Friday, August 26, 2016

Unavyoweza kupendezesha ukuta kwa zulia la kutundika

Hivi ulishawahi kukutana na zulia ambalo unaona ni zuri mno kwamba halistahili kuwekwa nyumbani kwako? Au umependa rangi na michoro yake lakini hujui uliweke wapi? Wengi wanadhani kwamba zulia ni kwa ajili ya kupamba sakafuni tu. Leo hii nakufahamisha kuwa si kweli! Historia inaonyesha kuwa kupamba ukuta kwa kutundika zulia ni utamaduni ulioanzia kwenye makasri ya kifalme. Kazi za sanaa zinazoonekana kwenye zulia zilitambuliwa kama ishara ya utajiri.
Zulia zuri kwa michoro na rangi linaweza kuwa silaha tosha kwa kupendezesha kuta za ndani mwako.

Baadhi ya washauri wa mapambo ya nyumba wameshagundua jambo hili na kuchukua hatua ya kulitoa zulia sakafuni na kulihamishia ukutani. Unalitundika kama lilivyo hakuna kuliwekea fremu. Chagua ukuta unaotaka kulitundika na liweke kwa jinsi ambayo litaning’inia katikati ya ukuta huo.

Kwa kawaida kupendezesha ukuta mkubwa na mpana inaweza kukuwia ngumu. Inawezekana huna muda wa kutengeneza ukuta wa sanaa au hata pengine bajeti ni kubwa na njia nyingine kama vile ya kubandika karatasi za ukutani ni kwamba yote haya yanahitaji muda na hela ili kufanikisha.  Badala ya kufuata njia tuliyoizoea ya kutundika picha na sanaa za ukutani, tundika zulia la kuvutia na utashangaa ni kwa jinsi gani litakamilisha ukuta mweupe. Kutokana na rangi na michoro iliyoko kwenye mazulia, linapendeza pale linapokuwa limetundikwa kwenye ukuta na chumba kikubwa. Zulia zuri linaleta muonekano wa kuvutia ukutani kuliko hata ilivyo kwa sakafuni.

Linapokuwa sakafuni, lengo la zulia ni kuleta mshikamano wa chumba, kuvuta pamoja michoro na  rangi kadhaa zinazoonekana kwenye fenicha na mapambo mengine yaliyopo hapo lilipo. Kama ilivyo kwamba sanaa ndogo ndogo zenye kazi za kuwaka zinasaidia kuchangamsha chumba chenye rangi na fenicha  zilizopoa, kutundika zulia ukutani kama mbadala wa hizo sanaa  kunatimiza malengo yote kwa kuua ndege wawili kwa jiwe moja huku ukiipa sakafu nayo nafasi nyingine ya kupendezeshwa. Rangi zinaweza kuhitajika kwa ajili ya chumba fulani kwahivyo zulia la ukutani litasaidia kutimiza lengo hilo bila kuongezea sanaa nyingine zozote za ukutani.

Kama ilivyo sakafuni, michoro ya zulia lililotundikwa ukutani inaweza vilevile kutengeneza muendelezo wa kushirikisha muonekano wa vitupio vidogodogo ambapo inaleta hisia za kuwa kitu kimoja kizima kilichokamilika. Kutundika zulia kwa mtindo huu kunalipa jicho fahari ya kuliangalia.

Rangi na michoro iliyopo kwenye zulia la kutundika ukutani hazina kikomo cha kuoanisha na vitu vingine kama mito ya kwenye makochi au utepe wa mezani. Moja ya faida kubwa ambayo zulia linatoa ni wigo mpana wa rangi au michoro ambapo isingewezekana hivyo kwa sanaa yoyote ya ukutani.

Zulia la kutundikwa ukutani lina uwezo wa kuunganisha rangi zote kuanzia nyeusi na nyeupe kadri utakavyolichagua kuendana na mahitaji yako ya rangi na michoro katika ukuta unaotaka kulitundika.
Zulia unalotaka kutundika ukutani hata kama ni jipya hakikisha kuwa unalisafisha kwanza. Usitundike zulia chafu.

No comments:

Post a Comment