Friday, August 12, 2016

Zingatia haya unaponunua mapambo mitandaoni


Kwa wengi wa Watanzania walioko mijini kununua vitu mitandaoni kunakuja kwa kasi siku hizi. Imewarahisishia wanunuzi wengi  wasio kuwa na muda au uvumilivu wa kuzunguka kwenye maduka kununua vitu mbalimbali na hapa nitazungumzia mapambo ya nyumbani. Uwepo wa mitandao kama instagram, facebook, website na hata whatsapp umechangania kurahisisha manunuzi mitandaoni kwani uzuri ni kwamba unanunua na kuletewa ulipo.

Hata hivyo kila kitu kina changamoto zake na
hapa nimekuandalia mambo7 muhimu ambayo unatakiwa kuyazingatia unapoamua kununua mapambo ya nyumbani mitandaoni.

Linganisha bei kwa wauzaji zaidi ya mmoja
Unapokuwa unalinganisha bei ya bidhaa hiyo hiyo kwa wauzaji zaidi ya mmoja kuna uwezekano mkubwa wa kuikuta ikiwa katika bei ya chini kwa muuzaji mwingine. Hii itakusaidia mwishoni kupata dili zuri.

Nunua kwa muuzaji mwenye bidhaa nyingi
Biashara nyingi hazikosekani wachuuzi kwahivyo zingatia kununua kwa wenye mali na sio mchuuzi. Unaponunua kwa mwenye mali kuna uwezekano mkubwa wa kupata faida kadhaa kama vile kubadilisha bidhaa na kuchukua nyingine kama utakuwa hujaipenda au ina kasoro na pia kupata punguzo la bei.

Ulizia vipimo halisi
Sio wauzaji wote wa mitandaoni wanafahamu hasa bidhaa wanayouza. Kwa kawaida mitandaoni tunanunua kwa kuona picha, na huwa mara nyingine zinadanganya. Hakikisha muuzaji anakupa vipimo halisi vya bidhaa unayotaka kununua. Hakuna kitu kinaudhi kama kunununua  kitu mfano  shuka au picha ya ukutani halafu ukaja kukuta kuwa haina ukubwa wa kukidhi hitaji lako.

Kuwa makini na rangi
Kamwe usiamini rangi ya picha unayoona mtandaoni kwani inawezekana kabisa ikawa sio sawa na ya bidhaa halisi. Usishangae kuletewa bidhaa ya rangi tofauti kabisa na uliyotegemea kwahivyo ni muhimu kujiandaa kwa hali hiyo endapo itatokea ufanyeje. Unaweza kumtaka muuzaji akuthibitishie rangi kabla hujanunua.

Fahamu kama unaweza kurudisha
Pambo fulani linaweza kuonekana kuwa na mvutio sana mtandaoni, hata hivyo ukajikuta kuwa hujalipenda sana kwa uhalisia wake. Kama umenunua kwa muuzaji ambaye haruhusu kurudisha ni kwamba utakuwa umepoteza hela yako.

Fahamu malighafi iliyotengenezea bidhaa
Kwa mfano bidhaa nyingi za mbao ngumu ni gharama sana. Unapotaka kununua mapambo kama meza ya kahawa au kabati la luninga hakikisha kuwa hufanyi uamuzi kabla ya kufahamu malighafi iliyotumika kutengenezea bidhaa hiyo.

Fahamu maingizo mapya
Huenda hujapenda bidhaa zilizopo kwa sana, ila uzuri ni kwamba karibia kila mtandao una jinsi ya kumjulisha mfuatiliaji pale kunapowekwa ingizo jipya. Kama unapendelea kufahamu kinachoendelea kwenye ulimwengu wa mapambo ya nyumbani basi jiandikishe kwenye mitandao hiyo ili uhabarike kila wanapoweka ingizo jipya.


Kununua mapambo ya ndani mitandaoni inaweza kukurahisishia sana maisha kwani unaletewa hadi ulipo. Cha muhimu ni kuzingatia dondoo hizi.

No comments:

Post a Comment