Thursday, August 9, 2012

My Article for Newspaper: Kabati la sebuleni


Boresha sebule yako kwa kuweka kabati
Kabati la sebuleni mara nyingi ni ndefu linaloanzia sakafuni; ni mara chache kuona limening’inia ukutani isipokuwa kama ni vishelfu vidogo vya kusimamishia mapambo na maua. Kabati la sebuleni linaweza kutumika kuwekea luninga au mapambo pamoja na picha za familia.
Kabla hujaamua kuweka kabati sebuleni kwako kwanza tafakari matumizi yake na ukubwa wa sebule. Kwa mfano kama kabati ni la kuwekea luninga hakikisha kabla ya kuwa luninga husika itatosha. Pia amua kama unataka kabati mbili ndogo za kufanana au moja kubwa. Tafakari aina ya mbao ungependa kabati lako litengenezewe; mninga na mkongo kwa mfano ni mbao imara na zinazopendwa zaidi na zina urembo wa asili kwa ajili ya fenicha za sebuleni. Makabati ya sebuleni ya viwango ni ya mbao ngumu na ni ya gharama lakini utakapoamua kubadilisha kwa kuliuza gharama yake huwa haishulki sana na ni kitu cha kudumu miaka nenda rudi.

Unapoweka kabati acha nafasi ya kutosha watu kupishana sebuleni, kutoka nje, kwenda chumba kingine ama kwenda kwenye ujia.
Hakikisha kabati lako limemaliziwa vyema pande zote hasa nyuma ili usiliweke ligusane na ukuta. Kwa ajili nyuma kutakuwa kumetengenezwa vizuri kama pande zingine huna haja ya kuficha upande wa nyuma na ukuta kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakifanya ambapo ni makosa ya upangaji wa fenicha sebuleni kugusisha fenicha na ukuta.

Makabati ya sebuleni yanakuja kwa aina na maumbo mbalimbali ambapo inaweza kumfanya mtumiaji achaganyikiwe matumizi. Makala hii itakujuza aina ya makabati unayoweza kuweka chumba hiki ambacho kinatembelewa zaidi nyumbani kwako.

Uwe na sebule ndogo ama kubwa kuna aina mbalimbali za mkabati haya ambayo utapata ya kukidhi hitaji lako:

Makabati ya kuweka mapambo
Makabati haya ni kwa ajili ya kuweka mapambo unayopendelea yawe sebuleni kwako.  Makabati ya kuweka mapambo yanakuwa wazi mbele au yanakuwa yamewekwa kioo kwa hivyo vilivyomo ndani vinaonekana. Huwa ni madogo na yanasimama yenyewe toka chini au madogo sana kama vishelfu vilivyotengenezewa ukutani au kuninginia toka juu na ukawa umeweka mapambo yako ndani. Kwa kawaida huwa yametengenezewa taa kwa ndani ambayo huwashwa ili kuonyesha uzuri wa mapambo yaliyomo kabatini.

Makabati ya kuhifadhia
Kama una upungufu wa sehemu kwa ajili ya kuwa na sebule ndogo, tumia makabati ya kuhifadhia kama suluhisho. Mengi ya makabati ya kisasa ya sebuleni ya aina hii yana sehemu mbili yaani ya kuweka mapambo na madroo ya kuhifadhia. Unaweza kuonyesha mapambo yako na wakati huohuo ukahifadhi vitu kama majarida, CD za muziki na vitu vingine vidogodogo.

Makabati ya kuweka luninga
Hii ni fenicha ambayo kwenye sebule nyingi haiepukiki, asante kwa umaarufu wa luninga kama chombo muhimu zaidi cha burudani na habari! Pia yapo makabati ya kuweka luninga yanayotumika kuwekea mapambo na pia kwa kuhifadhia.  Weka ambalo litakidhi mahitaji yako.

Makabati ya Vitabu
Haya yanasaidia sana kuwekea vitabu, majarida na hata magazeti. Mapambo kama fremu za picha na vesi za maua juu ya makabati haya yanaongeza uzuri wa sebule. Makabati ya vitabu yamegawanywa kwa mashelfu madogo kwa ajili ya kuhifadhia vitabu vidogo na mashelfu makubwa kwa ajili ya vitabu vikubwa. Katikati ya mgawanyo huu kuna nafasi ambayo unaweza kuweka mapambo yako madogomadogo vilevile.

Makabati ya kituo cha burudani
Makabati haya uzuri wake ni kuwa yametengenezwa kwa jinsi ambayo kuna sehemu za kupitishia waya  na miungo ya vifaa vyako vya burudani vya elektroniki na kuficha nyaya hizi kwa ndani ili kufanya kituo kionekne nadhifu. Mara nyingi makabati haya yanakuja kama vipande vipande na mtumiaji anaunganisha mwenyewe hadi kabati zima linatokea.  Baadhi yake yamegawanywa viboksi vya saizi ya kuweka DVD na michezo ya elektroniki, eneo la luninga, spika za miziki na eneo la ziada kuhifadhia vifaa vingine.

Sebule zinatumika tofauti kwa kila familia. Kwenye nyumba nyingine sebule inatumika kama eneo maalum la familia nzima kukutana, wakati kwa wengine sebule imekaa zaidi kama chumba cha maonyesho, kinachotumika tuu pale mgeni anapotembelea nyumbani. Kwa matumizi yoyote yale, nyumba zenye sebule zenye kabati ni nadhifu zaidi.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

2 comments:

  1. makala nzuri nimeipenda. lakini vipi kuhusu kabati ya tv ina umuhimu kama umeitundika tv ukutani?

    ReplyDelete
  2. Hi Matola, asante kwa kutembelea blog yangu. Inategemea na jinsi kabati lilivyokaa kama litaweza kutumika kwa matumizi mengine kama kuhifadhia etc. kama ulivyoona kabati la sebuleni lina matumizi mengi.

    ReplyDelete