Sunday, July 5, 2015

ILANI YA UCHAGUZI CCM YAIVA..

KIKAO Maalumu cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza jana Mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kupitisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

Kikao hicho ni mwanzo wa vikao vinavyotarajiwa kuanza mapema wiki ijayo, kwa ajili ya kuchuja majina ya walioomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya muda wa kurejesha fomu kwa wanaowania kuteuliwa kugombea urais kumalizika, vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea vinatarajiwa kuanza vikitanguliwa na Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kitakachokutana Julai 8, mwaka huu.

Kikao cha Kamati Kuu kinachotakiwa kujadili wagombea 38 na kuja na majina yasiyozidi matano kinatarajiwa kukutana Julai 9.
Majina hayo yasiyozidi matano, yanatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ambayo itakutana Julai 10.

Kikao hicho cha NEC, kinatarajiwa kupitia majina hayo na kuja na majina matatu, yatakayopelekwa katika Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika Julai 11 na Julai 12 utakaoteua jina moja la mgombea urais wa CCM, baada ya kupigiwa kura na wajumbe wote wa mkutano huo.

CC maalumu Zanzibar
Wakati huo huo, Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya (CCM) Zanzibar, inatarajiwa kukutana kesho mjini Zanzibar kupendekeza jina la mgombea wa urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Makao Makuu ya CCM, White House Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ally Vuai, alisema kikao hicho maalumu kitafanyika katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya chama hicho Kisiwandui Zanzibar.

Alisema mpaka sasa kuna mgombea mmoja ambaye ni Rais aliyepo madarakani, Dk Ali Mohammed Shein, ambaye alichukua fomu na amesharudisha.
Kwa mujibu wa Vuai, Kamati hiyo itapendekeza jina litakalopelekwa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na baadaye jina hilo litaenda mbele ya kikao cha NEC kitakachofanya uamuzi wa mwisho.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 114 (b) Kamati hiyo pamoja na kazi nyingine, ina kazi ya kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, juu ya wanachama wanaoomba nafasi ya Rais wa Zanzibar, ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,” alisema Vuai.

Wajumbe wa Kamati hiyo Maalumu kwa mujibu wa Ibara ya 113, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar anayetokana na CCM na Makamu wa Rais wa Zanzibar anayetokana na CCM.

Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu ya NEC wanaotoka Zanzibar, wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Zanzibar, Makatibu wa CCM wa Mikoa ya Zanzibar na wajumbe wote wa NEC Taifa wanaotoka Zanzibar.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment