Ndani
ya nyumba kuna meza za aina nyingi kama vile meza ya kahawa, meza ya kwenye
korido, meza ndogo za pembeni mwa makochi na
pembeni mwa kitanda bila kusahau meza ya kuvalia na pia wapo baadhi
wenye meza katikati ya jiko. Kati ya meza hizi zote meza ya chakula ndio ina
changamoto kubwa katika kuipendezesha kuliko hizi nyingine. Hii ni kwasababu ya
umuhimu wake kuwa pamoja na kwamba wewe mwenye nyumba au mkaaji unataka meza
yako ipendeze lakini wakati huo huo ikitumika kulia chakula.
Makala
hii itakujuza njia kadhaa za kupendezesha meza ya chakula bila kubughudhi kazi
yake kuu ambayo ni watu kukaa na kula chakula.
Kwanza
kabisa katika kufahamu njia za kupendezesha meza hii ni vyema ufahamu kuwa kuna
maumbo matatu yaliyozoeleka zaidi ya meza za chakula. Maumbo hayo ni meza za
pembe nne, za yai au za umbo la duara. Unapopendezesha meza ni muhimu sana
kuzingatia umbo lake. Kwa mfano trei la duara litaendana na kupendezesha zaidi meza
ya duara na sio ya pembe nne.
Njia
ya kwanza ni kwa kutumia usemi ambao sisi wapendezeshaji tunaita ni nguvu ya
vitu vitatu. Vesi tatu, tepe tatu au mabakuli matatu yaliyowekwa maua au
matunda yawe ni makavu au hai
yakisambazwa katikati ya meza yanaipendezesha na wala hayabughudhi
walaji wakati wa chakula.
Njia
ya pili ni kwa kuweka trei katikati ya meza. Trei hilo unaweza ukalibebesha
vitu vidgodogo kama vile kichupa cha kuhifadhia chumvi ya mezani, vijiti vya
kuondoa nyama katikati ya meno na kiungo chochote ambacho hakihitaji kuwekwa kwenye
jokofu lakini kinatumika wakati wa kula.
Njia
ya tatu ni kwa kuweka mishumaa mwili pamoja na stendi/vibebeo vyake kwenye kila upande wa
meza.
Njia
ya nne ni kwa kutandika utepe wa meza na kuweka bakuli lenye mipira midogo ya
mapambo hapo katikati ya meza.
Njia
ya tano ni kwa kutumia mati za kuwekea sahani. Mati hizi zinatumika wakati wa
kula lakini baada ya hapo meza inafutwa vizuri na zinarudishwa hapohapo mezani
zinakaa muda wote kuwe na mlo au kusiwe na mlo.
Njia
ya sita ni kuweka pambo lolote lenye umbo la chombo au chakula au tunda. Kwa
mfano kuna mapambo ya seramiki yaliyotengenezwa mfano wa birika au tunda kubwa
kama boga na kadhalika. Pambo la namna hii ni kwa ajili ya kuweka kwenye meza
ya chakula.
Njia
ya saba ni ile ambayo ni ya kale ya kutandika kitambaa cha meza. Ingawaje bado
kuna wanaotumia njia hii wengi wanaona kama vile inaficha uzuri wa meza.
Kwahivyo utakuta wenye nyumba wengi wenye meza za kuvutia aidha wanatumia
kitambaa wakati wa chakula tu lakini baada ya hapo kinaondolewa na meza
kupambwa kwa kutumia moja kati ya hizi njia nyingine.
Msomaji
wangu hizo ni baadhi ya njia za kupendezesha meza ya chakula, usikubali ya
kwako ibaki shaghalabaghala badala yake tumia njia moja ua mbili kati ya hizo.
No comments:
Post a Comment