Tuesday, February 12, 2013

My article for newspaper: Jinsi ya kupata kitanda sahihi


Jinsi ya kununua  kitanda kitakachokufaa

Katika maisha haya ya kuchoka sana, kitanda cha kukupa starehe ndio kila mmoja wetu anahitaji. Baada ya kazi nyingi mno na uchovu, sote tunataka usiku wa mapumziko na starehe. Kitanda cha namna hii hakikupi tu hamasa ya kuanza siku ya kesho yake bali pia kinakupa nguvu ya kupambana na mabaya ya maisha. Inawezekana hukuwahi kufikiria hivi kabla, lakini ni lazima ukubali kuwa kitanda ni moja kati ya vitu muhimu zaidi kwenye maisha yetu. Hii ndio maana kabla ya kununua kitanda unatakiwa kuwa na uhakika wa unachohitaji kutokana na kitanda hicho.  Starehe, uimara na mtindo ni vitu vya kuzingatia katika kujipatia kitanda kitakachokufaa. Fuatana nami katika makala hii ujionee jinsi ya kujipatia kitanda sahihi kwako.

Inawezekana umeshaona aina kadhaa za vitanda kwa nyumbani kwa majirani zako au kwa rafiki, fikiria kwa undani kama kuna mtindo ambao umekugusa. Ni vyema kununua kile ambacho moyo wako umekuwa ukitamani.  Baadhi ya watu wanapendelea vitanda vya mbao na wengine wanakuwa na furaha wakiwa na vitanda vya chuma.

Mara zote cheki ni aina gani ya godoro litakalofaa kwa kitanda unachotaka kununua kwa kuwa mengine yanaendana na  muundo wa kitanda wakati yapo ya kufiti kwenye kitanda chochote. Pia hakikisha saizi ya godoro lako litatosha kwenye msingi wa kitanda husika.

Ni kawaida kwa mtu kuwa na ufahamu binafsi wakati anajaribu kitanda kwenye duka la muuzaji, na wanunuzi wengi huwa wanajaribu kitanda kwa kukilalia mara moja na kuamka. Lakini ili uwe na uhakika kuwa kitanda na godoro ni sahihi kwako, unatakiwa ulale kwa pozi mbalimbali kwenye kila kitanda kama unavyolala usiku  kwa muda wa  si chini ya dakika tano.
Kama umechagua kitanda  cha aina fulani, hakikisha unacheki kabisa hali yake ya starehe. Kama kitanda hakikupi starehe hutakaa ukitumie kwa furaha. Haina maana kununua kitanda hicho ambacho hakitakuwa na matumizi kwako hapo baadaye kwa sababu tu eti umependa mtindo na muundo wake. Tafuta kingine ambacho kitakupa starehe unayoitaka. Kwa mfano, ni kuwa unatakiwa kuchagua kitanda ambacho kina urefu wa inchi 4-6 zaidi ya urefu wa mtu mrefu zaidi atakayelalia kitanda hicho.

Uimara wa kitanda husika ni kigezo muhimu.Ni ukweli kuwa unawekeza hela nyingi kwenye kitanda, sasa ina maana gani kununua ambacho ni dhaifu na kitavunjika siku za karibuni. Kwahiyo ni vyema ukawekeza hela zako hizo kwa kitanda imara ambacho kitadumu miaka nenda rudi kwani kitanda sio kitu cha kununua kila mara.

Zaidi ya yote swali muhimu la kujiuliza ni kuwa ni kitanda cha ukubwa gani kitatosha chumba chako kwa nafasi iliyopo. Kama kitanda hiki ni kwa ajili yako na mwenzi wako ni vyema mkakubaliana wote wawili kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi. Ni lazima mfikirie pia kama kunaweza kuwa na kitanda kitakachofaa zaidi ya hicho mnachotaka kununua. Kama eneo ni dogo ni vyema mkafikiria kununua kitanda chenye sehemu ya kuhifadhia. Kitanda cha kuhifadhia hakina tofauti kubwa na hivi vya kawaida vilivyozoeleka na wengi bali tu ni kuwa kina sehemu ya kuhifadhia mithili ya droo chini ya godoro na vingine vina shelfu zilizojengewa kwenye ubao wa kichwani hivyo kuondoa haja ya kuweka vimeza vya kando.

Mwisho kabisa kama una matatizo ya mgongo aina ya kitanda unachohitaji nayo inahusu.  Kama kuna aina yeyote ya kitanda itakayokusaidia kwa hali yako hiyo basi nunua. Kama mtu ni mlemavu au mgonjwa  na anatafuta kitanda cha kumsaidia katika hali yake hiyo ni wazo zuri. Kitanda ni kati ya vitu vya manunuzi ya hela kubwa yanayofanywa kwa matumizi ya nyumbani. Sio tu kinawezesha kupata usingizi mnono bali kinahusika pia na afya ya mgongo wako. Maumivu ya mgongo yanaweza kufanya maisha ya watu  kuwa ya taabu, bali kuwa na kitanda sahihi kwa mgongo wako italeta tofauti kubwa.

Manunuzi ya kitanda imara ni ya pesa nyingi, kwa hivyo fikiria kwa kina juu ya nini unachotaka kabla ya kufanya uamuzi. Unapendelea mbao, chuma, ngozi ama kitambaa? Hakikisha unalinganisha na kushindanisha mauzo ya vitanda mbalimbali kabla ya kufanya  uamuzi wa mwisho.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023

1 comment:

  1. Vivi asante kwa elimu nzuri ya mambo haya, mara nyingi tunapuuzia vitu hivi.Endelea kutuelimisha mama!!.Vale

    ReplyDelete