Baadhi ya siku unaweza kushangaa kama kupika kunalipa kwa nguvu
yote inayotumika. Kweli, unaweza kuweka mlo kabambe mezani, lakini jiko lako
likaishia kuwa chafu mno kwa, mrundikano wa vyombo vichafu. Unaweza ukawaza kuwa
inaenda kuchukua muda mwingi kusafisha kuliko kula!
Kanuni kuu ya jiko kuwa safi wakati ukiendelea kupika, ni kuanza
na jiko safi. Kwa njia hii uchafu unaokuogopesha ni ule unaotengeneza wakati wa
kupika tu. Kwa mazoea wengi wanajitahidi kuacha jiko safi kabla ya kwenda
kitandani kila ifikapo usiku. Vyombo visafi vinawekwa kabatini, vile vichafu
vinaoshwa, viporo vinawekwa kwenye vikontena na kuwekwa ndani ya jokofu, ndoo
ya uchafu inamwagwa na kwa namna hiyo hakuna uchafu unaobaki jikoni.
.
Siri ya kufanya jiko liwe safi wakati unapoendelea kupika ni
kuosha kadri vinavyochafuka. Nadhani hakuna njia nzuri zaidi ya kusisitiza hili.
Kama wali unaendelea kuiva kwa dakika 20, una muda wa kusafisha. Kama kuna muda
wa kusubiria chakula kiive, basi kuna muda wa kusafisha. Inashangaza jinsi
tunavyodharau hizi dakika 10 (au zaidi!) ambazo zingeweza kurahisisha kazi yetu
ya kusafisha hapo baadaye. Safisha kwanza, na utakuwa na muda wa kupumzika na
kufurahia chakula chako baadaye.
Pimia vyakula ndani ya sinki, na rudisha kila kitu mahali pake
baada ya kukitumia ili kaunta isishamiri vitu. Jitihidi kuwa unafanya
maandalizi yanayotakiwa kabla ya kuwasha jiko. Kama unatumia kikombe au kijiko
cha kupimia, hakikisha unakisuuza papo kwa hapo mara baada ya kukitumia. Futa
vyakula kwenye kaunta kila vinapowagika, hii itasaidia kuzifanya kaunta zako
zisiwe vululu vululu na kukusababishia kazi kubwa ya kusafisha baadaye. Hii pia
inasaidia kuwa na eneo la kutosha kufanyia kazi. Nyanya ndio kiungo
kinachochafua zaidi kaunta. Haiepukiki kupata matone ya nyanya ukutani na hata
juu ya stovu. Kufuta punde kwa kitambaa cha unyevu kunasafisha mara moja, kwa
ajili tone halijakomaa. Kwa chakula ama kiungo chochote kile kilichomwagika
jikoni mwako safisha kabla hayijakaukia kwenye eneo husika. Itasaidia kuokoa
muda na machukizo baadaye.
Hifadhi vifaa na vyakula unavotumia mara kwa mara maeneo ya
karibu na safisha makabati yako ya jikoni na jokofu kwa msimu. Kwa namna hii
hutakuwa na haja ya kuondoa vitu vyote kabatini kwa ajili ya kutafuta kitu
kimoja unachohitaji.
Wakati unapopika tumia vyombo vichache. Kwa mfano, wakati
unapotaka kumenya viazi badala ya
kumenyea maganda kwenye chombo, tumia mfuko au gazeti mbapo utabeba na kutupa
moja kwa moja kwenye ndoo ya taka na hivyo kupungukiwa na chombo cha kuosha.
Kwa siku zile ambazo una muda mchache sana, pika vyakula rahisi
ambavyo havihitaji kutumia sufuria na vikaangio vingi. Fanya mapishi ambayo
chakula zaidi ya kimoja kinapikiwa kwenye sufuria moja, mifano ni mchemsho na
mbogamboga.
Endapo utakuwa na mapishi kwa ajili ya wageni kadhaa nyumbani,
basi gawa kazi yako. Fikiria ni nini unaweza kuandaa usiku mmoja kabla ya ugeni
wako. Hii itasaidia kufanya maandalizi na kujikuta baada ya tukio ukiwa na
vyombo vichache vya kusafisha. Kama utapika maharage kwa mfano, unaweza
kuyasafisha na kuloweka usiku. Halafu unayaacha yamekaa kwenye jokofu, hadi
kesho yake wakati wa kuyapika.
Kupunguza mrundikano kwenye kaunta inafanya wepesi wa kusafisha
jiko lako. Unavyokuwa na vitu vingi kwenye kaunta ndivyo inavyokupasa kuvisogeza
vyote kabla ya kusafisha na hii inakupa kazi kubwa. Baadhi ya watu kanuni ni
kuwa, hakuna kifaa chochote kukaa juu ya kaunta vinginevyo kiwe ni kile tu
kinachotumika kila siku kwa mfano kipashio cha chakula. Vingine vyote kama
visagio na kadhalika vinahifadhiwa kabatini hadi wakati wa matumizi ndipo
vinapotolewa. Usipende vijiko na visu vyako vikae juu vikibeba mafuta mafuta na
vumbi. Viweke kwenye droo lililo karibu na stovu, ili unapovihitaji iwe rahisi
kufungua na kuchuka. Havina haja ya kuwa juu ya kaunta na kula eneo lako la
kazi.
Hizi ni baadhi ya njia za kukuwezesha kuweka jiko safi wakati
ukiendelea kupika. Je, wewe msomaji wangu ni kwa namna gani unaweka jiko lako
safi wakati ukiendelea kupika? Nitafurahi kusikia toka kwako!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
Kaunta yangu ya jikoni imemwagikiwa na mafuta ya kupikia. Nitumie sabuni gani kuondoa mafuta hayo kwani kila ninaposafisha hayatoki
ReplyDeletekaunta yako hiyo imetengenezwa kwa malighafi zipi?
ReplyDeleteNi marble
ReplyDeleteYeah, kwa kaunta ya marble sabuni yoyote yenye lemon itaondoa mafuta. Ila kwa baadhi ya watu wanakosea wanapoona sehemu moja ya jiwe la marble iko tofauti na nyingine na hudhani ni kitu kama mafuta yamemwagikiwa eneo hilo. Ukweli ni kuwa mawe haya hayafanani kila mahali kwenye jiwe zima. Kioo cha marble kinavyoteleza sio rahisi mafuta yakazama ndani hadi kushindwa kusafishika kwa sabuni sahihi.
ReplyDeleteAsante kwa ushauri. Nimekuelewa vizuri
ReplyDeletemy pleasure my d.
ReplyDelete