Malizia muonekano wa jiko lako kwa kuweka kizulia
Jikoni ni sehemu inayopitwa zaidi. Kwa familia
zinazopenda mapambo ni kawaida kukuta kizulia kwenye maeneo ya mbele ya stovu
na sinki au maeneo mengine ambapo mtu anasimama kwa muda mrefu jikoni. Vizulia hivi sio tu vinasaidia kuhifadhi
sakafu ya maeneo haya isisharibike zaidi ya yale mengine ambayo hayakanyagwi
sana bali pia vinasaidia kuburudisha miguu. Na pia unaweza kuweka kizulia
jikoni kwa lengo la kupamba. Vyovyote iwavyo, uchaguzi wa kizulia cha jikoni ni
tofauti na vile vizulia vingine vya ndani. Unatakiwa kuzingatia uimara,
umachachari wa kuzuia madoa na vifaa vilivyotengenezea kizulia husika. Makala
hii itakuambia jinsi ya kuchagua na utunzaji wa kizulia cha jikoni kwa lengo la
kumalizia muonekano wa jiko lako.
Miaka nenda rudi jikoni kwako pamekuwa ni mahali pa
kufanyia kazi ya kuandaa chakula. Badili jiko lako liwe ni sehemu ambayo
inavutia zaidi kwa mguso wa rangi za kizulia cha jikoni. Jikoni panapovutia
panakuwa ni mahali unapotamani kwenda na si mahali ambapo inakulazimu kwenda.
Unakapoweka jiko lako katika mandhari ya kuvutia utashangaa wageni wako
wanaoingia kwa kupitia mlango wa nyuma wanakosea njia kwa kuelekea jikoni
badala ya kuelekea sebuleni!
Kitu kizuri kuhusu vizulia vya jikoni ni kwamba viko
tofauti na ukawaida wa muonekano wa jiko. Watu wengi wanang’ang’ania marumaru
nyeupe au za rangi ya krimu jikoni na hii ni sifa ya rangi za jiko toka enzi na
enzi. Kwa kuweka kizulia cha rangi tofauti utahuisha muonekano wa jiko lako.
Chagua eneo unalotaka kuweka kizulia , ambalo mara
nyingi ni lile linalokanyagwa zaidi au linalokanyagwa kwa muda mrefu kwa mfano
chini ya meza, eneo la kuingilia, mbele ya stovu au chini ya sinki au jokofu.
Baada ya hapo pima ukubwa wa eneo hilo unalotaka kufunika kwa kizulia. Hii
itakusaidia kutupilia mbali kizulia kikubwa sana au kidogo sana wakati wa
manunuzi.
Chagua umbo la kizulia kwa kipimo na aina ya
fenicha. Kwa mfano, kama unataka kizulia kiwe chini ya meza ya duara basi
chagua kizulia cha duara. Amua kama kizulia hiki ni cha mapambo, je ungegependa
kiwe cha rangi moja? Unaweza kuchagua rangi ambayo inaoana na ya kabati zako za
jikoni au kaunta, au unataka kigeuze shingo kwa kuwa na michoro ya rangi zilizokolea.
Kizulia chenye rangi ya kukolea kitaonyesha madoa
machache na uchafu kidogo. Zingatia pia urahisi wa kukisafisha kwani kizulia
cha jikoni kiko kwenye hatari ya kupata madoa zaidi ya kizulia kwenye chumba
kingine chochote. Chagua kizulia ambacho
hakitelezi kwa maana ya ukikikanyaga kisihame kutoka eneo moja kwenda jingine
iwe ni kwenye sakafu ya mbao au marumaru kwani ni hatari kwa mtumiaji kwani
kinaweza kumwangusha.
Doa kwenye kizulia cha jikoni linaweza kuwa chochote
kutoka kwa mtoto, kikombe kilichoanguka toka juu hadi nyayo zenye tope. Kushughulikia
madoa ya kizulia cha jikoni barabara ndio kunakotofautisha mabingwa wa usafi na
watu wengine. Unaweza kujiita mtaalam kama utaweza kupambana na madoa ya
kizulia chako cha jikoni. Ila kiukweli huhitaji nguvu nyingi kushughulikia
madoa hayo.
Kwanza unatakiwa kuwa tu na hisia za kawaida.
Kuchukua hatua mapema kuondoa doa lolote mara linapotokea kwenye kizulia cha
jikoni kwa wakati huo huo. Doa
liliosahaulika litaumiza kichwa baadaye. Na doa la aina hii linaweza kuharibu
kabisa muonekano wa kizulia chako. Kama ukiliacha doa bila kulishughulikia
mapema linazama hadi mwanzo wa nyuzi za kizulia na hii itahitaji nguvu kubwa
kulishughulikia. Kwahivyo kila wakati kuwa na hisia. Tenda mapema na kwa
ufanisi.
Kuna madawa mengi yaliyoaminiwa kwa ajili ya kuondoa
madoa ya kwenye zulia. Tembelea maduka yanayohusiana na mambo hayo uwe na dawa
yako nyumbani wakati wote.
Kumbuka, jiko lako halitakiwi kuwa ni mahali pa kuandalia
chakula tu. Unaweza kubadili jiko lako kuwa kivutio ndani ya nyumba yako
kirahisi tu kwa kuleta mguso wa rangi na furaha japo kwa kuweka kizulia cha
jikoni.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment