Vitu vya kuzingatia wakati wa kununua kitambaa cha
meza
Kutandika kitambaa mezani kunatengeneza mandhari
tulivu na kunaivalisha meza wakati wa chakula au tukio maalum. Kitambaa cha
meza chaweza kuwa ni kwa ajili ya mapambo au kuilinda meza isidondokewe vyakula
wakati wa kula. Kitambaa cha meza chaweza kuwa ni kwa matumizi ya meza ya ndani
au nje. Sio gharama kubwa kununua au kushonesha kitambaa cha meza na huwa
vitambaa hivi vinapatikana kwa rangi na michoro mingi.
Kitambaa cha meza chaweza kuwa cha nguo au jamii ya
mpira. Kwa kawaida vitambaa vya meza vya
nguo ni rasmi kuliko vile vya mipira. Vitambaa vingi vya meza vya nguo
vimetengenezwa kusafishika kirahisi, isipokuwa lesi, ambayo huenda ikahitajika
kulowekwa na kufuliwa kwa mikono kwa uratatibu. Wakati wa kuchagua kitambaa cha
meza cha nguo, chagua kile ambacho kinaendana na staili ya chumba chako cha
chakula. Meza rasmi ya chakula inahitaji kitambaa rasmi cha meza.
Kwa umaridadi zaidi unaweza kutandika kitambaa cha
lesi juu ya kitambaa cha meza cha nguo. Na pia unaweza kununua vitambaa vya
meza viwili vya staili tofauti sahihi kwa muonekano rasmi au wa kawaida wakati
wa kujumuika mezani kwa chakula.
Kama unachagua kitambaa cha meza kwa ajili ya meza
ya nje, fikiria kununua cha mpira kwa ajili kitambaa cha nguo kinapauka
kirahisi na jua na pia ni ngumu kukisafisha. Kitambaa cha meza cha mpira
kinaweza kufutwa tu na kikatumika bila ya kukitoa mezani na kukifua. Vitambaa
vya meza vya mipira huwa ni vya bei nafuu zaidi ila havidumu sana lakini vinastahimili
zaidi mazingira ya nje.
Wakati wa kuchagua kitambaa cha meza inakupasa
kutizama vitu kama rangi, ukubwa wa kitambaa, michoro na vifaa
vilivyotengenezea kitambaa. Oanisha kitambaa unachotaka kununua na vitupio
vingine hapo mezani kama vile mati, utambaa na napkini.
Matumizi ya kitambaa cha meza kwenye meza ya chumba
cha chakula yanakuongezea nafasi ya ubunifu katika mapambo ya ndani mwako, hasa
kama unataka kubadili muonekano lakini huna bajeti kubwa ya kupamba upya.
Vitambaa vya meza vinakuja kwa kila rangi, na ni mahususi kwa msimu wa sikukuu au mapangilio wa meza
kwa mandhari fulani. Kuwa mbunifu kwa kuweka vyakula na mapambo yako ya meza
kirahisi ili yasichoshe walaji walioko mezani.
Chagua kitambaa cha meza kilichotengenezwa kwa nyuzi
za asili kwa kuwa huwa vitambaa vya aina hiyo vinakuwa laini na burudani zaidi
kimuonekano. Kwa mfano vitambaa vilivyotengenezwa kwa pamba vinadumu kwa miaka
mingi. Vitambaa vya meza vilivyotngenezwa kwa pamba na linen vimeonekana ni
sahihi kwa matumizi ya mezani na vinadumu kwa muda mrefu.
Ukubwa wa kitambaa unahusu hasa pale unapotaka ni
kwa kiasi gani kitambaa kining’inie kwa maana ya baada ya kitambaa kujaa mezani
kile kinachodondokea chini kuelekea sakafuni. Kwa mpangilia wa kawaida wa meza
kitambaa kinachoking’inia chaweza kuwa kifupi, kutegemea na maamuzi yako. Kama
unapenda kuchagua mpangilio maridadi, kitambaa cha meza kinatakiwa kikaribie
kabisa kugusa sakafu, na hii pia huleta muonekano rasmi zaidi. Kujua urefu wa
kitambaa cha meza unahitajika kupima meza. Kwa meza zilizozoeleka za pembe nne,
pima urefu wa meza ongezea na urefu wa mguu wa meza mara mbili ( Kumbuka
kitambaa kinaanguka sawa panda zote za meza). Kama una meza ya yai ama duara,
ni rahisi, nunua kitambaa cha yai ama duara na kumbuka kutumia mbinu ile ile ya
kipimo ili kujua ukubwa wa kitambaa utakaoning’inia. Na pia kumbuka kuwa kuna
vitambaa vingine ambavyo vimefungwa kwenye pakiti ambapo nje ya pakiti kuna
vipimo vimeandikwa.
Kama una muonekano fulani kichwani na hujapata
kitambaa sahihi, fikiria kushonesha kwa fundi. Vitambaa vya meza za pembe nne
ni rahizi sana kushonesha na mara nyingi ndio meza ngumu kuweza kupata kitambaa
cha ukubwa sahihi kilichotengenezwa tayari tayari. Kama utaamua kushonesha
kitambaa kwa fundi hakikisha unakuwa na uhakika wa mambo kama kuchujiana rangi
na pia kuna vitambaa vingine vinasinyaa na kupungua ukubwa vikifuliwa.
Kama wewe ni mtu unapenda sana mapambo fikiria pia
marinda ya kona. Kitambaa cha meza kikifanya marinda maeneo ya kona kinaongeza
umaridadi kwenye muonekano wa mapambo yako ya ndani.
Kwa kuwekeza kidogo, unaweza kununua au kushonesha
vitambaa vya meza kwa ajili ya matukio yote na kuleta muonekano wa ukaribisho
kwa meza iliyovalishwa maridadi. Unaweza kujikuta unafurahia muonekano huo na
hivyo kufurahia msosi wako.
Usidanganyike kuwa kwa kusema tu ni meza ya yai ya
watu 6 basi utapata kitambaa sahihi. Inaudhi umenunua kitambaa chako cha meza
na mara unapokifikisha nyumbani hakitoshi mezani. Hakikisha
unakuwa na vipimo sahihi vya meza yako kwa ajili ya kitambaa unachohitaji.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa
ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023
No comments:
Post a Comment