Umeshaanza
kupata hamasa ya sikukuu? Tunaona mitaani na kwenye maduka makubwa ambavyo
wauzaji wanauza mapambo mbalimbali ya sikukuu huku kwenye majengo makubwa na ofisi
mbalimbali wakiwa wameshaweka tayari mapambo ya mti wa krismasi. Kila mwaka
msimu huu wa sikukuuu duniani kote ni shamarashamra za aina yake.
Nyumbani
kwako huenda tayari unao mti wako wa krismasi au
kama bado, ndio uko kwenye
mchakato wa kuupata.
Kupamba
mti wa krismasi kama mtaalam sio kazi kubwa kivile, na nakuhakikishia baada ya
maelezo haya endapo hukuwa unafahamu namna ya kuupamba utafahamu kila kitu.
Unachohitaji ni mziki wa sikukuu, mti (ambapo watu wengi siku hizi wanapendelea
miti ya bandia), zawadi, mapambo ya kuzungusha, mapambo ya duara, taa za
vimulimuli, nyota moja na kitambaa.
Hatua
ya kwanza ni kuunganisha mti wako na kuusimamisha wima halafu funika kitako cha mti kwa kitambaa cha
rangi ya kijani, nyeupe au nyekundu.
Zungushia taa
za kamba za vimulimuli ukianzia juu ya mti kushuka chini. Kama mti ni wa kijani
(kumbuka siku hizi ipo hata myeupe) chagua taa ambazo waya wake nao ni wa
kijani – hii itasaidia waya ufanane na mti ili kuzifanya taa ndio zichomoze zaidi. Kama baadaye utakuja
kuweka nyota ya mwanga kule kwenye kilele cha mti hakikisha kwenye ncha ya waya
wa taa kuna mahali pa kuichomeka. Endelea kuzungusha taa hadi chini kabisa
mwisho wa majani.
Baada ya hapo chukua pambo lile refu
la rangi za kuendana na mandhari ya mti wako halafu lizungushie tena kwenye mti
mzima. Unaweza kutumia pambo hili likiwa kwenye rangi tofauti kama vile silva
na nyekundu. Mzunguko upishane umbali wa inchi 4 hadi 6 kuendana na ukubwa wa
mti. Kama kawaida anza kulizungushia kuanzia juu kushuka chini.
Halafu chukua vile vipambo vya duara
vya kuning’iniza. Navyo unaweza kuchagua vya rangi kadhaa kama vile bluu,
nyekundu na nyeupe na pia vya ukubwa tofautitofauti. Haya ndiyo mapambo ya
mwisho kwenye mti wako. Yatundike kwa jinsi ambayo unayasambaza kila mahali kwa
umbali unaoendana. Haya yanaruhusu mti kung’aa.
Panda kwenye stuli ndefu au ngazi ya
ndani, pachika nyota moja pale kileleni. Hili ndio pambo la kujivunia na linaloongeza
ladha ya kipekee. Kama ni nyota ya kutumia umeme unganisa na ule waya wa
vimulimuli ili nayo itoe mwanga tofauti tofauti.
Mwishoni kabisa panga zawadi chini
ya mti, ukianza na kubwa zikifuatiwa na ndogo. Zawadi hizo ziwe zimefungwa kwa
riboni na karatasi za kufungia zawadi ambazo zinaendana na rangi za mti ili
kuleta pamoja muonekano uliokamilika.
Mara umekamilisha kuupamba mti wako,
ufurahie! Ila usisahau kuzima vimulimuli wakati wa usiku au ndani kukiwa hamna
mtu.
No comments:
Post a Comment