Wednesday, August 22, 2012

My Article for Newspaper: Suti Sahihi ya Mwanaume



Suti sahihi ya mwanaume

Suti inahuisha muonekano wa mwanaume yeyote.  Kwa ujumla watu wanamchukulia kivingine mwanaume aliyevaa suti sahihi. Bahati nzuri ni kuwa kuna ushahidi wa kisayansi ya kuwa jinsi unavyovaa inaleta hisia tofauti tofauti kwenye dunia inayokuzunguka.
Maarufu sana kati ya suti za kiume ni suti ya taksedo, ni suti ambayo pia inajulikana kuwa rasmi zaidi.

Suti za kiume zipo za makoti yenye vifungo vilivyojipanga mstari mmoja  na za makoti yenye vifungo vilivyojipanga mistari miwili. Hizi za vifungo vilivyojipanga mstari mmoja ni za kisasa zaidi na hazipitwi na wakati. Suti zenye mistari miwili ya vifungo zinawafaa wanaume warefu na wembamba  kwa kuwa hii mistari miwili ya vifungo inaleta muonekano wa upana kuliko zile za mstari mmoja. Kama mazingira ya kazi yako yanakuhitaji kuvaa suti kila siku suti za mistari miwili ya vifungo hazikufai.
Zaidi pia suti za kiume zinakuja kwa staili mbalimbali – kifungo kimoja, viwili na vitatu. 

Kuna kanuni za wewe mwanaume kufuata kabla hujaamua kununua suti yako mpya.

Kwanza, kitambaa na rangi vinachukua sehemu kubwa kwenye uchaguzi wa suti yako. Vitambaa vya pamba, linen na polista ni vizuri kwa suti. Kwa kuendana na wakati chagua suti ya rangi nyingine badala tu ya nyeusi iliyozoeleka.

ukijaribu suruali ya suti unayotaka kununua na ukiweza kuchomeka kiunoni vidole viwili bila kubana inakuhakikishia kuwa suruali hiyo ni sahihi kwako. Hii ni suruali utakayoweza kuvaa kama ukiongezeka uzito kidogo na pia ukiwa umeshiba. Kama una nyama za ziada tumboni suruali yenye vipindo kiunoni itakuwa nzuri zaidi kwako kuficha nyama ila kama ni mwembamba usivae yenye vipindo kwani itakufanya uwe mwembamba zaidi. Suruali iwe na urefu sahihi ukiwa umeivaa ifunike soksi. Ile mikunjo ya chini kabisa ya suruali ni mizuri kwa kusaidia kuleta uwiano wa uzito kufanya suruali itulie mwilini. Suruali isiyokuwa na mikunjo chini inamfanya mvaaji aonekane mrefu. Hata hivyo vijana wa kisasa wawe wafupi ama warefu wameonekana kupendelea zaidi suruali zisizokuwa na mikunjo ya chini. Mikunjo ya chini ya suruali ninayozungumzia hapa ni ile ya kukunjiwa kwa nje.

Chagua koti lenye mikono ya urefu sahihi kwako. Mikono mirefu sana au mifupi sana inafanya watu wafikirie hiyo suti labda umeazima. Mikono mirefu sana ya koti la suti ni ile iliyofunika kabisa shati; kwa maana hiyo hii haitakiwi. Mikono ya koti la suti yenye urefu sahihi ni ile ambayo shati uliloovaa ndani limetokeza nje kati ya nusu hadi inchi moja. Kwa maana hiyo mikono ya shati itokeze kidogo nje ya mikono ya koti la suti. 
Jisikilizie kama uko huru kutembea ukirusha mikono ukiwa umevaa suti yako. Isiwe taabu kunyoosha au kukunja mikono, kuhakikisha hili nyoosha mikono yako kwenda mbele. Urefu wa koti la suti uwe sahihi, ukiwa umesimama na kunyoosha mikono koti lifikie walau kati ya kiganja na kwenye ncha ya kidole chako cha kati.

Kwa swala zima la muonekano  wa suti sahihi ya mwanaume soksi zioane na suruali, mkanda uoane na viatu kwa rangi na tai iwe na urefu wa kugusa bakoli ya mkanda. Viatu au buti za kuvaa na suti ziwe nyembamba mbele na visiwe na kisigino kirefu. Kuvaa suti na viatu vya aina hii inaleta muonekano mzuri zaidi kuliko viatu vya duara mbele na visigino virefu. Kalamu zisiwekwe kwenye mfuko wa shati, ziwekwe kweye mfuko wa ndani wa koti la suti. Vilevile simu zinazovaliwa kwenye mkanda nazo si sahihi, pengine fikiria kubeba briefcase!

Zingatia kanuni kuu ya msingi ya vifungo vya koti la suti kuwa kwa koti la staili ya vifungo vilivyojipanga mstari mmoja unaweza ukawa umefunga vifungo vyote lakini kamwe usifunge kifungo cha chini. Kifungo cha chini cha koti la suti iwe ni staili ya vifungo viwili, vitatu ama vinne (kwa suti chache) kamwe hakikuwekwa ili kifungwe. Mara zote vifungo vyote vya staili ya koti la suti la vifungo vya mistari miwili vifungwe.

Suti ni vazi linaloonyesha mamlaka na utanashati kwa hiyo walau kila mwanaume anatakiwa kuwa na suti moja “inayomtoa” kwenye kabati lake la nguo hata kama havai suti mara kwa mara.  

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

1 comment: