Una
ardhi ndogo lakini unahitaji bustani? Fikiria vyungu vya kuning’iniza.
Vyungu vya maua vya
kuninginiza ni njia inayopendwa ya kupendezesha makazi yako kwa kuotesha humo
mimea utakayoipenda na kuvitundika kwenye maeneo ya ukuta utakayochagua iwe ni
ndani au nje ya nyumba. Vyungu vya maua vya kuning’iniza vinasaidia kuongeza
rangi kwenye ukuta wa nyumba yako, veranda na bustani. Vyungu hivi vinaweza
kutumika kwa ufanisi hasa kwa nyumba yenye eneo dogo la nje na vinaweza kuwekwa
kama mapambo kwenye eneo ambalo linahitajika kupambwa. Kama ukichagua maua
vizuri bustani zako hizi za hewani zinaweza kudumu kwa miaka kadhaa kwa wewe
kuvipaka vyungu rangi tofauti tofauti kuendana na msimu.
Sokoni kuna aina
mbalimbali ya vyungu vya maua vya kuning’iniza. Fikiria ni vyungu vya namna
gani vitaendana na mapambo yako ya ndani
kama unataka kuvining’iniza ndani ya nyumba na pia mandhari ipi itaendana vyema
na bustani yako na maua unayotaka kuotesha humo. Vyungu vya maua vilivyotundikwa
ndani kwenye maeneo ya kona ya ukuta vinafanya eneo la sakafu liwe huru na
vinapendezesha ukuta wa kona, ule wa sehemu wa kuingilia na hata ule wa
sebuleni. Sanaa za kuning’iniza sebuleni kwako zinawasalimia wageni,
zinaelekeza njia na pia zinapambana kwa uzuri na rangi za ukuta Kama hutaki
kuweka vyungu vya maua vya kuning’iniza ndani ya nyumba basi weka kwenye ukuta
wa nje wa nyumba kwa maeneo ya dirishani kwa mfano vinafaa sana kwa kuleta
faragha na maua yake yanavutia kuangalia ukiwa ndani.
Vyungu vya maua kwa
ajili ya kuning’iniza vinatakiwa vile vyepesi. Hakikisha kuwa vyungu vyako vina
matobo kwani udongo unaosimamisha maji muda wote unafanya mizizi ya mimea ioze
kwa hivyo mimea kufa. Vyungu vya plastiki ni vyepesi ila tahadhari ni kuwa vinapasuka
kirahisi ikiwa eneo vilivyotundikwa vinachomwa na jua kali. Vile vile vyungu
vya maua vya kuning’iniza vinahitaji kuwekwa kwa vyuma imara kwani huwa
vinakuwa vizito hasa wakati wa kumwagilia. Epuka kusababisha ajali kwenye
familia yako pale chungu cha kuning’iniza kitakapomdondokea mwanafamilia.
Vyuma vilivyochimbiwa
ukutani kwa ajili ya kushikilia vyungu vya kuninginiza vinatakiwa kuwa imara.
Chungu chenye udongo na mimea kinaweza kuwa na uzito wa hadi kilo kumi na hiyo
ni hata kabla ya kumwagilia. Halafu pia kumbuka kama chungu kimening’inizwa
sehemu ambazo hazina paa ni kwamba maji ya mvua yatakuwa yanaingia moja kwa moja
hivyo kukifanya kuwa kizito zaidi.
Kabla ya kutundika
chungu chako cha maua cha kuning’iniza zingatia pia mahali unapokiweka. Je hali
ya hewa ya mahali hapo kwa mfano jua la kuchoma mmea moja kwa moja halitauathiri?
Ni upande upi upepo unakoelekea. Hali ya hewa ya joto kali na upepo utauvunja
vunja mmea. Upepo mkali unaweza kuukausha mmea na pia kuvunja matawi madogo
madogo. Halafu pia kama mmea unaootesha hautaki maji mengi mvua inaweza
kuuozesha. Na kitu kingine zaidi cha kuzingatia ni kama katika eneo husika kuna
kitu kinachoakisi joto kwa mfano lango la chuma linalopigwa na jua au pia kuna
rangi za ukuta za namna hiyo hata kama mmea unastawi kwenye jua kali basi hali
hii ya joto kuzalishwa maeneo ya karibu na chungu litauua mmea.
Kwa vyoyote vile, inatakiwa
iwe rahisi kwako kumwagilia na kutunza bustani yako ya hewani kwa hivyo hakikisha
mahali ulipochagua kuning’iniza chungu chako panafikika. Kwa mfano hutataka kuwa
unakanyaga maua mengine ya bustani ya ardhini ili kukifikia chungu, na kama
kimening’inizwa juu sana utahitaji jinsi ya kukifikia. Na zaidi ya urahisi wa
wewe kukifikia chungu, angalia eneo ulilokining’iniza isiwe inabughudhi
watembeaji wengine au inaziba muonekano.
Kama nilivyosema mwanzo
kuwa chungu inabidi kiwe na matobo kumbuka kuwa kitadondosha maji baada ya
kumwagiliwa, kwa hivyo kunahitajika kuwe na kisahani kinachoambatana na chungu
au unakiteremsha chungu chini ukimwagilie halafu ukiruhusu kukauka ndipo
ukirudishe juu. Lakini njia rahisi ni hii ya kuwa na chungu chenye kisahani cha
kudondoshea maji kwani maji hayo hayo yanahitajika wakati maji kwenye chungu yanapokauka.
Vyungu vya maua vya kuning’iniza na visahani vya kudondoshea maji ambavyo ni
vya bei rahisi vinapatikana walau kwenye kila kituo cha bustani.
Sasa basi unafikia
wakati wa kuotesha mimea kwenye chungu chako. Kuna mimea lukuki ya kuweza
kuotesha kwenye vyungu vya kuning’iniza. Unaweza kuotesha mmea mmoja mmoja au
mchanganyiko, iwe ni ya kusimama, kuning’inia ama yote kwa pamoja. Jua mimea
inayostawi kwenye vyungu. Weka kwenye kundi moja mimea itakayovumilia mahitaji
sawa ya maji, mwanga na joto. Maua mbali mabali inaweza kuwekwa kwenye vyungu vya kuning’inia, ubunifu
wako ndio kizuizi pekee. Inafurahisha kuona mmea ukikua kukubaliana na jinsi
unavyouongoza. Katikati ya chungu weka mimea inayotoa maua kupata muonekano wa
uhakika!
Ulishasikia hadithi ya bustani za kuning’inia za
Babiloni? Bustani sio za ardhini tu, kama huna ardhi ya kutosha lakini unapenda
bustani weka basi hizi za vyungu vya kuning’iniza uongeze uzuri angani!.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment