Nimekuwa
nikiulizwa hili swali mara kwa mara na wasomaji wangu kuwa ni kwanini mwenye
kupendezesha nyumba yake aamue kutumia stika ukutani badala ya wallpaper. Na
leo nitalijibu kama ifuatavyo. Stika na wallpaper zote zinapendezesha kuta na
zinakidhi malengo fulani kwenye kuta za nyumbani kwako.
Hapa
ni
dongoo muhimu za kuzingatia kati ya tofauti ya kupamba kwa stika badala ya wallpaper
wakati unapoamua kupendezesha kuta.
Lengo: Wallpaper kama
jina lake lilivyo kwamba ni karatasi za ukutani zinabandikwa kufunika ukuta wote
wa eneo unalobandika, wakati ambapo stika inafunika pale ilipobandikwa tu na
sehemu nyingine yote ya ukuta iliyobaki inakuwa wazi. Tofauti na wallpaper,
stika zina tabia ya kuupa ukuta hisia ya sanaa na ni nyembamba sana kiasi kwamba zinashikana
na ukuta kabisa. Bila kuchunguza kwa umakini na kugusa unaweza kudhani ni
mchoro uliochorwa moja kwa moja ukutani. Kwahivyo kama unataka kugusa maeneo fulani
tu ya ukuta na sio ukuta mzima basi stika ndio chaguo sahihi. Ila wakati huohuo
kama unataka kufunika ukuta wote basi chaguo sahihi litakalokidhi lengo lako
hilo ni wallpaper.
Ukubwa: Stika ni ndogo
ndogo na ziko kwenye mfumo wa ua moja moja ambalo limekamilika. Zinapendeza zikibandikwa
pembeni mwa luninga ambapo sehemu kubwa ya ukuta imefunikwa na kabati au shelfu
kiasi kwamba sehemu hiyo haionekani wazi kwa hivyo hakuna haja ya kubandika chochote
kwani hakitaonekana hata hivyo. Kwa upande wa wallpaper kama nilivyosema ni kwamba
inakupasa kuibandika ukuta mzima hata zile sehemua ambazo zitafunikwa kwa
fenicha nyingine.
Gharama: Kwa kuwa stika
ni kwa ajili ya sehemu fulani ndogo tu ya ukuta ni wazi kwamba gharama yake ni
nafuu kuliko ya wallpaper. Pia stika zina wigo mpana wa rangi na maua ya
kuchagua na hazikupi changamoto kubwa ya kuoanisha na mapamba mengine ya
chumba. Ni rahisi kwa stika kujenga timu na saa ya ukutani, fremu ya picha na
sanaa nyingine. Kwahivyo kuleta muonekano wa mandhari nzuri ya ukuta na urahisi
kwa kukontroli unachoongeza au kuondoa ukutani basi bandika stika badala ya
wallpaper.
Ubandikaji: Hata kama hujui
ukielekezwa mara moja tu ni rahisi kubandika mwenyewe stika uliyonunua. Iwe
unaibandika sebuleni au kwenye chumba cha watoto. Kwa upande wa wallpaper sio
rahisi uweze kubandika mwenyewe kama hujawahi kujaribu mara kadhaa. Kwani kuna
matumizi ya vipimo, gundi na ulinganishaji maungio ambao unahitaji utaalam na
uzoefu. Pia endapo unataka kubadili muonekano baadaye ni rahisi kufanya hivyo kwa
ukuta uliobandikwa stika zaidi ya ule uliobandikwa wallpaper. Uondoaji na
maandalizi ya ukuta kwa upande wa wallpaper unahitaji muda.
Nifuate instagram @vivimachange
No comments:
Post a Comment