Ongeza unadhifu wa chumba kwa kutumia tai za pazia
Tai za pazia ni kwa ajili ya matumizi na mapambo. Kutokana
na mitindo lukuki iliyopo ya tai hizi, unaweza kupata seti ya tai ambayo
itaendana na mapambo yako mengine ya ndani. Nia kuu ni kushikilia pazia mbali
na dirisha hivyo kudhibiti kiasi cha mwanga unaotaka kuruhusu uingie ndani kwa
kuwa na uwezo wa kufungua pazia zikashikiliwa kwa tai na wakati huo huo
ukaongeza umaridadi wa muonekano.
Tai za pazia ni njia rahisi ya kufanya pazia za kitambaa kuonekana nadhifu na maridadi, au kwa kudumu ama wakati wa mchana. Baadhi ya watu wanapendelea kuacha pazia wazi wakati wa mchana na kuzifunga usiku. Hii inasaidia kuongeza mwanga wa asili chumbani na kuleta hisia za usalama zaidi usiku. Kwa kufungua pazia zionekane maridadi, tai za pazia ni suluhisho. Kwa kawaida tai hizi zinashikiliwa na vishikizo ama kulabu zinazochimbiwa ukutani karibia na dirisha. Vishikizo hivi vyaweza kuwa vya mbao au chuma na vinawekwa kutegemea na staili na uzito wa pazia zikihudumia kuendana na mapambo ya chumba.
Tai za pazia zinatengenezwa kwa unene tofauti kutokana na uzito na staili ya
pazia. Tai nzito zinafaa kwa kushikilia pazia nzito lakini pia zinatumika kwa
pazia nyepesi. Tai za pazia zenye kifundo ni maarufu na za kimapambo zaidi na
zinatumika kwa pazia za vitambaa vinene na vizito. Kwa sababu tai hizi huwa ni
kubwa na nzito hivyo zinaendana moja kwa moja na aina hii ya pazia. Vifundo
kwenye tai hizi huwa vinakuwa ni vya kusukwa kwa nyuzi na wakati mwingine huwa
vifundo hivi vimeongezewa shanga. Kwa hivyo kwa umaridadi unaweza kuchagua
rangi mojawapo kwenye tai itakayooana na pazia na mandhari nyingine za chumba.
Tai za pazia zisizokuwa na maridadi zimetengenezwa kwa kitambaa chepesi na
zinatumika kufungia pazia nyepesi. Rangi zake zinaweza kuendana na zile za
pazia. Tai za pazia sio
lazima ziwe ni kitu cha kipekee, zinaweza hata kutengenezwa kutokana na
kitambaa hichohicho cha pazia. Hii ni njia rahisi ya kutumia kitambaa sahihi
cha pazia na tai zake kuendana na mandhari ya chumba.
Tai za pazia zinatofautiana sana
kwa umbo na ukubwa. Fikiria ni tai gani zinakazokidhi mahitaji yako na
muonekano wa chumba unaotaka kutengeneza. Kwa hivyo wakati wa kunua tai za
pazia hakikisha unajua kuwa unataka za ukubwa gani na ziendane kwa uzito na
pazia utakazotumia; hii itamalizia muonekano wa chumba. Uwe na uhakika pia wa
idadi ya tai unazohitaji, je utataka ziwe kwa seti au moja moja. Ni mara ngapi
tai husika zitatumika. Kwa mfano zitakuwa zimeshikilia pazia muda wote kama mapambo au ni wakati wa mchana tu. Kama
ni za kufungua na kufunga mara kwa mara basi tumia zile tai ambazo hazina
madoido mengi.
Kulabu za kushikilia tai za pazia zinawekwa kwa urefu ambao
hautakuwa shida kufungua pazia. Hakuna urefu maalum wa wapi pa kufunga tai za
pazia. Pia fimbo pazia zilikotundikwa
zinahusika kwani nyingine ni ngumu kuvuta pazia wakati wa kufungua, kwa hivyo
ziwe fimbo ambazo hazina usumbufu ukitaka kufungua na kufunga pazia. Weka fimbo
ambazo pazia litateleza kilaini wakati wa kufunga na kufungua.
Kwa kweli pazia zitakuwa hazijakamilika bila tai maridadi za
pazia. Kitupio hiki kidogo tu kinabadilisha muonekano mzima na mandhari ya
chumba chako.
Iwe nia ni kufungua pazia ili kuruhusu mwanga kiasi kuingia ndani au kuzipa pazia umbo la umaridadi zaidi basi tai za pazia ni muhimu kutimiza malengo haya mawili. Ni muhimu kuisikiliza sauti yako mwenyewe na kutengeneza makazi ambayo yanafaa staili ya maisha unayoishi wewe na ya familia yako. Mitindo inakuja na kuondoka lakini kama utajenga kujiamini na kuwa staili ambayo ni ya kipekee nyumbani kwako hutaangukia kwenye utumwa wa kurukia kila pambo la ndani utakaloona. Kulinganisha na kushindanisha kila pambo madukani kutanyonya nguvu yako ya ndani badala ya kuielekeza kwenye mambo mengine, ukiwa mkweli wa nafsi yako mwisho utapata ladha yako ya kudumu.
Iwe nia ni kufungua pazia ili kuruhusu mwanga kiasi kuingia ndani au kuzipa pazia umbo la umaridadi zaidi basi tai za pazia ni muhimu kutimiza malengo haya mawili. Ni muhimu kuisikiliza sauti yako mwenyewe na kutengeneza makazi ambayo yanafaa staili ya maisha unayoishi wewe na ya familia yako. Mitindo inakuja na kuondoka lakini kama utajenga kujiamini na kuwa staili ambayo ni ya kipekee nyumbani kwako hutaangukia kwenye utumwa wa kurukia kila pambo la ndani utakaloona. Kulinganisha na kushindanisha kila pambo madukani kutanyonya nguvu yako ya ndani badala ya kuielekeza kwenye mambo mengine, ukiwa mkweli wa nafsi yako mwisho utapata ladha yako ya kudumu.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023
No comments:
Post a Comment