Tuesday, May 16, 2017

Faida 9 za kuweka sakafu ya mbao

Ingawaje wenye nyumba wengi pamoja na wenye nyumba watarajiwa walionekana kutofuatilia sakafu za mbao kwa sababu tu ni gharama kuliko aina nyingine za sakafu kama vile marumaru na zulia, kwa siku za karibuni kumekuwepo na mwamko wa watu hawa kuanza tena kujenga upendeleo wa kuwa na sakafu za mbao. Ni kweli kuwa pamoja na kwamba utaongeza gharama kidogo ni kuwa kuna faida nyingi za kuwa na sakafu ya mbao. Karibu tuangalie baadhi ya faida hizi kama zinavyoelezwa na fundi wa sakafu hizi bwana Andrew Komba:

1.      Sakafu ya mbao yenye ubora inadumu kwa miaka angalau 15 kabla ya kufanyiwa ukarabati. Wakati watu wengi wanajikuta wakibadilisha zulia kila baada ya miaka mitano, kutokana na madoa, matundu au
tu manyoya kuisha baadhi ya maeneo kutokana na uchakavu, utagundua kuwa sakafu ya mbao inazidi kupendeza kadri miaka inavyosogea.

2.      Ni rahisi kusafisha sakafu ya mbao kuliko ya zulia. Sababu ziko wazi, ufagio tu au dekio la juu juu linafanya sakafu ya mbao ing’ae. Kama watoto wameingiza tope ndani dekio lililoloa kidogo tu linamaliza tatizo kirahisi kabisa. Wenye sakafu za zulia wakati kama huu wangekuwa wakipiga yowe. Ingawa vilevile ni rahisi kusafisha sakafu ya marumaru ila kiusalama wakati ikiwa imeloa ina nafasi kubwa ya kuangusha watu hasa watoto na watu wa umri mkubwa. Na pia bila kujulishwa si rahisi kuona eneo lililoloa. Na kwa swala la matope halipatana kabisa na bidhaa inayounganisha marumaru moja na nyingine yaani grauti.

3.      Sakafu ya mbao ni salama zaidi kiafaya kuliko zulia. Kuna ripoti nyingi za kuogofya kuwa mazulia yamekuwa yakihifadhi vijidudu na vumbi ambapo husababisha mzio hasa kwa watoto wadogo ambao muda mwingi wanakuwa wamekaa chini. Hii pia inahusika kwa nyumba zenye sakafu la zulia huku zikiwa na mbwa au paka ndani.

4.      Sio tu kwamba sakafu ya mbao ni salama zaidi kiafya bali pia hazidaki harufu mbaya kutoka kwa wanyama wa ndani au kivimiminika na vyakula ambayo vimemwagikia. Harufu ya sakafu ya mbao ni freshi na mng’ao wa polishi unafanya nyumba kuwa na mvuto.

5.      Kama isivyo kwa sakafu ya marumaru sakafu ya mbao haina ubaridi na wala huna haja ya kupasha joto miguu kwa kuvaa soksi kama vile ambayo ingekuwa kwenye marumaru hasa nyakati na maeneo ya baridi.

6.      Kama baada ya miaka kadhaa sakafu ya mbao itakuwa na mikwaruzo aidha kutokana na kusogeza vitu au tuu uchakavu wa kawaida, kuita fundi na kujaza kemikali ya sand and seal pamoja na kupaka polishi inairudisha kwenye upya tena. Hii ni gharama nafuu zaidi kuliko kutandaza zulia jipya.

7.      Moja ya faida kuu ambayo watu wanaisahau au hawaijui kuhusu sakafu ya mbao ni ile hali ya kutopitwa na wakati. Mazulia na marumaru yanakuja kwa mitindo mipya kila leo lakini sii kwa sakafu ya mbao. Mbao zimedumu karne na karne na kila siku zinaongezeka thamani na umaarufu.

8.      Ingawaje kale ilionekana kama sakafu ya mbao ni kwa ajili ya nyumba za “wenye nazo”, teknolojia imewezesha njia za uzalishaji ambapo inawezekana kumudu sakafu ya mbao kwa bajeti tofauti tofauti.

9.      Wadau wa nyumba kama vile wajenzi, madalali, wenye nyumba na wapangaji wote wamekiri kuwa nyumba yenye sakafu ya mbao ina thamani mara mbili iwe ni kwa kuuza au kupangisha kuliko nyumba zenye aina nyingine za sakafu.

Kwahivyo ingawa inaweza kukugharimu gharama kidogo zaidi, ila kwa suluhisho la muda mrefu sakafu ya mbao ni bora zaidi. Kutokana na faida hizi 9 fikiria mara mbili kabla ya kufanya uamuzi wa sakafu unayotaka kuweka. Muulize mwenye nyumba yeyote aliyeweka sakafu ya mbao na atakuambia kuwa ni uamuzi mzuri aliowahi kufanya kwenye maisha yake!!


Kwa mahitaji ya sakafu za mbao tuwasiliane 0755200023

No comments:

Post a Comment