Thursday, August 16, 2012

My Article for Newspaper: Mkanda unavyomtoa mwanamke bomba


Mwanamke anavyovutia akivaa mkanda kuendana na umbile lake
 
Mikanda sio rafiki wa kila mtu. Mkanda unaweza kuwa kitupio cha mitindo chenye changamoto kuvaa hasa kama huna umbile kama la wanamitindo. Kiukweli mkanda unaweza kuwa kinyume chako kwa kuonyesha yale maeneo ya mwili ambayo ungependa kuficha kama utachagua saizi, aina au kuvaa mahali pasipo sahihi.

Mikanda ya wanawake ipo iliyotengenezwa kwa ngozi, vitambaa, vito na kadhalika. Ipo ya rangi moja au yenye malighafi nyingine kama nyuzi, vito, mawe, bakoli na nyingine nyingi. Mikanda iliyozoeleka sana ni ya ngozi na vitambaa, chagua mkanda ambao sio tu unaendana na vazi lako, bali pia unaonyesha vyema umbo lako la kike. Kwa mfano mkanda mpana unapendeza kwa mwanamke mwenye umbo namba nane  kwa kutenganisha vyema kiuno hivyo kuleta mvuto kiunoni. Mkanda huo ukivaliwa sehemu nyembamba kuliko yote ya kiwiliwili – sehemu ya asili ya kiuno ambapo ni pale penye kitovu unasisitiza umbo halisi la kike na pia unamfanya mvaaji kuonekana slimu.

Kiasili mikanda ya wanawake ilivaliwa kwenye nyonga tuu ila karne hii inavaliwa popote kwenye kiwiliwili chake. Ipo inayovaliwa chini tu ya matiti, ipo inayovaliwa sehemu ya asili ya kiuno na ipo inayovaliwa chini ya kiuno karibia kabisa na makalio.

Inalipa kujaribu mikanda mbalimabali sehemu mbalimbali za kiwiliwili kuona matokeo tofauti tofauti. Pia zingatia aina na ukubwa wa bakoli kwa kuwa zinaweza kukuonyesha kiwiliwili kipana au chembamba. Usijali, kwa majaribio kadhaa utapata picha ya mkanda wa kukutoa bomba.

Kama baada ya kujifungua umebaki na tumbo kubwa wala usione aibu kuvaa mkanda. Mkanda uliovaliwa vyema kiunoni utanyonga tumbo na kukupa umbo namba nane. Mkanda mpana  wenye rangi zilizokolea unaovaliwa kwenye eneo asili la kiuno ( yaani pale kwenye kitovu) unakufanya uonekane tumbo slimu.  Usinyonge sana ili nyama zisigawanyike labda tu kama umevaa blauzi pana ambayo haitaonyesha mikunjo ya nyama.

Ukiwa umefungwa vyema mkanda wa kuzunguka nyonga ndio njia iliyozoeleka zaidi ya kuvaa mkanda na ambayo haipitwi na wakati. Vaa mkanda mwembamba au mpana nyongani na suruali au sketi ya mtindo wa katibu muhtasi au gauni la shifti au juu ya blauzi yenye vifungo. Ukivaa mkanda wa kwenye nyonga jitahidi kupunguza vitupio vingine na pia usivae na hereni au bangili za plastiki kwa ajili unawezekana kuonekana kama wa mwaka 47..

Jitahidi kuoanisha rangi kwa mfano, kama unavaa suruali pensi nyeupe na shati jeusi unaweza ukafikiria mkanda mweupe vile vile.

Kama mkanda utavaliwa karibia na makalio badala ya kwenye nyonga itasaidia kuondoa macho ya mtazamaji kwenye tumbo na kuelekezea kwenye mkanda. Pia kama una tumbo kubwa njia nyingine ni kuvaa mkanda chini tu ya matiti kuliko kiunoni kabisa. Mikanda inayovaliwa eneo hili la kiwiliwili inatakiwa kuwa myembamba na bila madoido. Vaa mkanda chini ya matiti pale tu nguo yako ikiwa ina vile vishikizo vya mkanda kwa ajili kama tujuavyo bila hivi vishikizo mkanda utang’ang’ania kushuka chini. Ila jua kuwa uvaaji huu wa mkanda utakufanya uonekane na kifua kikubwa.

Kama  una kiwiliwili kifupi unatakiwa kuvaa mkanda kwa jinsi ambayo kitaonekana ni kirefu. Chagua mkanda wa rangi ya jamii moja na nguo uliyovaa kwa ajili mkanda ukiwa na rangi tofauti kabisa na vazi utaleta mgawanyiko hivyo kufanya kiwiliwili kizidi kuonekana kifupi kwa kuonekana kimekatika nusu mbili. Kuvaa mkanda wa jamii moja na vazi ni njia pia ya kuonekana slimu hasa maeneo ya tumboni.
Kama una bahati ya kuwa na kiwiliwili cha umbo namba nane au umbo la tofali mkanda mpana ukivaliwa nyongani utakutoa bomba. Mkanda wa kiunoni utakufaa zaidi wewe mwenye umbile hili kulikoni ule wa chini ya matiti au wa kwenye makalio.

Miili midogo inapendeza na mikanda myembamba wakati wale wenye miili kikubwa wang’ang’anie mikanda mipana. Mikanda myembamba sana kwa miili mikubwa inaweza kuongeza ukubwa wa mwili wa mvaaji kimuonekano wakati ile minene na mipana kiasi italeta uwiano wa muonekano.

Uwe uwavyo mkanda kwa mwanamke ni sawa na polishi kwenye mbao huongeza mvuto kwa kila vazi. Kila leo mikanda inavaliwa kiubunifu zaidi kiasi kwamba unaweza kuazima mmojawapo hata kwenye kabati la nguo la patna wako.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

No comments:

Post a Comment