Mchakato wa kupata gauni la mama wa
bibi harusi.
Kama wewe ni mama, kati ya matukio yenye furaha zaidi ambayo utapenda Mungu
akuonyeshe ukiwa hai ni siku ya harusi ya bintiyo. Mara binti anakuambia mama
nataka kuolewa.
Hongera! Kuna harusi
mbele yako. Siku ambayo binti anaolewa na mwanaume wa ndoto zake inaleta
machozi ya furaha kwa mama yeyote mzaa chema. Kwa furaha yote unayokuwa nayo na
mipango yote unayoanza kupanga kumbuka tu kuwa ni harusi ya bintiyo na sio
yako. Ana mipango na mawazo yake mwenyewe ambavyo angetaka harusi yake iwe.
Sio siri kuwa siku ya harusi ni siku kubwa kwa bintiyo. Lakini usisahau kuwa
ni siku yako pia. Utakaa na marafiki zako na familia yako mpya. Utapigwa picha
na hata utapata nafasi ya kucheza mziki na mtoto wako wa kiume mpya (bwana
harusi). Na
cha muhimu katika yote
unashuhudia binti yako akienda kwa mume kuanza maisha mapya.
Kabla hujasema ndio kwa gauni fulani hakikisha linashinda vigezo vyako
mwenyewe. Nguo yako mama mzaa chema inatakiwa kuwa kama iliyoshonwa maalumu kwa
ajili yako kwa maana ya urefu, ikukae vyema na zaidi ya yote ipitishwe na bibi
harusi. Pia nguo hii ikufanye uonekane mrembo. Ni siku yako ya kung’ara pia. Makala
hii inakupa mawazo ya kukusaidia mama mzaa chema kupata nguo ya kuvaa siku hiyo
maalum maishani.
Kwanza, vaa nguo inayokukaa vizuri,
isipwaye--bila hata kujali rangi hili ndio muhimu zaidi. Tengeneza muonekano
mzuri kwa kuvaa nguo yenye kiuno au hata iliyounganishwa chini ya kifua na
ikamwagika vyema. Huna haja ya kuvaa mburuzo kwa kuwa unaweza kuwa kero kwenye kucheza
na kutembea.
Linapokuja swala la viatu vya siku hiyo chagua vya rangi kama ya silva na
epuka ile sare sare gauni na viatu. Viatu vya kamba vinafaa zaidi wenye umri
mdogo. Chagua kiatu chenye kisigino cha urefu wa wastani. Pia usisahau vitupio
kama hereni, bangili na mkufu mnene wa kuvuta jicho. Hakikisha uvaaji
haukusumbui wakati wa kusalimiana na kukumbatiana na marafiki wanaokupongeza.
Vaa kuendana na umri. Vazi lenye mikono ya urefu wowote linakubalika zaidi
kulinganisha na ambalo halina mikono. Vinginevyo ukichagua kuvaa lisilo na
mikono basi tupia na kimtandio au kikoti kidogo kwa juu.
Ungaro ungaro ukizidi unaweza usikupendeze
kwa umri wako, kumbuka unakuwa mwanamitindo wa hilo vazi kwa ajli ya binti
yako. Atataka kweli kukuona mama yake ukiwa umependeza. Kama binti anakubaliana
na mama kuwa mabega wazi sawa, ila kama anaogopa vichwa kukugeukia kutokana na
uvaaji usiozingatia umri na pengine kumfunika acha awe mchoyo. Ni siku yake sio
yako. Inawezekana kabisa kupendeza bila kuacha sehemu kubwa ya mwili wazi.
Rangi zilizokolea zinaendana na umri mkubwa. Kiukweli bintiyo akiwa anaweka
sahihi kwenye cheti cha ndoa mama unakuwa na hisia mbalimbali. Unaanza kuwaza
tokea akiwa mchanga na kihuzuni kinapenya kwenye mifupa yako lakini mara rangi
ya nguo yako inakupa tumaini/ mng’ao moyoni. Gauni lako lisifanane na la
wasimamizi wa harusi. Ni vizuri kupata ushauri wa rangi toka kwa bibi harusi
ili usijevaa rangi ambayo imekuwa tofauti sana na rangi za harusi. Pamoja na
kuwa rangi ya gauni lako haifanani na ya wasimamizi ila ni vyema ziwe rangi za
familia moja. Inashauriwa kuwa mama mzaa chema aepuke gauni la rangi nyeupe (ni
bibi harusi tu anatakiwa kuvaa rangi hii). Vile vile, nyeusi inakataliwa; laa
kama maharusi wamependa hivyo kwa kuwa inachukuliwa ni rangi ya maombolezo.
Wasiliana na bibi harusi kama kuna rangi maalum za harusi.
Kwa kawaida mama wa bibi harusi
ananunua gauni kwanza na ndipo anapomwendea mama wa bwana harusi mtarajiwa
kiupole na kumwambia juu ya chaguo lake
la nguo. Maelezo utakayompa yatamsaidia kujua avae nguo ya namna gani. Hata
hivyo mawasiliano haya yanatofautiana kutokana na familia. Unaweza pia ukaenda
manunuzi na mama wa bwana harusi mkachagua pamoja kwa ladha yenu. Kujenga
uhusiano huu wa mwazoni itasaidia sana familia zenu mbili huko mbeleni hasa
watoto watakapopatikana.
Nyie wamama wawili mvae kila mmoja
apendeze kwa ladha yake kwa kuwa sio mashindano. Wala mmoja asionekane kuwa
kiongozi au bosi juu ya mwingine kwa suala la mavazi ya siku hiyo. Hata hivyo
mama wa bwana harusi huenda akakushukuru wewe mama wa bibi harusi kwa kumpa
dondoo za nguo utakayovaa.
Kwa familia zenye talaka mama wa binti usijali
kuhusu mama wa kambo wa bwana harusi. Bwana harusi mwenyewe ataongea na huyo mama
yake mlezi kumtaarifu juu ya mavazi. Usimkwaze mama mzazi wa bwana harusi kwa
kuonekana unaungana na mke wa mtalaka wake.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23