Tuesday, September 13, 2016

Maswali matano ya kujiuliza kabla hujanunua sofa

 
Sofa mpya ni gharama na kwa bei ya chini kabisa ya seti nzima si chini ya shilingi milioni moja. Nimehojiana na wauzaji na wabunifu wa sofa na kuwauliza utaalam wao wa nini mnunuzi azingatie kabla ya kuanza mchakato wa kununua sofa.
Chukulia utaalam huu kama ni maswali ambayo unatakiwa kujiuliza wewe unayehitaji sofa mpya.

·         Je linatimiza lengo unalokusudia?
Mara zote fikiria ni kwa jinsi gani sofa litafanya kazi ndani ya sebule yako. Unatakiwa ukilikalia ujisikie burudani na
pia ujue linatosha kukalia watu wangapi.  

·         Litatosha unapotaka kuliweka?
Ni rahisi kushawishika na muonekano wa sofa huku ukisahau kama ukubwa na muundo wa fremu yake utaendana na sebule yako. Ni vyema ukafahamu kuwa chumba cha sebule chenye kuta zilizojikunja kinapendeza kikiwekwa sofa la muundo wa hivyo na kile chenye muundo wa kuta zilizonyooka za pembenne nacho kinapendeza kwa sofa la pembenne. Tukizungumzia ukubwa wa chumba unachotaka kuweka sofa, fikiria pia kuwa ingawa ni maalum zaidi kwa sebuleni, inaweza kufika wakati ukahitaji kuweka jipya na kuhamishia hilo la zamani chumbani.

·         Ukilikalia unapata pumziko?
Ni kweli kuwa tumezoea zaidi kuangalia umaridadi, lakini pia pumziko tunalopata tunapokalia sofa husika ni muhimu kulifahamu. Kama jinsi miili ya binadamu isivyo sawa ndivyo na sofa zilivyo. Zipe majaribio ya kuzikalia kabla ya kununua na fikiria ni kwa namna gani fremu na mito inakufanya ujisikie. Kwa mfano kama unahitaji sofa ambayo utaweza kupumzika vizuri huku ukiwa unaburudika na vinywaji na vitafunwa vilivyo kwenye meza ya kahawa, basi hakikisha unanunua ambalo halinesinesi kiasi cha kukuzamisha chini ukiwa umelikalia yani kubonyea zaidi.

·         Utawezaje kupata ya gharama nafuu?
Usiridhike na kupita kwa wauzaji wachache na kufanya maamuzi ya kununua! Kuna wajasiriamali wengi wazuri na wabunifu wanaotengeneza sofa za viwango ambapo unachagua muundo, unatoa oda unatengenezewa. Kwahivyo unajikuta umepata sofa lenye ubora kwa gharama nafuu. Fanya utafiti uende kama mnunuzi mwenye uelewa.

·         Je lina ubora?

Unapotaka kununua sofa fikiria vitu vitatu ambavyo ni malighafi iliyotengenezea fremu, malighafi iliyojazwa ndani na ile ya juu iliyolifunika. Unatakiwa ununue sofa ambalo fremu yake ni ya mbao ngumu (au chuma) na sio playwood. Pia hakikisha kuwa malighafi iliyojazwa ndani ya mito sio ya kusinyaa baada ya muda na kuicha ikiwa flati kama chapati. Kwa upande wa malighafi iliyofunika sofa jiulize kama unataka ngozi, kitambaa au mchanganyiko wa ngozi na plastiki. Hii inategemea na gharama unayoweza kumudu na pia tamanio binafsi. Zingatia kuwa sofa zenye rangi nyepesi zinaonyesha uchafu kwa haraka wakati zile za rangi nzito hazionyeshi uchafu/doa kirahisi.

No comments:

Post a Comment