Thursday, August 15, 2013

My article for newsapaper: kabati dogo la nguo



Jinsi ya kufaidika na kabati dogo la nguo

Sio wengi wenye uwezo wa kuwa na chumba maalum kwa ajili ya kujiandaa kwa kuvaa na kuwekea nguo na viatu. Badala yake wengi wanakuwa na kabati la nguo kwenye chumba cha kulala kwa hivyo ni lazima watumie nafasi waliyonayo ingawa yaweza kuwa ni ndogo sana. Makala hii itakupa jinsi ya kuweza kuongeza nafasi kwenye kabati lako la nguo na kuondoa mrundikano unaoweza kuwepo kwenye eneo hili muhimu ambalo pengine kukiwa na ajali ya moto ndani ya nyumba ni sehemu ungeweza kujitosa hata kama ni kuungua ili kuokoa viwalo vyako.

Kama ilivyo kwa vifaa vingine vya ndani, makabati ya nguo siku hizi yanakuja na maeneo mengi ya kusaidia kuhifadhi kwa mfano kulabu za kutundikia, shelfu na kadhalika. Iwe ni sehemu ya kuhifadhi nguo au hata zaidi ya hilo, karibia na kabati lako la nguo panatakiwa kuwa na sehemu ya kuvalia ukiwa umesimama na ukiwa umekaa, lazima pawe burudani kwa matumizi. Hapa ni maswali kadhaa yakujiuliza yatakayokusaidia kuboresha kabati dogo la nguo bila kujali ni vifaa gani unahifadhi humo:

•Je unataka sehemu ya kukaa?
Kiti ni kizuri kwa kukaa wakati wa kuvaa soksi na viatu. Unaweza kuweka kiti chini ya dirisha lililo karibu na kabati lako la nguo kwa kuwa huwezi kuitumia nafasi hii kwa kitu kingine chochote.

•Je wakati wa kuvaa unajiona vizuri kwenye kioo?
Jaribu kwenda angalau futi tatu mbali na kioo uone kama unajiona vizuri, na hakikisha kuwa kioo kiko sehemu isiyokuwa na kizuizi, kama vile nyuma ya mlango.

Je una mpango kunyooshea hapo hapo nguo zako zilipo?

Je unataka kuangalia TV wakati unapovaa?
Kama ndio, weka luninga karibia na kabati lako la nguo. Kama luninga haitakaa usawa wa macho basi inageuka radio.

Je unapenda kuangalia nje wakati wa kuvaa?
Kumbuka kuwa kama unaweza kuona nje, wa nje nao wanaweza kukuona! Uamuzi ni wako.

Ikiwa umeshajiuliza maswali hayo yote na kuwa na majibu yake zifuatazo ni suluhisho rahisi za kuweza kuongeza nafasi kwenye kabati dogo la nguo la chumba cha kulala.

Hatua ya kwanza ni kufungua milango ya kabati na kutazama ndani. Usiwe na hofu hamna anayekuona ni wewe tu na kabati lako. Linakuambia nini?
  • Rangi na mwanga. Kwenye kabati lako la nguo hakikisha kuna mwanga wa kutosha kwa ajili ya kuona vizuri kila kitu. Mwanga hafifu utakudanganya baadhi ya rangi. Kabati lako liwe kubwa au dogo kama halijatazamwa kwa miaka, hakikisha unalihuisha kwa kupaka rangi. Rangi nyeupe ni mahususi kwa kuwa inaongeza mwanga.
  • Ondoa mrundikano. Kwa vile tayari umeshakosa nafasi na unahitaji kuongeza, kuondoa mrundikano ni fursa sahihi kwako ya kuamua ni nini cha kuondoa na kuwa na nafasi ya ziada kwenye kabati lako kabla ya kuweka mpangilio. Ni lini mara ya mwisho uliondoa usivyohitaji tena kwenye kabati lako la nguo? Unajua wakati unapofungua kabati lako angalia kifaa na kufikiria: “Mara ya mwisho kuvaa hii sketi ilikuwa….ilikuwa lini?...Aaah, ndio kwenye harusi ya fulani!” Lakini kama harusi ya huyo fulani ilikuwa miaka 15 iliyopita, ni nini hii sketi inachofanya kwenye kabati lako la nguo??? Tafuta muda wa kuondoa mrundikano na uache vile tu unavyovaa na kupenda.
  • Weka mpangilio. Kuwa na mfumo unaoeleweka wa nini kinakaa wapi na jinsi ya kuhifadhi nguo za msimu. Hifadhi nguo za msimu kwenye masanduku na uyaweke juu ya kabati la nguo au kama una kitanda chenye hifadhi mvunguni hifadhi nguo za msimu humo. Chagua heng’a zenye kuweza kutundika vitu vingi kwa wakati mmoja. Weka vitu unavyotumia mara kwa mara usawa wa macho kiasi kwamba ukinyanyua mkono tu unachukua. Vile usivyotumia kila wakati weka mbali na macho.
  • Tumia mlango wa kabati kwa kutundika vitu kama mfuko wa vitupio ama mfuko wa viatu. Kama hujatumia mlango kwa mfuko wa viatu unaweza kutumia sakafu ya kabati kwa kuweka shelfu za viatu.Tumia maeneo kadhaa ya kabati kwa matumizi mbalimbali kwa mfano madroo kwa kuweka nguo za kukunja na tumia ile sehemu ya wazi kutundikia hasa magauni na suti. Pembeni wa kabati la nguo weka kasha la nguo chafu kurahisiha kuhifadhi nguo za kufua.
  • Remba. Ndio, weka urembo. Hii ina maanisha jipende na hivyo kuweka mazingira ya urembo kwenye kabati lako la nguo. Tundika hapo picha ndogo ya kumbukumbu nzuri kwako. Kila ukiwa unavaa unaiona na hivyo kukupa faraja. Uzuri ni silaha kubwa ya nguvu ya kutibu.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023

No comments:

Post a Comment