Monday, August 8, 2016

Namna rahisi ya kusafisha sakafu ya marumaru


Zaidi ya uzuri uliotukuka, sakafu ya marumaru ina faida kuu ya kuwa ni rahisi kusafisha na kutunza pia. Ni sakafu imara na pia chaguo la wengi wenye nyumba za kisasa. Wapo wanaochagua kuwa na sakafu hii kwenye nyumba nzima na wapo ambao wanaiweka sehemu chache kama vile katika vyumba vya jiko, bafu na maeneo mengine ya nyumba ambayo yanaweza kuloa maji kirahisi wakati wowote. Kwenye vyumba vingine watu hao wanatumia sakafu za aina nyingine kama vile zulia na mbao.

Marumaru zenyewe zimetengenezwa kwa jinsi ambayo hazinyonyi uchafu ila
changamoto kubwa iko kwenye yale maeneo yanayounganisha marumaru moja na nyingine hatimaye kufanya muonekano wa sakafu. Sakafu ya marumaru ikisafishwa vizuri inaweza kuonekana kama mpya hata baada ya miaka mingi. Pamoja na kwamba sakafu hii ni rahisi kusafisha, tuangalie mbinu za kufuata huku tukikumbuka pia hatupaswi kuzidisha kiwango cha kusafisha.

Fagia kila siku. Hii inasaidia kuondoa uchafu wa juujuu kama vile mabaki ya vyakula au kutokana na viatu vilivyoingizwa ndani vikiwa na chembechembe za uchafu kwenye soli zake.

Unapaswa pia kufagia kabla ya kudeki. Pitisha dekio au mopu sakafuni baada ya kuwa imeshafagiliwa.

Deki sakafu kwa maji safi yenye sabuni kidogo na tambara au kama unatumia mopu  iwe safi pia. Kama sakafu haina madoa ambayo yanahitaji usafi wa kusugua, kutumia mopu na tambara inatosha kuifanya iwe safi. Safisha tambara au mopu mara kwa mara unapokuwa unasafisha sakafu toka chumba au eneo moja hadi lingine. Kwa mng’ao wa kutosha angalau safisha sakafu yako ya marumari kwa maji kila siku.

Kausha sakafu. Baada ya kuwa umetumia maji na mopu iliyoloa, sasa ni wakati wa kutumia mopu kavu pekee kwa lengo la kukausha sakafu ili hata uchafu wowote ukiwa umeingia usigandie kwenye maji. Uchafu ukiruhusiwa kubaki kwenye maeneo yaliyoloa unaweza kung’ang’ania na kugeuka mara moja kuwa mgumu kusafisha wakati unaofuata.

Vilevile kukausha sakafu ya marumaru baada ya kuideki ni muhimu sana kwa usalama wa wanafamilia wasiteleze kwani haina kawaida ya kuonyesha kirahisi kuwa sehemu fulani ina maji.

Hata baada ya kumaliza zoezi hili endapo kuna chochote kimemwagika sakafuni ni vyema kukisafisha hapohapo. Kwa ajili kadri uchafu unavyobaki pale ndivyo unavyozama kwenye maungio ya marumaru na kutengeneza doa eneo hilo. Baadhi ya vimiminika kama vile chai ya rangi, kahawa au soda nyeusi pale zinapomwagika sakafuni na kukaa muda bila kusafishwa zinachangia sana kuharibu uzuri wa marumaru.


Vivyohivyo ikiwa umedondosha nyama mbichi, iokote mara moja, weka sabuni na maji na pasafishe.

No comments:

Post a Comment