Jinsi ya kung’arisha nguo nyeupe
Sababu kadhaa zinaweza kufanya nguo nyeupe zipoteze
weupe wake. Huenda utafuata kanuni za utunzaji wa nguo nyeupe, lakini bado
zinaweza kubadilika na kuwa na rangi ya njano baada ya muda. Unjano mara nyingi
unatokea kwenye nguo ambazo hazijahifadhiwa vizuri kwa kugusana na mbao au bodi
za kabati.
Haiepukiki kuwa baada ya muda nguo hupata udongo na kuanza
kuonyesha uchakavu. Nguo nyeupe ni chambo cha madoa, na madoa hayo huonekana
zaidi ya nguo yenyewe. Habari njema ni kuwa nguo nyeupe hata iwe imendamwa na
madoa kwa kiasi gani, bado inaweza kuokolewa.
Soma makala ifuatayo ambapo Aisha Idd ambaye ni mtaalam wa kufua
anatujuza namna tunavyoweza kurudisha tena uhai wa nguo nyeupe. Anasema kuna
njia kadhaa za kuweza kuzing’arisha tena. Baadhi ya njia zinaweza kuharibu
vitambaa laini kwa hivyo kuwa makini.
Unatakiwa kufua nguo nyeupe mara kwa mara. Madoa yanavyokaa
kipindi kifupi, ndivyo ilivyo rahisi kuyaondoa. Hii hasa inahusu kwa njano ya
kikwapa itokanayo na kutokwa jasho na deodoranti. Weka dawa ya kuondoa madoa
kwenye maeneo haya na mengine yenye madoa kabla ya kufua nguo nzima.
Njia ya kwanza na iliyozoeleka na wengi ya kung’arisha nguo
nyeupe ni kuweka blichi wakati wa kufua. Blichi ya klorini inashauriwa kutumika
zaidi kwa kipimo kilichoelekezwa kwenye chupa na kwenye nguo za pamba. Itumie
tu kwa nguo nyeupe na ambazo zinaruhusu blichi. “Hakikisha unasoma lebo ya nguo
kabla ya kuamua kutumia njia fulani ya kuing’arisha,” anasema Aisha. Kuna nguo
hata kama ni nyeupe ila lebo yake inasema usitumie blichi.
Pia blichi ikizidi inaweza kuharibu nguo na wakati mwingine
kuleta mistari ya njano kwenye nguo nyeupe kwa hiyo kuwa makini na kiasi cha
blichi kinachotakiwa kuchanganywa na maji. Wakati mwingine yapasa kuloweka nguo
zako kwenye maji yenye blichi kwa usiku mzima.
Unaweza kuweka rangi ya bluu kwenye maji ya kusuuzia
ili kufanya nguo zako nyeupe zing’ae.
Unachotakiwa ni kufuata maelekezo kwenye chupa ya bluu. Bluu inaongeza
ubluu kwenye nguo ambao unaifanya ionekane nyeupe zaidi na ing’ae. Bluu
inatakiwa kuwekwa na maji ya baridi.
Kuanika nguo nyeupe zikauke juani ni njia mojawapo pia ya
kuzingarisha. Kwenye jua kuna mionzi ya UV ambayo inafanya nguo nyeupe izidi
kuwa nyeupe, anasema Bi Aisha. Bila shaka! Mwanga wa jua ni zana mojawapo kuu
ya asili tuliyonayo ya kufanya nguo nyeupe zizidi kuwa nyeupe bila kutumia
kemikali.
Vinega;
ndio vinega hii hii unayoifahamu pamoja na sabuni yako ya kufulia vitang’arisha
nguo zako nyeupe. Vinega ni kilainishi na marashi ya nguo, hii inawekwa kwenye
maji wakati wa kusuuza. Usijali harufu kwani nguo zako hazitanukia kama vinegar
bali harufu itapotea juani wakati wa kukaushwa.Vinega hii nyeupe pia inasaidia
kuondoa mabaki ya sabuni kwenye nguo. Onyo: Kamwe usichanganye vinega na blichi
kwani inafanya kemikali hatari kwa nguo zako, anasema Aisha.
Juisi
ya ndimu ni njia nyingine ya asili ya kung’arisha nguo nyeupe. Weka nusu kikombe
cha chai na sabuni kwenye maji ya kufulia (hata kama unafua kwa mashine) na
endelea kufua nguo nyeupe kama kawaida. Itumie tu kwenye nguo nyeupe kwani
inaweza kuharibu nguo za rangi.
Magadi soda (Baking Soda)
nayo inaleta matokeo ya ajabu kwenye kung’arisha nguo nyeupe bila kutumia
blichi. Hii pia weka nusu kikombe cha chai pamoja na sabuni yako ya kufulia.
Nguo zitatoka nyeupe na zitang’aa kuliko.
Usishange hii ni moja ya viambato kwenye dawa za meno, ni kwa ajili ya
kuongeza weupe.
Hizo hapo juu ni njia mbalimbali za kufanya nguo nyeupe ziwe
nyeupe zaidi. Zingatia kuchagua sabuni za kufulia ambazo zimetengenezwa kwa
ajili ya kung’arisha na zitumie mara kwa mara kwa matokeo mazuri. Fua nguo nyeupe
kwa maji ya baridi ili kufanya madoa na unjano usizame na kung’angania zaidi
kwenye nyuzi za nguo. Usichanganye njia moja na nyingine pamoja kwani unaweza
kutengeneza kemikali itakayoharibu nguo zako.
Kwa hivyo kwa matokeo mazuri, fua nguo zako nyeupe kwa sabuni za
kawaida za kufulia ukiongeza moja ya njia za kung’arisha hapo juu tulizojuzwa
na Bi Aisha. Halafu tundika nguo zikauke juani. Utashangazwa ni kwa namna gani
zimeng’aa.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment