Jinsi ya kutandika kitanda ili kionekane nadhifu na maridadi
Linaweza kuonekana ni jambo rahisi
ila kufahamu mbinu za kutandika kitanda kionekane nadhifu na maridadi ni faida
ya kila mmoja iwe ni mtu wa umri mdogo au wa makamo na awe ni mwanaume au
mwanamke. Kuwa na kitanda kilichotandikwa vyema sio tu kinaonekana nadhifu,
bali pia unajisikia vizuri wakati ukifunua shuka kwa ajili ya kulala usiku.
Kitanda nadhifu kinaleta burudiko la moyo vilevile, kwa ajili kinaleta hisia ya
utulivu na muonekano wa kuwa na mapangilio chumbani. Kitanda kilichotandikwa
nadhifu pia, ni nadra kuanza kuhangaika kupanga shuka wakati wa kulala na hii inamaanisha
amani zaidi na muda mchache wa kupambana na shuka na blanketi.
Awali ya yote ondoa malazi yote (
shuka na blanketi au komfota) pamoja na mito kitandani. Chukua shuka safi
ambazo zinafiti ukubwa wa kitanda chako. Kama shuka zako ni zile za seti ya shuka
moja ya kufitisha (hii ni ile yenye mipira kwenye kona zake) na ya pili ni flati
(haina mipira), basi chukua hii ya mipira na ifitishe kwenye kona nne za
godoro. Shuka hizi za kufitisha zinarahisisha sana utandikaji wa kitanda hasa
kama saizi ya shuka na godoro ni sawasawa. Huna haja ya kunyoosha kusawazisha
mikunjo kwani huwa inajisawazisha yenyewe ukishavalisha kwenye kona za godoro.
Kama ni saizi sawa na godoro itafiti vizuri kabisa.
Baada ya hapo juu ya shuka ya kwanza
tandaza ya pili ambayo ni ile flati kwa jinsi ambayo upande wenye pindo kubwa
unakuwa kichwani na ule wa pindo dogo unakua miguuni. Hakikisha shuka hii inaning’inia
ukubwa sawa kwenye pande zote za kitanda ikifuatiwa na kuichomekea kwenye
godoro sehemu za miguuni wakati maeneo la kichawani na pembeni yakiachwa bila
kuchomekewa.
Tandaza blanketi juu ya shuka ya
flati ukilinyoosha vizuri kwa kadri unavyosogea. Ruhusu urefu kiasi wa blanketi
kwa ajili ya kuchomekea miguuni. Kunja blanketi eneo la kichwani ukiwa umelishikisha
pamoja na lile shuka la flati urefu wa saizi ya upana wa mto mkubwa wa
kitandani. Baada ya kukunja chomekea kwa pamoja blanketi na shuka kwenye pande
mbili ndefu za kitanda.Kama kitanda kinatumika kila siku utandikaji huu ni njia
rahisi kwa mlalaji kufunua upande anaopandia kitandani, shuka ya juu iliyokunjiwa
na blanketi na kuingia kitandani kulala. Ila kama kitanda husika hakitumiki
mara kwa mara, kwa mfano kama ni kitanda cha chumba cha mgeni unaweza
kufunika kwa kuchomekea kote kote na juu
yake kuweka kava la kuzuia vumbi hadi mgeni atakapotembelea.
Sasa basi endapo kitanda
tunachotandika ni kwa ajili ya matumizi ya kila siku njia ya kukunja shuka na
blanketi ni utandikaji utakaofaa zaidi. Eneo la kichwani mahali ambapo pamekunjiwa
blanketi, lile shuka la kufitisha litakuwa linaonekana kwa hivyo chukua mito na
weka juu yake. Huenda unahitaji mito
miwili tu kwa ajili ya kulalia, ila unaweza kuongeza mito kadhaa midogo midogo kama
mapambo kukipa kitanda mvuto.Unaweza kuweka mito mitano hadi sita kuendana na
ukubwa wa kitanda chako. Kanuni ya kuweka mito kitandani ni kuwa lile eneo la
kichwani lisibaki na uwazi wa ukubwa wa mto. Kwa maana ya kwamba kama kuna
uwazi wa kutosha mto uliobakia basi ongeza mto. Kwa mmoja namna hii ya utandikaji
inaweza kuwa mwisho na akajiridhisha kitanda kimekamilika na kina mvuto, ila
kwa mwingine anaweza kupenda kuongezea komfota.
Kwa hivyo kama wewe ni mmoja wa
wanaopenda kutandika komfota kitandani basi litandaze juu ya blanketi huku
ukilinyoosha vizuri kuondoa mikunjo yote inayoweza kutokeza. Huna haja ya
kuchomekea komfota na huwa lenyewe ni njia mojawapo ya kupamba kitanda – liache
tu likining’inia urefu unaolingana kwenye pande zote za kitanda na hapo kitanda
kinakuwa kimemalizika kutandikwa.
Kuna baadhi yetu ambao hatuoni
umuhimu wa shuka ya pili. Uzoefu wa kutumia shuka moja (ikiwa ni ile ya
kufitisha ni bora zaidi) na komfota pekee inafanya utandikaji wa kila siku wa
kitanda uwe rahisi, ila kiukweli ni kuwa hii shuka ya pili inaulinda mwili wa
mlalaji usikwaruzwe na ugumu wa blanketi au komfota na pia husaidia kuweka blanketi
au komfota safi na bila kusahau kuongezea mwili joto. Ni rahisi zaidi kufua
shuka mara kwa mara kuliko blanketi au komfota, na pia makava haya ya kitanda
yanadumu zaidi yakifuliwa mara chache.
Kutumia shuka ya flati ambayo ina
ukubwa wa kutosha inafanya kitanda kiwe rahisi kulalia na kutandika tena
asubuhi ya pili. Tumia shuka na blanketi zenye ukubwa wa kutosha kiasi kwamba
havitachomoka chomoka ukiwa umelala. Kama una blanketi dogo ni bora kulikunja na
kuliweka chini ya mito na ukawa unalikunjua na kujifunika wakati wa kulala tu
kwa maana ya kwamba wakati wa kutandika unalikunja kwani ukiamua kuchomekea blanketi
dogo litakusumbua kwa kuchomoka kila mara.
Zaidi ya kutandika safisha chumba
chako cha kulala ili kuonyesha zile juhudi zako za kutandika. Kitanda pekee
kikiwa maridadi ilhali sehemu ya chumba iliyobaki ni mrundikano unadhifu
hauwezi kuonekana. Kutandika kitanda kunakuwezesha kuanza siku yako vizuri na kunakufanya
ujiikie kuwa na mpandilio zaidi mapema mwa siku yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi
Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni
mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment