumnunulia kingine. Maadam sasa ni mkubwa
ataweza kuchagua rangi anazopenda ambazo zitaoana na zingine hapo chumbani.
Baada ya hapo unaweza
ukaenda na bintiyo kweye maduka ya mapambo ya ndani akachagua vitu vidogodogo
vya kuongezea kama taa za vivuli fremu za picha, kifungashio cha kalamu na
penseli kwenye deski lake, mishumaa na kibox cha kuweka hereni na mikufu na
vitu vyake vingine vya urembo. Na pia kama atapenda waweza mwekea vioo vya
ukutani. Sasa kitu pekee anachohitaji kwenye lile deski ni kompyuta. Mzazi usione
bintiyo anataka kutumia kompyuta yako ukamfukuza. Ni muda wake nae kuwa na yake
kwake.
Kwa majumuisho, pamba kwa
jinsi ambayo chumba kinakuwa na mwanga wa kutosha na sehemu kubwa ya kuhifadhi
vitu ili asitupetupe vitu chini kwa madai ya kuwa hakuna nafasi ya kuweka.
Mwanga wa kutosha na deski ni kwa ajili ya kujifanyia kazi zake za shuleni. Na
kama unapenda binti yako ajenge tabia ya kujisomea basi usidharau umuhimu wa
kumwekea shelfu la vitabu kwenye chumba chake kuweka vitabu vyake vya zamani na
vipya mahali pamoja.
Hongera! Umefanikiwa kupamba
chumba cha binti yako toka akiwa bebi hadi miaka 18 bila usumbufu mkubwa, muda
au pesa nyingi!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment