Chumba chako cha kulala ni
sehemu ambayo unalala, kwahivyo ni muhimu pawe katika mazingira ya kupumzikia.
Wakati huohuo unataka pawe eneo la kufanyia shughuli mbalimbali zinazotakikana
kufanyikia hapo kwa mfano kujiandaa kwa ajili ya kutoka asubuhi. Jinsi ambavyo
fenicha zimepangwa italeta matokeo chanya au hasi kwa mazingira ya chumba chako
cha kulala. Kitanda ni fenicha nambari moja kwa chumba chochote cha kulala na
kwa asili ndio kitovu cha jicho linakotazama.
Vyumba vya kulala
vinavyotumika na watu wa kundi fulani vina mahitaji ya kipekee kwa kundi hilo.
Iwe unapanga chumba cha kulala cha wakuu wa familia, cha mgeni au cha watoto
makala hii itakupa dondoo za jinsi unavyoweza kupangilia.
Iwapo
unapanga chumba cha kulala cha wakuu wa familia (kumbuka kuwa chumba hiki sio
lazima kiwe ni kikubwa zaidi kama wengi wanavyodhani) kinachotakiwa tu ni kuwa
na vifaa muhimu vinavyohitajika mule. Na kama chumba chako ni kidogo zaidi ya
ambavyo ungependa, fikiria mbinu za kukifanya kiwe kikubwa kama vile kuondoa
mrundikano na kuweka fenicha, pazia na malazi yenye rangi za mwanga kwani zinafanya
chumba kionekane kikubwa.
Tukiachana na ukubwa wa chumba cha kulala cha wakuu
wa familia, dondoo hizi zitakusaidia kukifanya kiwe sehemu bora zaidi ya
mapumziko. Weka vimeza vya pembeni mwa kitanda vyenye ukubwa wa kuendana na
eneo lako. Kama unatazama luninga ukiwa kitandani utagundua kuwa vimeza hivi
vitakusaidia. Tafuta eneo japo kwa kiti kimoja au viwili vya kukalia. Viti
vinasaidia sana siku ya ugonjwa, kupumzika mchana au wakati wa kusoma. Fikiria
kuweka zulia sakafu yote ya chumba hiki ili kuondoa kelele za fenicha na nyayo kwenye
chumba. Kama una nafasi si mbaya kuweka deski kwa ajili ya kukaa na kuandika
chochote.
Kwa upande wa watoto wanaoingia
kwenye rika la ujana huwa wanajua ni nini wanachotaka kwenye chumba chao cha
kulala, na hawachelewi kukuambia wewe mzazi au mlezi wanahitaji sehemu ya
kuhifadhia vitabu na muziki ama eneo lao lingine la kuhifadhia vitu vyao
vingine vyovyote unavyoweza kudhani.Wana mawazo yao kuhusu mpangilio na rangi,
kwa hiyo waulize!
Pilika nyingi zaidi ya kuperuzi
mitandao na burudani zinafanyika kwenye chumba cha kulala cha watoto wa rika
hili la kuingia kwenye ujana. Viti vya ziada na vimeza vitawezesha eneo la
wageni wao. Weka fenicha zitakazotumika na rahisi kutunza.
Vyumba vya
kulala vya watoto wadogo viwekwe fenicha kwa kufikiria miaka yao ijayo. Ila
mwanzoni, hakikisha unaweka eneo la kuwabadilishia karibia na kitanda. Kwenye
chumba hiki hakikisha usalama unapewa kipaumbele. Usiweke kitanda karibia na
dirisha kama dirisha hilo linafunguliwa mara kwa mara. Mara nyingi kuweka
kitanda katikati kama chumba kina nafasi kubwa huwa ndio mpangilio mzuri zaidi. Ila kama nyumba yako
ina viyoyozi na madirisha hayahitajiki kufunguliwa basi unaweza kuweka kitanda
chini ya dirisha.
Hakikisha mtoto hawezi kuanguka toka
kitandani. Hakikisha droo za chumba
hiki ni laini kufunga, kwa mfano endapo mtoto atakuwa amefungua kwa bahati
mbaya basi reli zitateleza zenyewe na droo kufunga. Zikiwa ni droo ngumu
kufunga mtoto anaweza akanyanuka droo ikiwa wazi na kona yake ikamtoboa
kichwani. Vitasa vya milango na mikono ya makabati visiwe na ncha kali kwenye
chumba hiki. Ikiwezekana funika swichi za umeme na nyaya zisisambae sakafuni.
Kuwa na chumba
cha mgeni kunamfanya mgeni wako kuwa huru zaidi ugenini na hata wewe mwenyeji
wake. Unaweza kupanga chumba cha kulala cha mgeni kwa kitanda sahihi na vifaa
vinavyohitajika na kukisahau. Hakikisha kuwa mgeni wako ana sehemu ya kutosha
ya kuhifadhia, seti mbili za shuka, mito na komfota au kava la duveti.
Kwa
kufanya haya utakuwa umeweka mpangilio wa kufaa kwa kila chumba cha kulala kwa
watu wa kada mbalimbali walioko ndani ya familia yako.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment