Hakuna anayetaka kusafisha bafuni, lakini ukisafisha
kila unapotumia, kazi inakuwa na maumivu kidogo kuliko kuacha hadi wakati wa
usafi mkubwa. Makala hii itakujuza ni jinsi ya kuweka kuta, bafu, sinki, bomba,
eneo la kuogea na bakuli la choo nadhifu kila wakati.
Unapoanza kusafisha bafuni, kwanza ondoa vitu vyote
vya kuhamishika kama vile vizulia, tenga la nguo chafu, kimeza au kikabati na
kindoo cha taka.
Baada ya hapo ondoa buibui kwenye
kona za dari ikifuatiwa na kufuta vumbi mlango kwa nje na ndani. Kwa ujumla
wakati wa kusafisha chumba anzia juu kushuka chini. Ruhusu taka za vumbi na
buibui zimwagike sakafuni kwa ajili utasafisha mwishoni. Kitambaa cha kufutia
kinafaa sana kwa kazi hii japo pia waweza kutumia fagio.
Mimina blichi ama sabuni za
kusafishia kwenye bakuli la choo na iache iondoe uchafu taratibu.
Weka dawa ya unga wa kusafishia zile sehemu ambazo
zina uchafu. Kama kuna uchafu umejijenga kwenye lile eneo la kuogea, sinki ama
pembeni na bomba weka unga wa kusafishia halafu sugua taratibu kwa brashi.
Ukiacha unga huu ukae kati ya dakika 10 hadi 15 wakati ukifanya jambo jingine itaruhusu
kulainisha uchafu. Hakikisha unasoma maelezo ya dawa ya kusafishia ili kuwa na
uhakika unatumia kiasi sahihi ambacho hakitaharibu maeneo yako. Pia ni vyema
kujaribu dawa eneo dogo kabla ya kusafishia eneo kubwa.
Paka sabuni au dawa nyingine za kusafishia kwenye kuta
za bafu kama ni za marumaru. Kwa kutumia sponji ama brashi sugua sehemu uliyoweka
sabuni. Isuuze vizuri kuondoa michirizi yoyote michafu na kama ukuta ni wa
karibia na sinki ama bakuli la choo ukaushe kwa taulo. Ukuta wa sehemu ya
kuogea unaweza kuuacha bila kuukausha. Ni vyema kuvaa glovu wakati wa kusugua
kwani baadhi ya madawa na sabuni zinaweza kuchubua ngozi.
Safisha bomba la kuogea ambalo sio siri kuwa
wasafishajiwengi huwa hawakumbuki kusafisha. Bomba inatumika tu kusafishia
kwingine ila yenyewe inasahaulika kusafishwa. Ni kama msemo wa mshumaa kujiunguza
kumulikia wengine! Kwa sababu hiyo utakuta kwenye bomba na vichwa vyake
kunakuwa na uchafu wa sabuni zilizogandian. Hali huu huweza ikasababisha makazi
ya vijidudu.
Pazia la bafuni huwa linaandamwa na ukungu eneo
linalogusana na sakafu. Ni vizuri zaidi ukalifungua na kulifua kwenye maji ya
moto kwa kiasi kidogo cha sabuni na blichi. Kumbuka adui nambari moja wa ukungu
ni blichi. Kiasi kidogo kitaondoa uchafu bila hata kusugua.
Angalia eneo la sinki na sugua mabaki ya sabuni na
dawa za mswaki kwa sabuni kidogo pamoja na sponji au brashi. Mswaki wa zamani
unaweza kutumika kuondoa uchafu kutoka eneo la kati ya bomba na mishikio yake. Kuwa makini kuwa brashi
la kusugulia bakuli la choo lisitumike kusugulia sinki. Hii inaweza kusambaza maradhi kwa
kuruhusu vijidudu vya kwenye choo kuingia kwenye sinki la mswaki. Kuzuia hali
hii isitokee, brashi la bakuli la choo liwe la peke yake. Ni muhimu kutumia
blichi kusafishia bafuni ili kusaidia kuua vijidudu.
Safisha kioo kwa kutumia ama maji na taulo au dawa
ya kusafishia vioo na taulo.
Safisha nje ya choo ukianza na ile sehemu ya juu ya
kuvuta maji, taratibu endelea kusafisha eneo lote la nje ya choo ambalo ni
pamoja na mfuniko na eneo la chini ya pale pa kukalia na futa kwa taulo. Kumbuka
kitaulo hiki kimetengwa kwa kusafishia choo pekee.
Sugua ndani ya bakuli la choo kwa brashi yake halafu
vuta maji. Huna haja ya kusugua kwa nguvu nyingi. Acha sabuni na dawa ya
kusafishia ikufanyia kazi hiyo.
Sasa ni wakati wa kusafisha sakafu ukinanzia na zile
sehemu zilizojifisha hadi zile za wazi. Safisha mavumbi yote na uchafu wote
ulio chini na pale eneo la choo lilipounganika na sakafu. Eneo hili kwa kawaida
huwa ni chafu sana na lile bomba la nyuma linajaa mavumbi. Malizia kwa kusuuza kwa
maji masafi kuondoa sabuni itakayoweza kubaki na kusababisha utelezi.
Subiri kidogo sakafu ikauke ndipo urudishe vile vitu
ulivyoondoa awali.
Ili kuweka bafu lako katika hali ya usafi na
kupunguza kutumia nguvu kubwa ya kusafisha unatakiwa uwe unasafisha maeneo
mbalimbali ya bafu mara baada ya kuyatumia. Kwa mfano safisha bakuli la choo
kila baada ya kulitumia, vile vile eneo la kuogea pamoja na sinki. Hata kama
sehemu hizi hazionekani kuchafuka safisha tu kwani madini yaliyoko kwenye maji
nayo yaweza kufanya alama. Kama utafanya hivi, usafi mkubwa utakuwa na maumivu
kidogo kwani uchafu hautakuwa umejijenga.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
Dawa gani nzuri ya kung'arisha choo?
ReplyDeletehuwa natumia harpic na sijawahi kujutia hela yangu. inafanya vizuri kwa kweli
Delete